'
Wednesday, October 10, 2012
SAINTFIET APATA ULAJI YEMEN
KOCHA Mkuu wa zamani wa Yanga, Tom Saintfiet (katikati) akitia saini mkataba wa kuifundisha timu ya taifa ya Yemen mjini Sana'a juzi. Pembeni yake ni viongozi wa Chama cha Soka cha Yemen. (Picha kwa hisani ya blogu ya Bin Zubeiry).
KOCHA Mkuu wa zamani wa Yanga, Tom Saintfiet kutoka Ubelgiji amepata ulaji mwingine mpya baada ya kuingia mkataba wa kuinoa timu ya taifa ya Yemen.
Tom aliingia mkataba huo juzi, ikiwa ni siku chache baada ya uongozi wa Yanga kuamua kukatisha mkataba wake.
Kwa mujibu wa blogu ya Bin Zubeiry, hafla ya kutia saini mkataba huo ilifanyika katika mji wa Sana'a na kuhudhuriwa na viongozi mbali mbali wa Chama cha Soka cha Yemen.
Blogu hiyo ilimkariri Tom akisema kuwa, amefurahia kupata mkataba huo kwa sababu ni mzuri. Pia alieleza kufurahishwa na mapokezi aliyoyapata kutoka kwa viongozi wa chama hicho.
“Nimefurahi sana, kila kitu ni kizuri, mazingira ya kufanyia kazi na watu waelewa pia, sasa ni jukumu langu kuwafurahisha watu wa Yemen kwa kuwatengenezea timu nzuri itakayowapa furaha kwa matokeo mazuri,”alisema Tom.
Kocha huyo aliieleza blogu hiyo kwamba, anatarajia kuiongoza Yemen katika michuano ya Kombe la Mataifa ya Magharibi mwa Asia inayotarajiwa kufanyika nchini Kuwait mwishoni mwa mwaka huu.
“Kwa sasa nipo katika Jiji la Sana'a na kesho nitaanza kazi kwa kambi ya kujiandaa na mchezo wa kirafiki Beirut, Oktoba 16 dhidi ya Lebanon,”alisema Tom.
Kocha huyo alifukuzwa Yanga baada ya kutofautiana kimsimamo na uongozi, akiwa amefanya kazi siku 80. Kocha huyo alikuwa amerithi mikoba ya Kostadin Papic, ambaye naye alitimuliwa kutokana na timu kufanya vibaya msimu uliopita.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment