'
Wednesday, October 24, 2012
GUARDIOLA, CAPELLO WAMMWAGIA SIFA FALCAO
MADRID, Hispania
MSHAMBULIAJI Radomel Falcao wa klabu ya Atletico Madrid ya Hispania yupo njia panda baada ya klabu za Chelsea ya England na Real Madrid kumtolea udenda huku zikipigana vikumbo kuwania saini yake.
Mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Colombia kwa sasa ndiye tegemeo kubwa la Atletico Madrid, ambayo imeshatamka wazi kuwa haina kipingamizi cha kumuuza.
Atletico Madrid imesema itamuuza Falcao wakati wa usajili wa dirisha dogo Januari mwakani, iwapo klabu inayomtaka itakuwa tayari kulipa ada ya uhamisho ya pauni milioni 45.
Kwa upande wake, Falcao (26) ametoa masharti ya kupatiwa mkataba wa miaka minne na mshahara wa pauni milioni tano kwa mwaka baada ya kukatwa kodi.
Chelsea ndiyo inayopewa nafasi kubwa ya kumsajili Mcolombia huyo kutokana na ukweli kwamba, haitakuwa rahisi kwa Falcao kujiunga na Real Madrid, ambao ni wapinzani wakubwa wa Atletico Madrid.
Chelsea imekuwa na uhusiano mzuri na wawakilishi wa Falcao, akiwemo wakala maarufu, Jorge Mendes.
Hata hivyo, Mendes pia ndiye wakala wa Kocha Jose Mourinho wa Real Madrid na baadhi ya wachezaji nyota kama vile Cristiano Ronaldo.
Iwapo Falcao atasajiliwa na Chelsea, huenda ukawa mwisho wa mshambuliaji Fernando Torres, ambaye alisajiliwa na klabu hiyo msimu wa 2011 akitokea Liverpool, lakini ameshindwa kukidhi kiu ya mashabiki wa klabu hiyo.
Masharti mengine yaliyotolewa na Falcao ni kuhakikishiwa namba kwenye kikosi cha kwanza na Chelsea inaonekana wazi kuwa tayari kukidhi sharti hilo.
Chelsea ilimuhakikishia namba Torres kwenye kikosi chake cha kwanza, lakini kutokana na kushindwa kwake kuonyesha makeke yoyote, imeamua kutafuta nyota wengine wenye uzoefu zaidi.
Mbali na Falcao, wachezaji wengine wanaowaniwa na Chelsea kwa ajili ya kuiongezea nguvu ni Andre Schurrle wa klabu ya Bayer Leverkusen ya Ujerumani.
Chelsea ilianza kuvutiwa na Falcao baada ya kuifungia mabao matatu timu hiyo ilipomenyana na Atletico Madrid katika mechi ya fainali ya Kombe la Super iliyopigwa Agosti mwaka huu mjini Monaco, Ufaransa.
Falcao alisajiliwa na Atletico Madrid msimu wa 2011 akitokea Porto ya Ureno. Mcolombia huyo alimwaga wino katika klabu hiyo kwa ada ya uhamisho wa pauni milioni 35.
Kocha wa zamani wa Chelsea, Andre Villas-Boas alitaka kuondoka Porto akiwa na Falcao, lakini mmiliki wa klabu hiyo, Roman Abramovich alimwekea ngumu, akiamini kuwa Torres angeweza kurithi vyema mikoba ya Didier Drogba.
Atletico Madrid imeshatamka wazi kuwa, uamuzi wao wa kumuuza Falcao utaisaidia kutatua tatizo la kifedha, lakini imedokeza kuwa, huenda asiuzwe wakati wa dirisha dogo.
Mbali na Chelsea na Real Madrid, klabu zingine zilizoonyesha nia ya kumsajili Falcao ni matajiri wa Zenit St Petersburg na Anzhi Makhachkala wa Russia, ambao wapo tayari kulipa kitita kikubwa zaidi cha pesa.
Hata hivyo, Falcao imeonyesha nia ya kutaka kubaki Hispania ama kuhamia England na hivyo kutoa mwanya zaidi kwa Chelsea na Real Madrid kumnyakua.
Majina halisi ya mwanasoka huyo ni Radamel Falcao García Zárate. Alizaliwa Februar 10, 1986 katika mji wa Santa Marta nchini Colombia). Falcao pia ni maarufu kwa jina la El Tigre.
Falcao amekuwa akielezewa na wachambuzi wengi wa soka kuwa ni mmoja wa washambuliaji bora duniani kwa sasa, akiwa ameipiku rekodi ya Jurgen Klinsmann wa Ujerumani ya kufunga mabao 15 katika michuano ya ligi ya mabingwa wa Ulaya.
Mcolombia huyo pia alitoa mchango mkubwa kwa Porto ya Ureno ilipotwaa nafasi ya pili katika michuano ya Kombe la UEFA msimu wa 2010-11. Alikuwa mwanasoka bora wa tano duniani katika kura zilizopigwa na waandishi wa habari barani Ulaya.
Msimu huo huo, Falcao alishinda tuzo ya mpira wa dhahabu baada ya kuibuka mfungaji bora katika ligi ya Ureno, akiwa Mcolombia wa kwanza kunyakua tuzo hiyo.
Katika misimu mitatu iliyopita, aliyochezea klabu za Porto na Atletico Madrid, Falcao aliweka rekodi ya kufunga mabao zaidi ya 100. Pia aliiwezesha Real Madrid kuweka rekodi ya kushinda mechi 12 mfululizo za michuano ya ligi ya Ulaya.
Falcao amerithi kipaji cha baba yake, Radamel Garcia, ambaye alikuwa mmoja wa mabeki wa kutumainiwa nchini Colombia
Kocha Mkuu wa zamani wa Barcelona, Pep Cuardiola aliwahi kumwelezea Falcao kuwa ni mchezaji mwenye kipaji cha aina yake duniani na mwenye uwezo wa kufanya chochote uwanjani.
Kocha Fabio Capello pia amekuwa akimwelezea Falcao kuwa ni mchezaji mwenye kiwango sawa na Lionel Messi na Cristiano Ronaldo na pia kumwelezea kama mmoja wa washambuliaji bora duniani kwa sasa.
Alianza kung'ara kisoka akiwa katika klabu ya River Plate ya Argentina kabla ya kuhamia Porto msimu wa 2009-10, ambayo ilimsajili baada ya kumuuza Lisandro Lopez kwa klabu ya Plympic Lyon ya Ufaransa.
Alianza kuichezea timu ya taifa ya Colombia mwaka 2007 akiwa na umri wa miaka 21 na kuifungia bao katika mechi ya michuano ya Kombe la Kirin dhidi ya Montenegro kabla ya kuifungia bao lingine katika mechi dhidi ya Nigeria iliyochezwa mwaka 2008.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment