'
Tuesday, October 30, 2012
TFF: CHONDE CHONDE YANGA, MLIPENI NJOROGE
TFF inapenda tena kuihimiza klabu ya Yanga kumalizana na mchezaji wake wa zamani, John Njoroge Mwangi kabla ya Novemba 2, 2012 ili ijiepushe na adhabu kaili inayoweza kuchukuliwa na Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Mpira wa Miguu (FIFA). Kwa mujibu wa barua ya FIFA, iwapo Yanga haitakuwa imemlipa mchezaji huyo na kusiwepo na mawasiliano yoyote, shauri hilo litawasilishwa kwenye Kamati ya Nidhamu ya FIFA itakayokutana Novemba 14, 2012 kutathmini hukumu iliyotolewa mapema Januari mwaka huu.
Mchezo namba 10 wa Ligi Daraja la Kwanza (FDL) baina ya Morani na Polisi Tabora uliokuwa uchezwe Kiteto mjini Tabora Oktoba 31, 2012, sasa utachezwa Novemba 01, 2012 baada ya treni ambayo Morani walikuwa wakisafiria kutoka kupata matatizo njiani wakati wakitoka Kigoma ambako walicheza na Kanembo.
TFF inapenda kutoa ufafanuzi wa taarifa zilizotolewa na baadhi ya vyombo vya habari leo, likiwemo gazeti la Habari Leo na Daily News, vikimnukuu rais wa TFF, Leodegar Tenga akisema kuwa amewataka watu wanaotaka kugombea uongozi wa shirikisho watangaze nia ili wapate kujadiliwa. Waandishi walioandika habari hiyo hawakumnukuu vizuri Rais Tenga wakati akizungumzia masuala ya uchaguzi na hivyo kupotosha maana nzima ambayo Ndg. Tenga alitaka iwafikie wapenzi wa michezo na hasa mpira wa miguu. Rais Tenga alivitaka vyombo vya habari vianzishe mjadala utakaowashirikisha wapenzi wa mpira wa miguu ili waelezee wanatarajia nini katika miaka ijayo na hivyo kuwafanya viongozi watakaochaguliwa kufanya kazi kwa utashi wa maoni hayo ya wananchi. Tunaelewa kuwa Rais Tenga ni muumini wa kuheshimu katiba, sheria na kanuni na hivyo hawezi kutoa kauli ambayo inakiuka mchakato wa uchaguzi wa TFF kwa kuwataka wanaowania uongozi kutangaza nia sasa badala ya kusubiri muda wa kikanuni ufike. Ikumbukwe katika kikao chake na wahariri aliwahi kuulizwa swali kama hilo na akasema kuwa akijibu lolote atakuwa amekiuka kanuni za uchaguzi kwa kuwa itamaanisha anaanza kampeniu kabla ya muda. Ni vizuri waliohusika wakafanya masahihisho ili kuzuia habari zao kutafsiriwa tofauti na wadau wa mpira wa miguu na hivyo kuweka uwezekano wa kuvuruga mchakato wa uchaguzi.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment