KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, October 24, 2012

WAAMUZI WALA RUSHWA KUCHUNGUZWA


CHAMA cha Waamuzi wa Soka Tanzania (FRAT), kimesema kinafanyia kazi tuhuma za waamuzi wake kupokea rushwa ili wachezeshe kwa upendeleo katika mechi za ligi kuu ya Tanzania Bara.
Mwenyekiti wa FRAT, Joan Minja alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, wamekuwa wakipokea tuhuma hizo mara kwa mara kutoka kwa wadau wa soka hivyo wameona ni vyema wazifanyie kazi ili kubaini ukweli.
Joan alisema tuhuma zozote zinazohusiana na rushwa ni nzito na zinapaswa kuchunguzwa kwanza ikiwa ni pamoja na kupatikana kwa uthibitisho kabla ya kutolewa uamuzi.
Alisema baada ya kuzifanyiakazi tuhuma hizo, wanatarajia kuwasilisha ripoti kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa ajili ya maamuzi zaidi.
"Hatuwezi kutoa ripoti za uchunguzi wetu kwa vyombo vya habari, tutafanya hivyo kwa TFF kwa sababu ndicho chombo tunachofanyanacho kazi,"alisema mwenyekiti huyo mpya wa FRAT aliyechaguliwa hivi karibuni mjini Dodoma.
Timu kadhaa zinazoshiriki katika michuano ya ligi kuu, zimekuwa zikiwalalamikia baadhi ya waamuzi kwa madai kuwa, wamekuwa wakichezesha kwa upendeleo kutokana na kupewa rushwa.
Tayari kamati ya ligi imeshatangaza kuwasimamisha baadhi ya waamuzi na kuwaondoa kwenye ligi kwa madai ya kuvurunda katika baadhi ya mechi.
Mmoja wa waamuzi waliofungiwa ni Mathew Akrama kutoka Mwanza, aliyechezesha mechi ya ligi hiyo kati ya Simba na Yanga, iliyopigwa kwenye Oktoba 3 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1.

No comments:

Post a Comment