KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Sunday, October 21, 2012

YANGA YAZIPUMULIA SIMBA NA AZAM




LICHA ya kuwa nyuma kwa mabao 2-0, Yanga jana ilizinduka na kuicharaza Ruvu Shooting mabao 3-2 katika mechi ya ligi kuu ya Tanzania Bara iliyopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Ushindi huo umeiwezesha Yanga kufikisha pointi 14 baada ya kucheza mechi nane na hivyo kuchupa hadi nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi hiyo, ikiwa nyuma ya Simba na Azam.
Mashabiki wa Yanga walijikuta wakinyong'onyea dakika 10 za mwanzo za pambano hilo baada ya Ruvu Shooting kufunga mabao mawili ya haraka haraka kupitia kwa Seif Abdalla.
Yanga ilihesabu bao la kwanza kupitia kwa beki wake, Mbuyu Twite aliyefunga kwa mpira wa adhabu ya moja kwa moja uliowapita mabeki na kipa Benjamin Haule wa Ruvu Shooting na kujaa wavuni.
Jerry Tegete aliiongezea Yanga bao la pili dakika chache baadaye, akiunganisha wavuni mpira wa krosi uliopigwa na beki Juma Abdul. Timu hizo zilikwenda mapumziko zikiwa sare ya mabao 2-2.
Didier Kavumbagu ndiye aliyeifungia Yanga bao la tatu na la ushindi baada ya kutokea kizaazaa kwenye lango la Ruvu Shooting.
Katika mechi nyingine ya ligi hiyo iliyochezwa jana kwenye Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga, wenyeji Coastal Union waliendelea kujiimarisha nafasi za juu katika msimamo wa ligi hiyo baada ya kuibanjua Mtibwa Sugar mabao 3-1.

No comments:

Post a Comment