MCHEZA filamu machachari wa Tanzania, Hissan Muya 'Tino' ameibuka na movi mpya kali inayokwenda kwa jina la CID.
Akizungumza mjini Dar es Salaam wiki hii, Tino alisema filamu hiyo inahusu mambo ya upepelezi dhidi ya mtandao wa majambazi na wauaji.
Tino alisema filamu hiyo inatarajiwa kuzinduliwa rasmi kesho katika onyesho litakalofanyika kwenye ukumbi wa Business Park, ulioko Mikocheni, Dar es Salaam.
Alisema uzinduzi wa filamu hiyo utapambwa na burudani mbali mbali, zikiwemo muziki wa dansi na kizazi kipya.
Mcheza filamu huyo mwenye mvuto alisema, kwa sasa ameamua kuachana na filamu za mapenzi, badala yake atakuwa akicheza filamu za mapigano.
Alisema uamuzi wake huo umelenga kupiga hatua kubwa zaidi kimaendeleo katika fani hiyo baada ya kubaini kwamba, filamu za mapenzi hazina mvuto mkubwa kwa mashabiki.
Tino, ambaye amecheza filamu zaidi ya 20 alisema, mbali na filamu za mapigano, atakuwa akicheza filamu zenye mwelekeo wa kuielimisha jamii juu ya masuala mbali mbali.
"Kwa sasa watu wengi wamejikita kutengeneza na kucheza filamu za mapenzi na kusuahau mambo mengine muhimu yanayoigusa jamii, hasa ujambazi, magonjwa kama vile ukimwi na mengineyo,"alisema msanii huyo.
Aliitaja sababu nyingine iliyomfanya azitose filamu za mapenzi kuwa, ni baada ya kupata matatizo alipotengeneza filamu ya shoga.
Filamu hiyo ilikuwa ikielezea tabia ya ushoga katika jamii, lakini mamlaka zinazohusika ziliamua kuipiga marufuku kwa madai kwamba, ilikuwa inakiuka maadili ya kitanzania.
Hata hivyo, baada ya filamu hiyo kufanyiwa marekebisho, ilibadilishwa jina na kuitwa Shoga yangu. Tino hakufurahishwa na uamuzi huo kwa madai kuwa, ulipoteza maana halisi ya filamu hiyo.
“Filamu za mapenzi sasa kwangu basi, nataka kugeukia kwenye filamu za mapigano na zile zinazogusa maisha ya binadamu wa kawaida,” alisema Tino.
Tino amewashauri wasanii wengine kutojikita sana katika filamu za mapenzi kwa vile yapo matukio mengi yanayotokea katika jamii, ambayo yanapaswa kuandikiwa filamu.
Katika hatua nyingine, Tino ameanzisha shindano la Bongo Movie Star Search, linalotarajiwa kuanza hivi karibuni.
Tino amesema ameamua kuanzisha shindano hilo kwa lengo la kuibua na kuviendeleza vipaji vya vijana, hasa wanaoishi mikoani.
Alisema wazo la kuanzisha shindano hilo lilitoka kwa marehemu Steven Kanumba na walikuwa wamepanga kulifanyiakazi kwa pamoja kabla ya mauti kumkuta.
No comments:
Post a Comment