KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, October 18, 2012

DIAMOND AFURAHIA KUITWA MFALME WA BONGO FLEVA





MSANII nyota wa muziki wa kizazi kipya, Naseeb Abdul ameelezewa kuwa ndiye Mfalme wa Bongo Fleva kwa sasa hapa nchini.
Naseeb, ambaye ni maarufu zaidi kwa jina la Diamond, amepewa hadhi hiyo na mtandao wa MSN Africa.
Mbali na Diamond, mtandao huo pia umemtaja Judith Wambura Lady JayDee kuwa ndiye malkia wa muziki wa miondoko hiyo hapa nchini.
Kwa mujibu wa MSN Africa, Diamond na JayDee wanastahili hadhi hiyo kutokana na mafanikio mbali mbali waliyoyapata kimuziki.
Diamond ameeleza kupitia tovuti yake wiki hii kuwa, amepata furaha kubwa kutokana na hadhi aliyopewa na mtandao huo.
"Kiukweli, nimejisikia furaha kubwa kuandikwa katika mtandao mkubwa kama huu juu ya kazi zangu za muziki ninazozifanya," ameeleza Diamond katika sehemu ya taarifa yake aliyoitoa kwenye mtandao wake.
"Tena kubwa zaidi ni kupewa heshima hii ya kuwa Mfalme wa Bongo Fleva. Kiukweli imenipa matumaini sana ingawa nafsi yangu inaniambia bado sistahili kuitwa jina hilo kwani nina safari ndefu sana," aliongeza msanii huyo.
Diamond amewashukuru mashabiki wa muziki nchini kwa kuendelea kumuunga mkono kutokana na kazi zake na kuufanya muziki wa bongo fleva kuanza kupata umaarufu barani Afrika.
Ameishukuru familia yake, hasa mama yake mzazi na menejimenti inayosimamia kazi zake kwa kumuunga mkono muda wote wa kazi yake.
Diamond ni miongoni mwa wasanii, ambao wamekuwa wakitwaa mara kwa mara tuzo za muziki za Kilimanjaro kutokana na muziki wake kukubalika na mashabiki wengi, ndani na nje ya mipaka ya Tanzania.
Msanii huyo ameelezwa kuwa, ndiye anayeongoza kwa mapato yatokanayo na muziki na pia kualikwa katika nchi mbali mbali kufanya maonyesho.
Katika hatua nyingine, Diamond amewatahadharisha mashabiki wake kuhusu baadhi ya watu wanaotumia anwani yake ya facebook na twitter kuomba misaada ya pesa.
Diamond ameeleza kupitia tovuti yake kuwa, watu hao pia wamekuwa wakitumia akaunti zake kutoa maneno machafu kwa mashabiki wake.
"Nimevumilia sana hii tabia, lakini naona kama uzalendo umenishinda. Mara kwa mara nimekuwa nikipokea malalamiko kutoka kwa wadau wangu, mbali mbali kwamba nawajibu vibaya kwenye akaunti yangu ya facebook, kutoa maneno machafu na kuweka picha chafu,"alisema.
"Kibaya zaidi, watu hawa wamekuwa wakiomba pesa kwa njia ya Western Union, M-Pesa, Tigo Pesa na nyinginezo. Kiukweli jambo hili limekuwa likinisikitisha sana,"aliongeza.
Diamond amesema akaunti hiyo yenye jina la Diamond Platnums Swaqq ni feki kwa sababu siyo ya kwake, ni ya mtu anayetumia jina na picha zake kuwachezea akili mashabiki wake.
Wakati huo huo, Diamond ametoa mwito kwa watanzania kujenga utamaduni wa kutembelea vivutio vya kitalii vilivyopo nchini.
Diamond alitoa mwito huo wiki iliyopita baada ya kutembelea Hifadhi ya Ngorongoro iliyopo mkoani Arusha.
Akizungumza baada ya ziara yake hiyo, Diamond alisema kamwe katika maisha yake hakuwahi kufikiria iwapo Tanzania inavyo vivutio vizuri vya kitalii kama Hifadhi ya Ngorongoro.
Alisema alikuwa akiviona vivutio hivyo kupitia vipindi mbali mbali vya televisheni, lakini baada ya kuvishuhudia kwa macho yake, anatamani kuvitembelea mara kwa mara.
Diamond alitembelea hifadhi hiyo baada ya kumalizika kwa Tamasha la Fiesta, ambapo alikuwa miongoni mwa wasanii waliofanya vizuri na kupata tuzo maalumu.

No comments:

Post a Comment