KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, October 10, 2012

FLAVIANA MATATA SASA HAKAMATIKI


BARA la Afrika limekuwa chimbuko kubwa la wanamitindo mbali mbali maarufu wa mavazi wanaong'ara duniani hivi sasa katika fani hiyo.
Mbali ya kutoa wanamitindo wanaong'ara kwa miondoko yao stejini, biashara ya mavazi nayo imeongezeka kwa kasi kubwa katika bara hili, ikilinganishwa na miaka kadhaa iliyopita.
Siku hizi, maonyesho ya mavazi yamekuwa yakifanyika kwa wingi ndani na nje ya bara hili kutokana na uwepo wa wanamitindo wenye mvuto na wa kisasa.
Mmoja wa wanamitindo wanaolipamba bara hili katiki fani hiyo ni Flaviana Matata (25), ambaye amejipatia umaarufu mkubwa kimataifa kutokana na mvuto wake awapo stejini.
Hivi karibuni, Flaviana alishika nafasi ya sita kwa ubora katika mashindano ya dunia ya maonyesho ya mavazi yaliyofanyika mjini Mexico City nchini Mexico na kuwashinda wanamitindo kadhaa waliokuwa waking'ara miaka ya nyuma.
Flaviana mwenye urefu wa futi tano na inchi tisa, alizaliwa na kukulia Tanzania na alianza kupata umaarufu baada ya kushiriki na kushinda shindano la Miss Universe Tanzania 2007.
Mtandao wa MSN African umemwelezea Flaviana kwamba, alikuwa mwanamke mwenye mvuto wa pekee katika mashindano ya dunia ya Miss Universe yaliyofanyika mwaka huo na hivyo kuwavutia wabunifu wengi wa mitindo ya mavazi kutoka sehemu mbali mbali duniani.
Kutokana na mafanikio yake, Flaviana amekuwa kivutio kikubwa kwa wasichana wengi wa kiafrika wenye mapenzi na fani hiyo. Umbo lake, sura yake na rangi ya mwili wake ni vitu vyenye mvuto wa aina ya pekee.
Mama wa mwanamitindo huyo alifariki dunia kwa ajali ya meli ya MV Bukoba iliyotokea miaka 16 iliyopita, lakini bado kumbukumbu hiyo huwa ikimjia mara kwa mara akilini.
Pamoja na kujiwa na kumbukumbu hiyo, ambayo humpa simanzi kubwa, Flaviana ameamua kujenga maisha yake kwa kutumia fani ya mitindo ya mavazi.
Mara baada ya kushiriki shindano la dunia la Miss Universe, Flaviana alikwenda Afrika Kusini kuanza kazi ya uanamitindo wa mavazi chini ya usimamizi wa Kampuni ya Ice Models. Baadaye aliingia mkataba na kampuni ya Boss Models.
Ni kuanzia wakati huo, milango ya neema ilifunguka kwa Flaviana. Baada ya kutembelea Marekani na kushiriki kwenye onyesho la hisani la mavazi lililofanyika mjini New York, mbunifu wa mavazi Russell Simmons alibaini kipaji chake na kuamua kumsaidia. Alifanyiwa usaili na mawakala kadhaa wa mavazi wa Marekani kabla ya kuingia mkataba na wakala wa kimataifa wa mavazi, Next Network.
Flaviana ameelezewa na jarida la Essence la Marekani kuwa ni mmoja wa wanamitindo wake bora 10 weusi na makao yake kwa sasa ni mjini New York.
Amekuwa akifanyakazi chini ya Next Network katika miji ya New York, London, Paris, Milan na mingineyo barani Ulaya. Picha zake zimekuwa zikichukuliwa na wapiga picha maarufu kama vile Russell James, Fadil Berisha, Josh Ollin, Mario Torres na Patrick Demarchelier.
Flaviana pia amewahi kuonyesha mavazi ya wabunifu maarufu kama vile Sherri Hill Tommy Hilfiger, Mustafa Hassanali, Vivienne Westwood, Tory Burch, Suno, Louise Gray, Rachel Roy, Charlotte Ronson, Tony Burch na wengineo kadhaa.
Mbali na kuwa bize na kazi za kuonyesha mavazi, Flaviana pia amekuwa akijihusisha na kazi za kijamii. Hivi karibuni aliteuliwa kuwa balozi wa SOS Children Village Tanzania na kutoa elimu kwa vijana kuhusu athari za matumizi ya dawa za kulevya.
Flaviana pia ni balozi wa Diamond Empowrment Fund (DEF). Alipewa heshima hiyo sambamba na Kim Kardashian na Selita Banks.
Hivi karibuni, Flaviana alizindua taasisi yake ya Flaviana Matata Foundation (FMF), ambayo lengo lake kubwa ni kutoa misaada kwa wanawake na watoto wenye matatizo wa Tanzania. Amekuwa akipata misaada ya kuendesha taasisi hizo kutoka ndani na nje ya nchi.
"Kwangu mimi, hii haikuwa tu njia ya kurejesha fadhila, bali pia kumbukumbu ya mama yangu, ambaye alikuwa mwanamke wa aina yake niliyepata kumfahamu. Aliwalipia ada wanafunzi kadhaa, ambao hawakuwa wa kwake na siku zote alikuwa tayari kutoa misaada,"amesema Flaviana katika mahojiano na mtandao huo.
"Hivyo jukumu la kwanza la taasisi yangu lilikuwa ni kuwasaidia watoto, hasa wanafunzi wa kike kuwadhamini katika elimu. Japokuwa sikuwahi kutangaza hadharani kuhusu yaliyokuwa yakifanywa na mama yangu, lakini nilitaka watu wafahamu thamani yake kwangu nini lengo la taasisi yangu,"aliongeza mwanamitindo huyo.
Mapema mwaka huu, Flaviana aliamua kufanya kitu kinachohusiana moja kwa moja na ajali ya MV Bukoba iliyosababisha kifo cha mama yake. Alitoa msaada wa maboya na fulana 500 za kujiokolea.
"Nilizisafirisha hadi Tanzania na kuzipeleka hadi katika mji wa Mwanza ulioko kando ya Ziwa Victoria, ambako boti kadhaa husafiri kila siku kwenda katika miji kadhaa, ukiwemo wa Bukoba, ambako mama yangu alipanda meli ya MV Bukoba kabla ya ajali na kufariki dunia,"alisema Flaviana.
Flaviana pia amekuwa akifanyakazi na taasisi ya Life Project for Africa, ambayo lengo lake kubwa ni kurejesha matumaini kwa baadhi ya watu wa Afrika kupitia huduma za afya, elimu na mavazi.

No comments:

Post a Comment