KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, October 24, 2012

DEANGELIS GABRIEL BARBOSA, Mbrazil mwenye






Na Sophia Wakati, Tanga
KLABU ya Coastal Union ya mjini Tanga wiki iliyopita ilimtambulisha rasmi mshambuliaji wake mpya, Deangelis Gabriel Barbosa kutoka Brazil, ambaye anatarajiwa kuichezea katika michuano ya ligi kuu ya Tanzania Bara.
Barbosa (27) aliwasili mjini Tanga akiwa amefuatana na mkewe, Zaira Caroline na binti yao, Lara Barbosa na kupokewa kwa shangwe kubwa na mashabiki wa klabu hiyo yenye maskani yake barabara ya 12.
Kwa kumsajili Barbosa, anayecheza nafasi ya kiungo mkabaji, Coastal Union imeweka historia ya kuwa klabu ya kwanza ya Tanzania kumsajili mchezaji kutoka Brazil.
Barbosa amejiunga na Coastal Union akitokea klabu ya New Road ya Nepal aliyojiunga nayo mwaka 2010.
Kiungo huyo mkabaji pia amewahi kuzichezea klabu za Paham Footbal Club, Flamengo na Santa Cruz za Brazil na Churchill Brothers ya India.
Usajili wa mchezaji huyo umezua maswali mengi kutoka kwa mashabiki wa soka nchini. Wapo wanaohoji iwapo Mbrazil huyo ana kiwango kinachofanana na wachezaji kutoka nchi yake na wengine wanahoji iwapo Coastal Union itaweza kumlipa malipo anayotaka kulingana na mkataba wake.
Akimtambulisha mchezaji huyo kwa waandishi wa habari, Makamu Mwenyekiti wa Coastal Union, Steven Mnguto alisema wamefurahishwa na ujio wake kwa sababu wanaamini atatoa msaada mkubwa kwa timu hiyo.
Mnguto alisema kwa sasa wanashughulikia kibali chake cha kufanyakazi kutoka Idara ya Uhamiaji ili aanze kuichezea timu hiyo katika michuano ya ligi kuu ya Tanzania Bara, inayoendelea kwenye viwanja mbali mbali nchini.
Kwa mujibu wa Mnguto, Mbazil huyo ametia saini mkataba wa kuichezea Coastal Union kwa mwaka mmoja na anatarajiwa kuonekana uwanjani baada ya kupatiwa kibali hicho.
Mnguto alisema tayari mchezaji huyo ameshapata hati ya uhamisho wa kimataifa (ITC) kutoka kwa Chama cha Soka cha Nepal.
"Ujio wa Barbosa umekuja kwa wakati mwafaka kwa sababu tunahitaji sana mchezaji wa aina yake,"alisema.
Hata hivyo, Mnguto alikiri kuwa hawafahamu vyema uwezo wa Barbosa kisoka, lakini kutokana na wasifu wake kutoka kwa wakala aliyemleta nchini, wanaamini kuwa ni mchezaji mwenye uwezo mkubwa.
Akizungumza wakati wa utambulisho huo, Barbosa alisema amefurahi kuja kucheza soka Tanzania na Afrika kwa jumla na kuwataka mashabiki wa Coastal Union watarajie mambo mazuri kutoka kwake.
"Mimi na mke wangu hatukutarajia kupata mapokezo makubwa na mazuri kama haya. Ninachoahidi ni kwamba nitajitahidi kucheza kadri ya uwezo wangu ili kuisaidia timu yangu mpya,"alisema.
Mbrazil huyo alisema atarejesha shukurani zake kwa viongozi na mashabiki wa Coastal Union kwa kukipiga kwa uwezo wake wote ili timu hiyo iweze kufanya vizuri katika ligi kuu.
Hata hivyo, Barbosa alikiri kutoifahamu vyema Tanzania kisoka, lakini alisema hilo haliwezi kumpa matatizo kwa sababu mchezo huo unafanana kote duniani.
Barbosa alisema alianza kucheza soka nchini kwao Brazil katika Jiji la Paulo Alonso na kuitaja klabu yake ya kwanza kuwa ni Paham. Baadaye alijiunga na timu ya vijana ya Flamengo kabla ya kuhamia Santa Cruz zote za Brazil.
Mbrazil huyo alisema baadaye aliamua kwenda India, ambako alijiunga na klabu ya Churchill Brothers kabla ya kutua Nepal, ambako alijiunga na klabu ya New Road.
Kwa mujibu wa mtandao, majina halisi ya mchezaji huyo ni Deangelis Gabriel Galvão Barbosa da Silva. Alizaliwa Agosti 25, 1984. Ana uzito wa kilo 77 na anatumia zaidi mguu wa kulia.

1 comment:

  1. Deangelis great, his success in this new journey, you deserve a boy s dedicated, hard-working and further plays a sweepstake. big hugs. Junior Fernandes

    ReplyDelete