KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Tuesday, October 23, 2012

HASSANALI KUIWAKILISHA TANZANIA MAONYESHO YA MAVAZI AFRIKA KUSINI


Mbunifu maarufu wa mavazi kutoka Tanzania, Mustafa Hassanali ndiye Mtanzania pekee katika fani ya mitindo aliyepewa mualiko wa kushiriki katika maonyesho ya Wiki ya Mitindo Afrika chini ya African Fashion International (AFI) yatakayofanyika kwa siku nne kuanzia tarehe 24-28 Oktoba, 2012 katika ukumbi wa Melrose Arch, jijini Johannesburg, Afrika ya Kusini.
Mashindano hayo yanayodhaminiwa na kampuni ya kutengeneza Magari ya Mercedes-Benz yanatarajiwa kuwashirikisha wabunifu wa mavazi zaidi ya 35 kutoka sehemu mbalimbali barani Afrika, baadhi ya nchi hizo ni wenyeji Afrika ya Kusini, Ivory Coast, Morocco, Msumbiji, Cameroon, Rwanda, Angola, DRC, Nigeria, Ghana na Tanzania.
“Ni maonyesho ya pekee na yenye heshima yake barani Afrika na hata duniani kwa ujumla kwani wabunifu walioalikwa ni wazoefu na bora katika fani ya Mitindo barani Afrika. Hivyo mwaliko wangu si tu utaweza kutangaza kazi ni nazofanya bali pia utasaidia kutangaza nchi yetu ya Tanzania kupitia maonyesho haya” Alisema, Mustafa Hassanali.
“Watakapotaja jina langu pale katika maonyesho, hawatasema tu huyu ni Mustafa Hassanali, bali watasema huyu ni Mustafa Hassanali kutoka Tanzania, hivyo itakuwa ni mchango mkubwa kwa nchi yetu kuweza kuonyesha fursa zilizopo kupitia Ubunifu wa Mitindo. Nimejiandaa vizuri katika haya maonyesho, nataka kuonyesha nini Tanzania tunacho katika tasnia ya ubunifu kwa ulimwengu mzima ni imani yangu kufanya vizuri” aliongeza Hassanali.
AFI inaandaa mashindano haya ili kuweza kutangaza kazi za wabunifu wa mavazi kutoka barani Afrika katika soko la dunia kwani Afrika ina wabunifu wazuri na imara hivyo kujitokeza kwao katika maonyesho haya kutafungua milango zaidi katika soko la kimataifa na kuongeza fursa nyingi zitakazoinua uchumi wa bara hili kupitia sanaa ya ubunifu wa mitindo.
Licha ya kushiriki katika maonyesha haya, Mustafa Hassanali pia anawaomba Watanzania wote kwa ujumla kuweza kumpigia kura ya kuwa mwanamitindo bora barani Afrika kupitia tovuti ya www.awardnomination.afi.za.com na kuweza kuiletea sifa tasnia ya mitindo nchini Tanzania.
Huu ni mwaka wa tisa kwa Mustafa Hassanali kupata mwaliko wa kuonyesha ubunifu wake katika maonyesho haya. Ameshashiriki katika maonyesho zaidi ya nchi 16 katika miji 25 tofauti duniani, amekuwepo katika kilinge cha sanaa ya mitindo kwa muda mrefu hapa nchini, amechangia kwa kiasi kikubwa mabadiliko na maendeleo ya kazi za ubunifu wa mavazi hapa Tanzania.

No comments:

Post a Comment