Timu ya Taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 17 (Serengeti Boys) imefuzu kucheza raundi ya tatu na ya mwisho ya michuano ya kutafuta tiketi ya kucheza Fainali za Afrika kwa Vijana baada ya Misri kujitoa.
Serengeti Boys ilikuwa icheze raundi ya pili dhidi ya Misri; mchezo wa kwanza ungechezwa Oktoba 14 mwaka huu jijini Dar es Salaam na ule wa marudiano wiki mbili baadaye jijini Cairo.
Katika raundi ya kwanza, Serengeti Boys inayofundishwa na Jakob Michelsen kutoka Denmark, ilikuwa icheze na Kenya mwezi uliopita, lakini nchi hiyo ilijitoa katika michuano hiyo ambayo fainali zake zitachezwa Machi mwakani nchini Morocco.
Serengeti Boys sasa itacheza raundi ya tatu kwa kumkabili mshindi wa mechi kati ya Zimbabwe na Congo Brazzaville. Mechi ya kwanza itachezwa Novemba 18 mwaka huu jijini Dar es Salaam wakati ya marudiano itafanyika ugenini wiki mbili baadaye.
Zimbabwe na Congo Brazzaville zitapambana kati ya Oktoba 12-14 mwaka huu, Zimbabwe ikiwa mwenyeji wa mechi ya kwanza wakati ya marudiano itafanyika kati ya Oktoba 26-28 mwaka huu.
No comments:
Post a Comment