KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Friday, October 19, 2012

BAKHRESSA APIGWA CHINI DRFA

MAAMUZI KUHUSU RUFAA DHIDI YA MAAMUZI YA KAMATI ZA UCHAGUZI VYAMA VYA MPIRA WA MIGUU MKOA WA MBEYA (MREFA), MKOA WA SHINYANGA (SHIREFA) NA MKOA WA DAR ES SALAAA (DRFA).

19 OKTOBA 2012
1. Kwa mujibu wa Katiba ya TFF Ibara ya 49(1), Kanuni za Uchaguzi za wanachama wa TFF, Ibara ya 10(6), 12(1) na 26(2) na (3), Kamati ya Uchaguzi ya TFF katika vikao vyake vilivyofanyika tarehe 12 na 18 Oktoba 2012 ilijadili michakato ya chaguzi za vyama vya mpira wa miguu vya Mikoa ya Mbeya (MREFA), Shinyanga (SHIREFA) na Dar es Salaam (DRFA) na kutoa maamuzi kama ifuatavyo:
(a) Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Mbeya (MREFA)
(i) Rufaa ya Ndg. Charles Makwaza: Kamati ilijadili rufaa iliyowasilishwa na Ndg. Charles Makwaza dhidi ya Kamati ya Uchaguzi ya MREFA, iliyoomba Kamati ya Uchaguzi ya TFF kubatilisha uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi ya MREFA kumpitisha Ndg. John Mwamwaja kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa MREFA, kwamba hakutekeleza wajibu wa kikatiba wa kuitisha Mkutano Mkuu wa MREFA kwa muda wa miaka 3.
Baada ya kupitia maelezo ya warufani na warufaniwa, Kamati ya Uchaguzi ya TFF ilijiridhisha kuwa vielelezo na maelezo ya Ndg. Charles Makwaza yaliyowasilishwa mbele ya Kamati kwa kiwango kikubwa hayakuwa ya kweli. Kamati ya Uchaguzi ya TFF imeitupa rufaa hiyo.
(ii) Rufaa ya Ndg. Lusekelo E. Mwanjala: Kamati ilijadili rufaa iliyowasilishwa na Ndg. Lusekelo E. Mwanjala ikipinga maamuzi ya Kamati ya Uchaguzi ya MREFA kuliondoa jina lake kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa MREFA, kwa kigezo cha kutokuwa na uzoefu wa uongozi wa mpira wa Miguu.
Kamati ilipitia vielelezo kuhusu rufaa na kujadili maelezo ya Mrufani na Mrufaniwa na ilijiridhisha kuwa Ndg. Mwanjala anakidhi kigezo cha uzoefu. Kamati inakubaliana na rufaa ya mrufaa dhidi ya maamuzi ya Kamati ya Uchaguzi ya MREFA na hivyo imemrejesha Ndg. Mwanjala kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa MREFA.
(iii) Rufaa ya Ndg. Thadeo T. Kalua: Kamati ilijadili rufaa iliyowasilishwa mbele yake na Ndg. Kalua ikipinga maamuzi ya Kamati ya Uchaguzi ya MREFA kuliondoa jina lake kugombea nafasi ya Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF, kwa kigezo cha kutokuwa Mkazi wa Mkoa wa Mbeya. Kamati ilipitia vielelezo kuhusu rufaa hii na kubaini kuwa Katiba ya MREFA iliyosajiliwa haina sharti hilo kwa waombaji uongozi. Kamati inakubaliana na maombi ya
(iv) mrufaa na inamrejesha Ndg. Thadeo Kalua kugombea nafasi ya Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF.
(v) Uchaguzi wa MREFA utafanyika Jumamosi, tarehe 27 Oktoba 2012 kama ulivyopangwa.
(b) Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Shinyanga (SHIREFA).
(i) Rufaa ya Ndg. Ibrahim Magoma: Kamati ilijadili rufaa iliyowasilishwa na Ndg. Magoma ikipinga maamuzi ya Kamati ya Uchaguzi ya SHIREFA kuliondoa jina lake kugombea nafasi ya Katibu wa SHIREFA, kwa kigezo cha kuingilia Mchakato wa Uchaguzi kunyume na Kanuni za Uchaguzi za wanachama wa TFF na pia kutozingatia matakwa ya Kanuni hizo katika kujaza fomu za maombi ya uongozi wa SHIREFA.
Kamati ilipitia vielelezo kuhusu rufaa ya Ndg. Magoma na kujadili maelezo ya Mrufani na Mrufaniwa na ilijiridhisha kuwa Ndg. Magoma aliingilia mchakato wa uchaguzi wa SHIREFA kunyume na Kanuni za Uchaguzi za wanachama wa TFF akiwa Katibu Mkuu wa SHIREFA kwa kushiriki kuivunja Kamati ya Uchaguzi ya SHIREFA iliyokuwa ikendelea na mchakato wa uchaguzi wa SHIREFA. Kamati inakubaliana na uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi ya SHIREFA wa kumwondoa Ndg. Magoma kugombea nafasi ya Katibu wa SHIREFA. Kamati ya Uchaguzi ya TFF imeitupa rufaa hiyo.
(ii) Uchaguzi wa SHIREFA umesogezwa Mbele kwa siku nne. Uchaguzi huo utafanyika Alhamisi, tarehe 25 Oktoba 2012, mjini Shinyanga.
(c) Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es salaam (DRFA).
Kamati ya Uchaguzi ya TFF ilijadili Mchakato wa Uchaguzi wa DRFA na rufaa dhidi ya maamuzi ya Kamati ya Uchaguzi ya DRFA na kuamua kama ifuatavyo:
(i) Marekebisho na usajili wa Katiba ya DRFA: Hoja ya rufaa iliwasilishwa na Ndg. Michael R. Wambura ilikihoji uhalali wa marekebisho na usajili wa Katiba ya DRFA, kwamba usajili wa Katiba ya DRFA si halali. Kamati ilibaini kuwa marekebisho ya Katiba hiyo yalifanyika kwa kufuata maagizo ya TFF na kwamba DRFA ilizingatia maagizo hayo. Kamati ya Uchaguzi ya TFF iliridhika kuwa Katiba ya DRFA imesajiliwa na Msajili wa vyama na vilabu vya michezo baada ya kuridhiwa na TFF, na hivyo, Kamati iliitupa hoja hiyo ya Mrufani kuhusu uhalali na usajili wa Katiba ya DRFA.
(ii) Kuundwa kwa Kamati ya Uchaguzi ya TFF : Hoja ya rufaa ya Ndg. Michael R. Wambura iliomba Kamati ya Uchaguzi ya TFF kutoa tamko kuwa Kamati ya Uchaguzi ya DRFA imeundwa bila kufuata Kanuni za Uchaguzi Ibara ya 3(2). Kamati iliridhika kuwa Kamati ya Uchaguzi ya DRFA iliteuliwa kabla ya marekebisho ya Kanuni za Uchaguzi za wanachama wa TFF hususan, Ibara ya 3(2), hivyo uteuzi wa wajumbe wa Kamati hiyo haukukiuka Kanuni za Uchaguzi. Kamati iliitupa rufaa hiyo.
(iii) Wapiga kura wa Mkutano Mkuu wa DRFA: Hoja za rufaa za Ndg. Michael R. Wambura na Ndg. Juma Jabir ziliomba kuyaondoa majina ya Ndg. Abeid Mziba, Ndg. Salehe Ndonga, Peter Muhinzi na Ndg. Daudi Kanuti katika orodha ya wapiga kura wa Mkutano Mkuu wa DRFA na uongozi wa wanachama wa DRFA, kwamba hawana sifa kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi na Katiba za wanachama wa DRFA. Kamati ya Uchaguzi ya TFF haikupata vielelezo kuhusu hoja iliyowasisilishwa mbele ya Kamati na hivyo kuitupa hoja hiyo ya mrufani.
(iv) Rufaa dhidi ya Ndg. Mohamed Salim (Bakhressa) kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa DRFA. Rufaa dhidi ya uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi ya DRFA wa kumpitisha Ndg. Amin Mohamed Salim (Bakhressa) kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa DRFA iliyowasilishwa na Ndg. Michael R. Wambura na Ndg. Juma Jabir iliomba jina la Ndg. Amin Mohamed Salim (Bakhressa) liondolewe katika orodha ya wagombea uongozi wa DRFA kwa nafasi ya Mwenyekiti, kwa kuwa hana elimu ya kiwango cha kidato cha nne na hivyo kutokidhi matakwa ya Katiba ya DRFA Ibara ya 29(2) inayotamka kwamba ‘Mtu yeyote anayegombea nafasi yoyote ya DRFA hana budi awe na kiwango cha elimu kisichopungua kidato cha nne (Academic Certificate of Ordinary Secondary Education).
Kamati ya Uchaguzi ya TFF ilipitia vielelezo kuhusu rufaa dhidi ya maamuzi ya Kamati ya Uchaguzi ya DRFA na kujadili maelezo ya Warufani, Kamati ya Uchaguzi ya DRFA na Ndg. Amin Mohamed Salim na ilijiridhisha kuwa Ndg. Amin Mohamed Salim (Bakhressa) hana elimu ya kiwango cha kidato cha nne na hivyo hakidhi matakwa ya Katiba ya DRFA Ibara 29(2). Kwa kutokidhi matakwa hayo ya katiba ya DRFA, Ndg. Amin Mohamed Salim (Bakhressa) hastahili kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa DRFA. Kamati ya Uchaguzi ya TFF inakubaliana na maombi ya Warufaa.
(v) Rufaa kupinga kuenguliwa kugombea Uongozi DRFA: Ndg. Evans Elieza na Ndg. Juma Jabir waliwasilisha rufaa wakiomba Kamati ya Uchaguzi ya TFF kutengua uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi ya DRFA wa kuwaengua kugombea uongozi kwa madai ya kugushi sahihi ya Katibu wa Chama cha Mpira wa Miguu Wilaya ya Kinondoni (KIFA). Katika vielelezo mbalimbali vilivyoletwa mbele ya Kamati na baada ya kuwahoji warufani, Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya DRFA, Katibu wa KIFA, Ndg. Seif Ally Mailo aliyeshuhudia maelezo ya fomu za waombaji uongozi DRFA na baadhi ya waombaji uongozi ambao kupitishwa kwao na Kamati ya Uchaguzi ya DRFA kulilalamikiwa, Kamati ilibaini kuwa kulikuwa na ukiukwaji mkubwa wa Kanuni na taratibu za uchaguzi zilizofanywa na Kamati ya Uchaguzi ya DRFA na pia ama KIFA au wagombea wenyewe. Kutokana na mkanganyiko, maelezo yenye utata kutoka kwa warufani na warufaniwa na maamuzi ya utata ya Kamati ya Uchaguzi ya DRFA yameufanya mchakato wa uchaguzi wa DRFA kupoteza hadhi ya uchaguzi unaozingatia Kanuni za Uchaguzi na misingi ya demokrasia na uwazi kama ilivyoainishwa kwenye Kanuni za Uchaguzi za TFF. Kamati ya Uchaguzi ya TFF ilijiridhisha kwamba:
· Kamati ya Uchaguzi ya DRFA iliwapitisha wagombea Ndg. Gungurugwa Tambaza, Ndg. Mohammed Bhinda, Ndg. Benny Kisaka na Ndg. Hamisi Ayoub Mpapai bila kuwa na vielelezo vinavyothibitisha kuwa wana kiwango cha elimu kisichopungua kidato cha nne (Academic Certificate of Ordinary Secondary Education).
· Hoja ya kughushi saini ya Katibu wa KIFA katika kushuhudia maelezo ya baadhi ya wombaji uongozi, ambayo ilitumiwa na Kamati ya Uchaguzi ya DRFA kuwaondoa kugombea uongozi waombaji uongozi watano (5) Ndg. Hamis Ambar, Ndg. Hamisi Kisiwa, Ndg. Andrew Tupa, Ndg. Evans Elieza na Ndg. Juma Jabir haikutumika kuwaondoa baadhi wagombea ingawa fomu za waombaji uongozi saba zilisainiwa na Ndg. Ndg. Seif Ally Mailo.
· Ndg. Seif Ally Mailo ambaye si mwajiriwa na si kiongozi wa KIFA hakuwa na mamlaka ya kushuhudia maelezo ya wagombea kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi.
· Kulikuwa na hali ya kumficha Ndg. Seif Ally Mailo aliyesaini fomu za wagombea walioenguliwa kwa kigezo cha kughushi saini asifike kwenye kamati ya Uchaguzi ya TFF kutoa maelezo kuhusu ushiriki wake katika mchakato wa uchaguzi wa DRFA.
· Fomu za wagombea Ndg. Said H.Tully na Ndg. Shaffih Dauda zilizojadiliwa na Kamati ya Uchaguzi ya DRFA na hivyo kupitishwa na Kamati hiyo zilichezewa (tempered-with) kwa kunyofolewa baadhi ya kurasa na kuwekwa kurasa zenye maelezo na saini ambazo si za Ndg. Said H.Tully na Ndg. Shaffih Dauda. Wagombea hao ambao walikuwa wamepetishwa na Kamati ya Uchaguzi ya DRFA kwa maelezo kwamba fomu zao zilikuwa zimeshudiwa kwa sahihi halali ya Ndg. Ndg. Seif Ally Mailo walikana kwa maandishi na kutoa vielelezo vilivyothibitisha kwamba fomu zao zilichezewa na maelezo yaliyo kwenye kurasa zilizobadilishwa siyo wao walioyandika na kusaini.
· Kamati ya Uchaguzi ya DRFA iliwaondoa baadhi ya waombaji uongozi kwa maelezo kwamba maelezo kwenye fomu za wagombea hao hayakushuhudiwa na viongozi vyama wanachama wa DRFA wenye mamlaka ya kushuhudia maelezo ya waombaji uongozi lakini bila kuzingatia matakwa hayo ya kikanuni ikawapitisha kugombea Ndg. Muhsin S. Balhabou na Ndg. Benny Kisaka ambao maelezo ya kwenye fomu zao hayakushuhudiwa na kiongozi wa chama mwanachama yeyote wa DRFA.
· Kamati ya Uchaguzi ya DRFA inahusika kwa kiwango kikubwa katika ukiukwaji wa Kanuni na taratibu za uchaguzi na kutozingatia matakwa ya Katiba ya DRFA katika mchakato wa uchaguzi wa viongozi wa DRFA.
Kamati ya Uchaguzi ya TFF kwa kuzingatia Katiba ya TFF Ibara ya 49(1), Kanuni za Uchaguzi za wanachama wa TFF Ibara ya 10(6), 12(1) na 26(2) na (3):
(i) Imeifuta Kamati ya Uchaguzi ya DRFA. DRFA inaagizwa kuteuwa Kamati mpya ya Uchaguzi itakayoandaa na kutekeleza majukumu yake ikizingatia Kanuni za Uchaguzi za wanachama wa TFF na Katiba ya DRFA. Uteuzi wa Kamati mpya ya Uchaguzi ya DRFA ufanyike kabla ya tarehe 25 Oktoba 2012
(ii) Imefuta mchakato wa Uchaguzi wa DRFA. Mchakato wa uchaguzi utaanza upya tarehe 29 Oktoba 2012 na uchaguzi utafanyika tarehe 08 Desemba 2012. Wagombea wote waliokuwa wamelipia Fomu za maombi ya uongozi (Fomu Na. 1) wanaokidhi sifa za kugombea uongozi kwa mujibu wa Katiba ya DRFA na Kanuni za Uchaguzi za wanachama wa TFF wajaze upya Fomu Na.1 bila kutozwa ada kwa nafasi zinazoendana na zile walizokuwa wameomba kugombea.
Deogratias Lyatto
MWENYEKITI KAMATI YA UCHAGUZI TFF

No comments:

Post a Comment