KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Tuesday, July 31, 2012

AUNTY EZEKIEL KUFUNGA NDOA OKTOBA

ILE kasumba kwamba hakuna msanii wa bongo muvi anayeweza kuolewa na kudumu ndani ya ndoa, inatarajia kufutwa na msanii Aunty Ezekiel, ambaye anatarajia kufunga ndoa mwezi October mwaka huu, na mpenzi wake anayeishi Dubai ambako ndiko atakoenda kuishi baada ya kufunga ndoa.
Mtandao , ulifanya mazungumzo mafupi na msanii huyo juu ya maisha yake na filamu kwa ujumla ambapo, alisema kuwa ameamua kuchukua maamuzi hayo ya kutaka kufunga ndoa kwani anahitaji kuishi na mtu ambaye wataweza kupanga naye maisha.
Alidai kuwa mpenzi wake huyo ni Mtanzania ingawa anaishi nje, ambapo anaamini baada ya kufunga ndoa na yeye anataweza kwenda kufanya kazi huko.
“Nilikuwa kimya juu ishu hii lakini nachotaka kusema ni kwamba mambo yangu sasa yameanza na nimeamua kufunga ndoa, hivyo mashabiki wangu nahitaji nao waweze kujua kuwa sasa nimeamua kuchukua maamuzi hayo,” alisema.
Ezekiel alisema kuwa vikao vya harusi na kupanga itakavyokuwa wameshaaza kukaa, kwani wameanza Jumapili.
Aliongeza kuwa mbali na mchakato huo mkubwa pia mwaka huu wa 2012 kampuni yake inatarajia kufunga mwaka kwa kutoa filamu mbili ambazo anaamini zitakuwa moto wa kuotea mbali.
CHANZO CHA HABARI;ODAMA1.BLOGSPOT

NGORONGORO, NIGERIA ZAINGIZA MIL 12/-

Mechi ya kwanza ya raundi ya pili kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Afrika kwa vijana chini ya umri wa miaka 20 kati ya Tanzania (Ngorongoro Heroes) na Nigeria (Flying Eagles) iliyochezwa juzi (Julai 29 mwaka huu) imeingiza sh. 12,901,000.
Fedha hizo zimepatikana kutokana na watazamaji 3,377 waliokata tiketi kushuhudia pambano hilo lililochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Sehemu iliyoingiza watazamaji wengi ilikuwa viti vya bluu na kijani ambapo 2,697 walikata tiketi kwa kiingilio cha sh. 3,000 kila mmoja. Viingilio vingine katika mechi hiyo vilikuwa sh. 5,000 kwa viti vya rangi ya chungwa, sh. 10,000 kwa VIP C na B, na sh. 15,000 kwa VIP A iliyoingiza watazamaji 21.
Mgawanyo wa mapato hayo ni kama ifuatavyo; asilimia 18 ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ilikuwa sh. 1,967,949.15, gharama ya kuchapa tiketi sh. 2,250,000, gharama za waamuzi na kamishna wa mechi hiyo sh. 760,000 na ulinzi na usafi kwa Uwanja wa Taifa sh. 2,350,000.
Malipo kwa Wachina (Beijing Construction) sh. 2,000,000, asilimia 20 ya gharama za mchezo ni sh. 714,610.17, asilimia 10 ya uwanja sh. 357,305.08, asilimia 5 ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) sh. 178,652.54 na asilimia 65 ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) sh. 2,322,483.05.
Mechi ya marudiano ya michuano hiyo ambayo fainali zake zitafanyika mwakani nchini Algeria itachezwa Agosti 12 mwaka mjini Ilorin, Jimbo la Kwara, Nigeria.
PONGEZI KWA UONGOZI MPYA SIREFA
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linatoa pongezi kwa uongozi mpya wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Singida (DOREFA) uliochaguliwa katika uchaguzi uliofanyika Julai 28 mwaka huu.
Ushindi waliopata viongozi waliochaguliwa kuongoza chama hicho unaonesha jinsi wajumbe wa Mkutano Mkuu wa SIREFA walivyo na imani kubwa kwao katika kusimamia mchezo huo mkoani Singida.
TFF inaahidi kuendeleza ushirikiano wake kwa Kamati ya Utendaji ya SIREFA chini ya uenyekiti wa Baltazar Kimario ambaye amechaguliwa kwa mara ya kwanza.
Uongozi huo mpya una changamoto nyingi, kubwa ikiwa ni kuhakikisha unaendesha shughuli za mpira wa miguu mkoani Singida kwa kuzingatia katiba ya SIREFA pamoja na vyombo vya mpira wa miguu vilivyo juu yake.
Pia tunatoa pongezi kwa Kamati ya Uchaguzi ya SIREFA na Kamati ya Uchaguzi ya TFF kwa kuhakikisha uchaguzi huo unaendeshwa kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi za wanachama wa TFF.
Viongozi waliochaguliwa katika uchaguzi huo uliofanyika Chuo Cha Maendeleo ya Jamii Singida ni Baltazar Kimario (Mwenyekiti), Hussein Mwamba (Katibu Mkuu), Gabriel Gunda (Katibu Msaidizi), Gabriel Mwanga (Mhazini), Hamisi Kitila (Mjumbe wa Mkutano Mkuu TFF), Omari Salum (Mwakilishi wa Klabu TFF), Yagi Kiaratu na Dafi Dafi (wajumbe wa Kamati ya Utendaji).
Nafasi za Makamu Mwenyekiti, Mhazini Msaidizi na wajumbe wawili wa Kamati ya Utendaji zitajazwa katika uchaguzi mdogo utakaofanyika baadaye.
MICHELSEN AITA 22 KAMBI YA COCA-COLA
Kocha wa timu za Taifa za vijana za Tanzania, Jakob Michelsen ameita wachezaji 22 kwa ajili ya michuano ya kimataifa ya Coca-Cola itakayofanyika baadaye mwaka huu nchini Afrika Kusini.
Baadaye watachujwa na kubaki 16 ambao ndiyo watakaokwenda kwenye michuano ya Afrika Kusini.

Wachezaji waliochaguliwa wametokana na michuano ya Copa Coca-Cola iliyofanyika jijini Dar es Salaam na mkoani Pwani kuanzia Juni 24- Julai 2 mwaka huu.
Wachezaji walioitwa ni Abdulrahman Mandawanga (Dodoma), Abraham Mohamed (Mjini Magharibi), Ayoub Alfan (Dodoma), Bakari Masoud (Tanga), Daniel Justin (Dodoma), Denis Dionis (Ilala), Edward Songo (Ruvuma), Fikiri Bakari (Tanga), Hassan Kabunda (Temeke), Joseph Chidyalo (Dodoma), Mutalemwa Katunzi (Morogoro) na Mwarami Maundu (Lindi).
Wengine ni Nankoveka Mohamed (Ilala), Nelson Peter (Morogoro), Omari Saleh (Singida), Rajab Rajab (Mwanza), Said Said (Kagera), Shiza Kichuya (Morogoro), Shukuru Msuvi (Temeke), Tanganyika Suleiman (Kigoma), Tumaini Baraka (Kilimanjaro) na William John (Ruvuma).
Pia Michelsen ameongeza wachezaji saba kwenye kikosi cha Serengeti Boys ambacho Septemba mwaka huu kitacheza na Kenya kuwania tiketi ya fainali za vijana wenye umri chini ya miaka 17 za Afrika zitakazofanyika mwakani nchini Morocco.
Wachezaji walioongezwa kwenye kikosi hicho ambao pia wametoka kwenye Copa Coca-Cola ni Abdallah Baker (Mjini Magharibi), Abdallah Kheri (Mjini Magharibi), Calvin Manyika (Rukwa), Dickson Ambunda (Mwanza), Hassan Mganga (Morogoro), Miza Abdallah (Kinondoni) na Mzamiru Said (Morogoro).

JB AMGALAGAZA RAY

Msanii nyota wa filamu, Jacob Steven, maarufu kwa jina la JB

Msanii machachari wa bongo movie, Vicent Kigosi, maarufu kwa jina la Ray


Mcheza filamu nyota nchini, Jacob Steven ameibuka mshindi wa shindano la mcheza filamu bora wa kiume wa bongo lililoandaliwa na blogu ya liwazo zito.

Shindano hilo liliwashirikisha wacheza filamu wanne wa kiume wa bongo movie na washiriki walipigiwa kura na wasomaji wa blogu hii kutoka sehemu mbali mbali duniani.

Jacob, ambaye ni maarufu zaidi kwa jina la JB aliibuka mshindi baada ya kupata kura 33, ambazo ni sawa na asilimia 82 ya kura zilizopigwa.

Vicent Kigosi, maarufu kwa jina la Ray alishika nafasi ya pili baada ya kupata kura nne, ambazo ni sawa na asilimia 14,

Single Mtambalike, maarufu kwa jina la Richie alishika nafasi ya tatu baada ya kuambulia kura mbili wakati Issa Mussa, almaarufu kwa jina la Cloud aliambulia kura moja.

Msanii Awadh Mahsen, maarufu kwa jina la Dk. Cheni ndiye pekee, ambaye hakuambulia kura katika washiriki watano walioshindanishwa katika shindano hili.

Mmiliki wa blogu ya liwazo zito, Rashid Zahor amesema lengo la kuandaa shindano la aina hii ni kuwapa nafasi wasanii wa fani mbali mbali wajitambue kupitia kwa watazamaji na mashabiki wa fani wanazoshiriki.

Zahor, maarufu kwa jina la Ramoza alisema kupitia kura hizi zinazopigwa na wasomaji na watazamaji wa fani hizo, wasanii wanaweza kujitambua namna wanavyokubalika ama wasivyokubalika na mashabiki wao na nini wafanye ili waweze kupiga hatua zaidi.

Alimpongeza JB kwa kuibuka mshindi wa shindano hilo na kuwashukuru wasomaji wote wa blogu hii walioshiriki kupiga kura na wale wanaoipitia kila siku kwa ajili ya kupata taarifa mbali mbali zinazohusu michezo na burudani ndani na nje ya nchi.

AZIM DEWJI AIPONGEZA YANGA

MWANACHAMA maarufu wa klabu ya Simba, Azim Dewji ameipongeza timu yasoka
ya Yanga kwa kufanikiwa kutetea ubingwa wa michuano ya AfrikaMashariki na Kati.Yanga ilifanya hivyo mwishoni mwa wiki, baada ya kuizamisha Azam kwamabao 2-0 katika mchezo mkali wa fainali kwenye Uwanja wa Taifa, Dares Salaam.

Akizungumza jana, Dewji aliyewahi kuifadhili Simba na kuifikisha fainali za Kombe la CAF mwaka 1993, alisema pamoja na yeye kuwa `SimbaDamu’, ana kila sababu za kuimwagia sifa Yanga kwa kuwa imezika harakamatatizo yake na kugeukia kusaka maendeleo.

“Huwezi kuamini kama Yanga iliyopigwa 5-0 na kuibua tafrani nzitoJangwani, ndiyo hii ya leo. Wameikubali hali na kubadilika ndani ya muda mfupi sana. Wana amani na matunda yake yameonekana ingawa walikuwa na kipindi kifupi cha kusuka timu na kurejesha mshikamanondani ya klabu.

“Naipongeza Yanga na hasa Mwenyekiti wake, Yussuf Manji kwa sababunaamini imani ya
wanachama juu yake ndiyo iliyorekebisha hali haraka,naye kama kiongozi kuhakikisha usajili makini unafanyika, kochaanapatikana na uzalendo ndani ya Yanga unarejea,” alisema Dewji.

Aliongeza kuwa, pamoja na matunda ya haraka ya uongozi wa Manji,wana-Yanga wanapaswa kumpa ushirikiano ili kuiondoa Yanga katikautegemezi wa miaka nenda rudi, huku akisisitiza Manji hatabaki Yangamilele.

“Wana kiongozi shupavu, sasa washirikiane naye kuujenga uchumi waklabu. Haya mambo
ya kutegemea mtu kila kukicha si mazuri. Na hili sikwa Yanga tu, hata Simba na klabu nyingine
zinapaswa kujikita katikakujijenga kiuchumi ili ziwe na jeuri ya fedha bila ya kutegemea mifukoya mwanachama mmoja mmoja,” alisema.

Akisisitiza kujijenga kiuchumi, Dewji mmoja wa wafanyabiashara maarufunchini, alisema viongozi wa klabu kubwa za Simba na Yanga zianzekuutumia mtaji wa wanachama kujijenga, huku akitolea mfano kuwa, kilamoja ina zaidi ya wafuasi milioni 15, lakini klabu zinabaki kuwamasikini.

“Huu ni mtaji mkubwa sana, lakini utashangaa klabu haina hata asilimia moja (150,000) ya wanachama wa kweli. Kila siku utasikia wanachama3,000 hadi 6,000. Kiongozi wa klabu anachaguliwa na wanachamawasiofika 2,000?

“Jamani, kwa klabu inayoshabikiwa na mamilioni ya watu inashindwajekujijenga kiuchumi kwa kuwatumia mashabiki wake waliozagaa kila konaya nchi? Jiulize, kama angalau hao watu 150,000 tu wakilipa ada yamwaka ya 12,000 ambayo hata hivyo bado ni ndogo, si wanaweza kuvuna shbilioni 1.8 kwa mwaka, hizi si fedha nyingi?

“Kuna haja ya kufanya mapinduzi ya kweli, badala ya kufikiria kuifungaSimba au Yanga na kutwaa ubingwa wa Bara. Timu yenye uchumi imara,ndiyo inayokuwa na jeuri ya kuwa na kikosi imara na hivyo kufanyavizuri zaidi ndani na nje ya mipaka ya Tanzania. Huko ndikotunakopaswa kwenda,” alisisitiza.

SIMBA YAMNASA TWITE WA APR

MAKAMU Mwenyekiti wa Simba, Godfrey Nyange Kaburu amesema wapo kwenye hatua za mwisho za kupata saini ya beki wa APR, Mbuyu Twite kuziba pengo la Kelvin Yondani aliyetimkia Yanga.
Akizungumza jana, Kaburu alisema mpango wao wa kuimarisha kikosi chao unakwenda vizuri na umepata baraka zote za kocha Milovan Circkovic.
Alisema beki huyo amekubali kucheza Simba msimu ujao."Ni mapema kutaja kiasi cha fedha tutakachotumia kukamilisha usajili wake, lakini wiki ijayo atatua nchi kwa lengo la kukamilisha usajili." alisema Kaburu.
Akithibitisha hilo kwa simu jana kutoka Kigali, Rwanda, Twite alisema kuwa anashawishika kuja kukipiga Simba baada ya viongozi wa klabu hiyo kuzungumza naye.
"Ukweli ni kwamba jana (juzi) kabla hatujarudi nyumbani Rwanda nilikutana na watu wa Simba tukazungumza ili nije kuichezea timu yao, niliwaambia nipo tayari ingawa hatukufikia muafaka wa moja kwa moja."Hata hivyo, hakuna shaka kwamba mambo yatakwenda vizuri na hatutashindwana kwa vile binafsi napenda kuja kucheza Tanzania," alisema Twite
Kuhusu dau analohitaji ili aweze kujiunga na Simba,Twite hakuwa tayari kusema. Katika hatua nyingine, Kaburu alisema kabla ya kocha Milovan kuondoka alishauri kuachwa kwa beki Lino Musomba, Haruna Shamte pamoja na Salim Kinje.
"Kocha ameonyesha kutoridhisha na viwango vya wachezaji hao hivyo ameshauri tuwaache," alisema na kuongeza:"Musomba alionekana kama hayuko tayari kucheza, naye Shamte ameshindwa kuonyesha kiwango hivyo ametushauri kuwaacha.
Kuhusu ushiriki wa Simba kwenye michuano ya Kombe la BancABC Supa 8, kiongozi huyo alisema hawatashiriki kutokana na maslahi duni.
Kaburu alisema katika mkataba uliongia kati ya TFF na wadhamini wa michuano hiyo unaonyesha shirikisho lilitapokea asilimia 50."Sisi kama wadau wakubwa wa mashindano hayo tulipaswa kushirikishwa tangu mwanzo ili tufaidike kuliko ilivyokuwa sasa."
Ukiangalia mkataba huo utaona kila timu inapewa Sh5 milioni za maandalizi, na zawadi anapewa bingwa pekee ambayo ni Sh30 milioni."Hakuna zawadi ya mshindi wa pili, watatu sasa hayo ni mashindano gani, hatutoshiriki na endapo tutaamua kucheza basi tutaitumia timu ya vijana chini ya miaka 20.

CHANZO CHA HABARI;MWANANCHI

WATEJA AIRTEL SASA KUTUMA PESA URE KUPITIA AIRTEL MONEY

Kampuni ya simu za mkononi ya Airtel imeendelea kuboresha huduma ya Airtel money kwa kurahisisha upatikanaji wa muongozo (menu) kwa kupiga *150*60# Bure pamoja na kuzindua promosheni kabambe itakayowawezesha wateja wa Airtel nchi nzima kutuma pesa bure.
Akiongea wakati wa uzinduzi wa huduma hiyo M'eneja Uhusiano wa Airtel Jackson Mmbando alisema” Airtel tunaendelea kutoa uhuru kwa wateja kupata huduma zetu kirahisi zaidi nchini kote, kuanzia sasa mteja akipiga *150*60# anapelekwa mojakwamoja kwenye horodha yake ya huduma na kuweza kuchagua anachohitaji kufanya ikiwa ni pamoja na kuongeza salio, kufanya malipo, kutoa pesa na mengine mengi.
"Tumefanya hivi hii ili kumwezesha mteja mwenye simu yeyote kupata huduma za kibenki na kuondoa changamoto zozote zitakazojitokeza, sasa mteja anauhuru wa kuchagua kutumia njia ya awali ambayo ni kwenda mojakwa moja kwenye muongozo wa simu yake na kupata horodha(Menu) ya Airtel au kupiga namba *150*60# na kuunganishwa moja kwa moja
vilevile tunayofuraha kuzindua ofa kabambe kwa wateja wetu nchini zima ambapo kutuma au kupokea pesa chini ya kiwango cha 100.000 ni BURE na mteja atakaponunua LUKU kupitia Airtel money ni BURE (hakuna viwango vya miamala vitakavyotozwa).
Tunawajulisha wateja wetu wote na wakala wetu waliosambaa nchi zima kutumia huduma hii iliyorahisi ni rahisi aliongeza” Mmbando
Airtel ni mtandao ulioenea nchini na unatoa huduma za kifedha za Airtel money yenye mawakala zaidi ya 10,000 waliosambaa maeneo mbalimbali mjini na vijijini kwa dhamira ya kupunguza changamoto ya upatikanaji wa huduma za kifedha na kusaidia wateja wetu kuokoa muda kwenda mbali kupata huduma za kibenki.
Kupitia Airtel money mteja anaweza kupata huduma mbalimbali ikiwemo: kupokea pesa, kulipa bill kama DSTV, LUKU na DAWASCO, USA visa , kununua salio na huduma nyingine nyingi

TUHUMA ZA HUJUMA ZAMTESA SURE BOY

KIUNGO wa Azam FC, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, amesema kwamba anasikitishwa na tuhuma zilizozagaa kwamba yeye ni miongoni mwa wachezaji waliocheza chini ya kiwango katika Fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame dhidi ya Yanga, timu yao ikilala
2-0.

Sure Boy Jr. ameiambia BIN ZUBEIRY kwamba tuhuma hizo zinamnyima raha na kwa mara ya kwanza tangu aanze kuchezea Azam, hivi sasa anajisikia mnyonge.

Sure amekana tuhuma hizo hazina ukweli wowote ndani yake na kwamba wanazungumza dhana tu, kitu ambacho ameonya si kizuri na kitaivuruga timu yao.

“Ukiutazama ule mchezo, utaona sisi tulijituma sana, siwezi kusema nani hakucheza kwa uwezo wake wote, muda mwingi tulikuwa kwenye lango lao na tulitengeneza nafasi nyingi kuliko wao. Ila tu bahati haikuwa yetu.

Kuna bao moja Yanga waliokoa mpira ukiwa unaelekea nyavuni na mimi ndiye nilitoa pasi ya mwisho, sasa unasemaje tulihujumu timu? Au kwa kuwa tumefungwa? Mimi kwa kweli sipendi haya maneno.Sisi tulitaka hilo Kombe, lakini bahati haikuwa yetu. Sisi ndio tumeumia zaidi.

Mimi nawashauri viongozi wetu, wayachukulie haya kama matokeo ya kawaida ya mchezo, tusianze kuvurugana saa hizi mapema, tuanze kujipanga kwa ajili ya mechi ya Ngao ya Jamii na Ligi Kuu,”alisema kiungo huyo bora kwa sasa Afrika Mashariki na Kati.

Jumamosi Azam ilifungwa mabao 2-0 na Yanga katika fainali ya Kagame, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kushindwa kutimiza ndoto zake za kuwa timu ya kwanza nje ya Simba na Yanga kutwaa Kombe hilo.

Lakini wengi wanaamini, Sure anakuwa miongoni mwa wanaotuhumiwa kwa sababu baba yake mzazi, Abubakar Salum ni kocha wa timu ya vijana ya Yanga ni pia mchezaji wa zamani wa klabu hiyo.

CHANZO CHA HABARI: BIN ZUBEIRY

Monday, July 30, 2012

AZAM SASA YATANGAZA KUMUUZA NGASA

Siku chache baada ya mchezaji wa kimataifa wa Tanzania ,Mrisho Ngassa kuonekana akiwa amevaa jezi ya Yanga na kuibusu logo ya klabu hiyo, waajiri wake wa klabu ya Azam kupitia ukurasa wao wa mtandao wa kijamii wa Facebook wamesema yafuatayo.
Azam FCKlabu ya Azam FC inapenda kutoa taarifa rasmi kuwa baada ya baada ya mchezaji wetu Mrisho Ngasa kuonesha wazi kuwa na mapenzi na Yanga kwa kuivaa na kuipiga busu Logo ya Yanga, tuliwapa Yanga nafasi ya upedeleo ya kumnunua lakini hadi leo hakuna ofa iliyokuja toka Yanga. simba wametoa ofa na uongozi unatafakari ofa ya SimbaYanga.... Ngasa anauzwa $50,000 wadau wa Yanga tunajua mnampenda sana Ngasa... fikisheni ujumbe kwa uongozi wenu

AIRTEL TANZANIA YAENDELEA KUSAMBAZA MAWASILIANO KANDA YA ZIWA

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais, Mh Charles Kitwanga akikata utepe kuashira uzinduzi wa mawasiliano uliojengwa na Airtel Tanzania, nje kidogo ya mkoa wa Mwanza katika wilaya ya Misungwi ili kurahisisha upatikanaji wa huduma zake zote kama intaneti, Airtel Money na kupiga simu vijiji vya Nyamainza, Buhunda, Ishoke na Seke. Wengine, wa kwanza kulia ni Meneja Uhusiano wa Airtel Tanzania, Jackson Mmbando. Hafla ya uzinduzi wa mnara huu ilifanyika katika kijiji cha Nyamayinza wilayani Misungwi mwishoni mwa wiki



KAMPUNI ya Airtel Tanzania, imezindua mwishoni mwa wiki imezindua mtambo kabambe wa mawasilano katika mkoa wa kanda ya Ziwa nje kidogo ya mkoa waMwanza katika wilaya ya Misungwi, ikiwa ni mkakati wa kampuni hiyo kuendelea kufikisha huduma zao bora vijijini.

Akizindua mnara huo mpya, Naibu Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais, Mh, Charles Kitwanga ‘Mawe Matatu’, alisema Maendeleo vijijini yatakuwakwa kasi sana iwapo wananchi watatumia mawasiliano ya simu za mkononi kutafuta masoko ya madini, mifugo au vyakula anavyozalisha sehemu mbalimbali.

Waziri Kitwanga alibainisha hayo katika kijiji cha Nyamayinza, kata ya Gulumungu wilaya ya Misugwi Mkoani Mwanza wakati akiongea na wananchi na kuzindua mnara wa mawasiliano uliojengwa na kampuni ya Airtel Tanzania.

“Mawasiliano yana faida kubwa sana duniani na ndio hufanya maendeleo ya jamii kwenda kwa kasi, hivyo wananchi wa vijiji vyote vinavyoizunguka Nyamayinza, tumieni fursa ya kupata mawasiliano haya ya Airtel kwa kuendesha au kuendeleza biashara zenu, pia anzisheni biashara za kutuma na kupokea pesa za Airtel Money na mtumie mawasiliano haya haya pia kutafuta wateja wa kutosha katika bidhaa za kilimo na mifugo mnazozalisha,”alisema.

Nae Meneja Mauzo wa Airtel Kanda ya Ziwa Bw, Garlus Mgawe, akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Airtel Tanzania, alisema; “Airtel kwa kukamilisha dhamira yetu ya kutoa mawasiliano yenye uhakika kwa mwaka huu, tunaanza na kuzindua mtambo huu wa mawasiliano hapa wilayani Misungwi, utakaowezesha zaidi ya watu 15,000 waliopo vijiji vya Nyamainza, Buhunda, Ishokela, na Seke kuwasiliana na ndugu na jamaakwa uhakika wakiwa Airtel,”alisema.

Kupatikana kwa mtandao huu wa Airtel, pia kutasaidia wakazi wa vijiji vyote na jirani kufurahia huduma zote za Airtel ikiwemo ile ya Airtel Money, kutuma na kupokea sms, pamoja na kufurahia mtandao bora na nafuu wa Intaneti.

Uboreshwaji na uwekaji wa Minara ya mawasiliano ya Airtel katika vijiji, unawezeshwa kwa ushirikiano na Serikali na Mamlaka za Mawasiliano nchini kwa kuwa imeweka mikakati bora zaidi wakati wa uwekaji wa miundo mbinu hiyo ya mawasiliano kila mahali.

Akiongezea kuhusiana na mpango wa kusambaza mtandao unaoendelea, Meneja Uhusiano wa Airtel Tanzania, Bw Jackson Mmbando alisema; “Kuongezeka kwa mahitaji ya huduma za mawasiliano kutokana na mazingira au kupanuka kwa shughuli za jamii, ndio kunatufanya (Airtel Tanzania) kuitikia wito wa kutanua zaidi wigo wa mtandao wetu kwa maeneo yote.

“Huduma ya mawasiliano imekuwa moja kati ya nyenzo muhimu katika kuwezesha shughuli nyingi za kijamii nchini Tanzania na duniani kote, kupanuka na kufikisha mawasiliano vijijini ni chachu ya kukua kwa uchumi na kuwezesha jamii iliyopo maeneo hayo kupata miundombinu mbadala katika shughuli za uzalishaji.

Airtel bado tunategemea kuendelea kupata ushirikiano wa kutosha kati yetu na serikali katika kuhakikisha tunafikisha mawasiliano vijijini, kwa kutuwekea mfumo bora wa kulipa kodi na kupata vibali vya kuweka mitambo ya mawasiliano ili kufaidisha jamii,”alisema.

Airtel ni mtandao bora ulioenea zaidi na kutoa mawasiliano nchini kote, kwa kufikisha mawasiliano ya uhakikia kwa takribani asilimia 85, kwenye maeneo ya miji na vijiji nchini Tanzania.

KIDUNDA ADUNDWA

Bondia wa Tanzania, Selemani Kidunda (kulia) akiwa hoi baada ya kudundwa kirahisi kwa pointi 20-7 dhidi ya bondia wa Moldova, Vasilii Belous katika pambano la uzito wa welter (69kg) mzunguko wa 32 kwenye Ukumbi wa ExCeL katika michuano ya Olimpiki ya London 2012 leo Julai 29, 2012. Picha: REUTERS

TASWA YAPIGA MARUFUKU SHUGHULI ZOTE ZA CECAFA TANZANIA

CHAMA Cha Waandishi wa Habari za Michezo (TASWA), kimesikitishwa na hatua ya Baraza la Michezo la Vyama vya michezo la Afrika Mashariki (CECAFA), kuwanyanyasa na kuwadhalilisha waandishi wa habari katika mchezo wa fainali Jumamosi iliyopita kwenye uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
Kufuatia kudhalilishwa huko kwa waandishi katika fainali hiyo ya michuano ya kombe la Kagame kati ya Yanga na Azam, TASWA imelaani kitendo hicho na kuwaondolea utu, udhalilishaji na unyanyasaji kulikosababishwa na baadhi yao kutandikwa makofi na askari polisi mithiri ya vibaka.
Waandishi wa habari za michezo wa Tanzania wamekuwa wasikivu, waadilifu na watu wanaofuata taratibu, lakini katika fainali hiyo mara baada ya mchezo walifanyiwa vitendo ambavyo havikulingana na tabia yao.
Lengo la waandishi si kuleta vurugu bali kuhakikisha wananchi wanapata habari kwa kila tukio lilikuwa linatokea uwanja, badala yake walionekana hawana thamani mbele ya jamii inayowawakilisha.
TASWA inalaani kitendo cha Katibu Mkuu wa CECAFA, Nicolas Musonye kwa kutoa agizo kwa polisi kuwazuia waandishi kuingia uwanjani kumalizia kazi zao za kuhoji makocha na wachezaji, hali iliyosababisha vurugu.
CECAFA walijenga urafiki wa karibu na waandishi kipindi chote cha mashindano hayo na Kagame kwa lengo la kuyatangaza , lakini mwisho wa yote walionekana kama taulo la deki limekuwa na thamini pale ambapo linahitajika kwa deki, lakini baada ya hapo halina thamani tena.
Lakini TASWA inafanya uchunguzi juu ya tukio hilo, kufuatia baadhi ya waandishi kuonesha utovu wa nidhamu kama baadhi ya viongozi wa TFF na CECAFA walivyodai kuwa walionesha vitendo vya utovu wa nidhamu kwa kutoa maneno ya kashfa na kutaka kumpiga Musonye
Kufuatia hatua hiyo TASWA imechukua maamuzi yafuatayo
1.Kutoandika jambo lolote linahusu Shirikisho la vyama vya michezo Afrika Mashariki (CECAFA).
2.Kutoandika jambo lolote linahusu mashindano yoyote yaliyo chini ya CECAFA.
Ili kuweza kufanya kazi pamoja na CECAFA,TASWA inataka kuombwa radhi na CECAFA kutokana na kitendo hicho na kuwalipa fidia waandishi ambao wamepoteza vifaa vya vya kazi na wengine kuhalibiwa vifaa vyao.
TASWA inatoa onyo kali kwa baadhi ya vyama,viongozi na makampuni wenye tabia ya kutotoa ushirikiano na dharau kwa waandishi wanapokuwa kwenye kazi zao.

Juma Abbas Pinto
CHAIRMAN
Julai 30, 2012

Sunday, July 29, 2012

YANGA BINGWA KOMBE LA KAGAME

Wachezaji wa Yanga wakiwa na kombe la ubingwa wa michuano hiyo

Wachezaji wa Yanga na Azam wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa CECAFA

Wachezaji wa Yanga wakishangilia moja ya mabao yao



Yanga jana iliweka rekodi ya kutwaa ubingwa wa michuano ya soka ya Kombe la Kagame baada ya kuichapa Azam mabao 2-0 katika mechi kali ya fainali iliyopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Washambuliaji Hamizi Kiiza na Saidi Bahanuzi ndio waliowezesha Yanga kutwaa taji hilo kwa mara ya pili mfululizo baada ya kuifungia mabao hayo mawili, moja katika kila kipindi.

Katika mechi hiyo iliyohudhuruwa na mashabiki lukuki, Azam ilishindwa kabisa kuonyesha cheche zake kutokana na mfumo uliokuwa ukitumiwa na Yanga wa kujaza mabeki wengi nyuma na kuacha washambuliaji wawili mbele.

Kwa kutumia mfumo huo, washambuliaji wa Azam walishindwa kabisa kuipenya ngome ya Yanga na kucheza zaidi katikati ya uwanja, ambako viungo wake walitawala.

Kilichoiwezesha Yanga kulishambulia lango la Azam mara kwa mara ni wachezaji wake wa kiungo na mawinga wa pembeni kupanda wanafanya mashambulizi na kurudi nyuma wakati lango lao likiwa linashambuliwa.

Kutokana na ushindi huo, Yanga ilizawadiwa kitita cha dola 30,000 za Marekani wakati Azam ilizawadiwa dola 20,000. AS Vita ya DRC ilizawadiwa dola 10,000 kwa kushika nafasi ya tatu baada ya kuichapa APR ya Rwanda mabao 2-1.

Friday, July 27, 2012

SHIGONGO AJIBU MAPIGO YA CHAMELEONE

Mkurugenzi wa Global Publishers, Eric Shigongo(kulia) akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) juu ya sakata lake na Chameleone. Kushoto ni Meneja Mkuu wa Global Publishers, Abdallah Mrisho.



MD wa Global Publishers Ltd, Eric Shigongo, mapema leo ameongea na media kuhusu madai ya Jose Chameleone kudai paspoti yake, ambaye jana alikwenda Ubalozi wa Tanzania nchini kwake Uganda kushinikiza kurejeshewa paspoti yake.


Eric amefunguka kwa kusema kuwa, kampuni yake na msanii huyo waliingia makubaliano ya kufanya shoo kwenye Tamasha la Usiku wa Matumaini, liliofanyika Uwanja wa Taifa Julai 7 mwaka huu, ambapo katika mazungumzo ya awali, msanii huyo aliomba kulipwa dola 5000 na kulipiwa tiketi 2 za ndege ili kuhudhuria tamasha hilo, masharti ambayo yalikubaliwa.


Mazungumzo hayo ya awali yalifanyika kati ya Global Publishers na agenti wa Chameleone ajuliikanae kwa jina la George. Kabla ya kutuma fedha hizo, kampuni yake ilihitaji kujiridhisha kama ajenti huyo alikuwa kweli anawasilina na kukubaliana na Chameleone kuhusu shoo ya Dar, ili kuepuka utapeli.


“Tulipokubaliana nae kupitia ajenti wake, tuliamua kwenda mbele zaidi ili kujiridhisha, ambapo tuliwasiliana na mwanamuziki Kidumu ambaye anamfahamu huyo George na kwenda mpaka Kampala kukutana ana kwa ana na wahusika, kwa niaba yetu”, alisema Shigongo.


Akielezea zaidi, Shigongo alisema kuwa Kidumu alikwenda Kampala na kukutana na George pamoja na Jose Chameleone, ambaye alikubali kuja kufanya shoo na kumruhusu Kidumu kusainishana mkataba na ajenti wake na kumpatia hizo fedha.


“Chameleone alitoa ruhusa kwa ajenti wake kusaini mkataba na kupokea advance ya dola 3,500 kwa niaba yake kwa madai kuwa yeye asingeweza kusubiri malipo wakati huo kwa sababu alikuwa anawahi sehemu nyingine.


“Baadae Jose alikuja kugeuka na kudai hakupewa hizo pesa na ajenti wake, kitu ambacho kilonekana kama mchezo wa kitapeli kati ya Chameleone na ajenti wake kwetu sisi.


“Kwa kuwa ujio wake Tanzania ulikuwa umeshatangazwa sana, uongozi wa Global Publishers, ulilazimika kufanya mazungumzo mengine na Chameleone na kumuomba sana kuja nchini kufanya shoo, ambapo this time akakubali kwa masharti ya kulipwa dola 8000 na tiketi nne za ndege.


“Ndugu zangu, sikua na jinsi, nililazimika kumkubalia na kumlipa dola 8000, kwa sababu tayari tamasha lilikuwa limeshatangazwa sana, billboards zimewekwa barabarani na promosheni kubwa ilikuwa inafanyika,” alisema Shigongo kwa uchungu.


Hivyo mara baada ya kukubaliana, safari hii akalazimika kumtuma meneja wake kwenda mpaka Kampala na kukutana na Chameleone ana kwa ana na kumpatia dola 8000 na kusaini mkataba mwingine wa pili.


“Ni dhahairi kabisa alichokifanya Chameleone kilikuwa ni utapeli kwa kushirikiana na ajenti wake, kwa sababu tunamuamini Kidumu, ambaye tumeshafanya naye kazi mara kadhaa kwa uaminifu mkubwa. Pia ni Chameleone ndiye aliyemuidhinisha ajenti wake kuchukua pesa hizo, hivyo ulikuwa ni mchezo wa pamoja, na hiyo ni tabia ya Chameleone, kwani ameshawafanyia mapromota wengi kiasi kwamba hivi sasa hakanyagi nchini Kenya.


“Dola 3,500 siyo fedha nyingi, ningeweza kuzisamehe, lakini nimeamua kuzidai kwa manufaa ya watu wengine. Watanzania tusikubali kufanywa wajinga kwa sababu ya upole wetu, tutaendelea kudhauriwa na kufanywa wajinga mpaka lini,” alihoji Shigongo.


Mwisho Shigongo alitoa wito kwa Watanzania kuungana katika suala hili, kwani Chameleone ameonyesha dharau kubwa kwa Watanzania kwa kumfuata balozi wetu nchini Uganda na kuondoka ofisini kwake huku akisonya na kubamiza mlango, akiendelea kuonyesha dharau kwa Watanzania wote wapatao miloni 40!

KEPTENI KOMBA AREJEA KUTOKA INDIA

Kepteni John Komba akiwa na mkewe Salome, nyumbani kwake Mbezi, Dar es Salaam.


MKURUGENZI wa Kundi la Tanzania One Theatre (TOT), ambaye pia ni Mbunge wa Mbinga Magharibi, John Komba amerejea nchini kutoka India, ambako alikwenda kufanyiwa upasuaji kwa ajili ya kumtibu ugonjwa wa nyonga uliokuwa ukimsumbua upande wa mguu wake wa kulia.


Akizungumza na waandishi wa habari leo, nyumbani kwake Mbezi kwa Komba, mjini Dar es Salaam, Komba alisema alirejea nchini juzi baada ya kupatiwa matibabu hayo kwenye hospitali ya Appolo iliyopo Hydrabad nchini India tangu mwanzoni mwa wezi huu.


Komba alisema, aliondoka nchini Julai 2, 2012 baada ya kupelekwa na serikali kwa maelekezo ya Rais Jakaya Kikwete, Spika wa Bunge Anna Makinda na Katibu wa Bunge John Kashilila na kwamba alikwenda baada ya kukosa matibabu hapa nchini kwa sababu ya mgomo wa madaktari.


"Siku napelekwa Muhimbili tu, tayari madaktari walikuwa wameanza siku ya kwanza ya mgomo wao, nikawa sina namna ila kuujulisha uongozi wa Bunge na kisha nikamuomba Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete, naye kwa mamlaka yake akanisaidia haraka kama ambavyo huwasaidia wengine kwenda kutibiwa nje", alisema Komba.


Alisema uzito ulichangia sana kusababisha mifupa kusagana kwenye nyonga upande wa mguu wa kulia, ambapo hadi anakwenda India, alikuwa na uzindo wa kilo 138 wakati wastani wa uzito aliotakiwa kuwa nao kulingana na ukubwa wa mwili wake ni kilo 90 au 100 tu.


Komba alisema baada ya matibabu, amerejea nchini akiwa na uzito wa kilo 128, ambao hata hivyo ametakiwa kuudhibiti na kuupunguza katika siku ambazo atalazimika kupumzika nyumbani kabla ya kuanza kazi Septemba mwaka huu kama alivyoelekezwa na madaktari.

Akizungumzia upasuaji ulivyoendeshwa, Komba alisema ulichukua saa tano na kukamilika bila matatizo. Alisema katika upasuaji huo, sehemu iliyopasuliwa ni ya ukubwa wa futi moja.

Hata hivyo, alisema baada ya upasuaji huo, hakuweza kurejea katika wodi ya kawaida kwa sababu magonjwa kadhaa yaliibuka, ikiwemo homa kali na presha hivyo akalazimika kulazwa katika wodi ya wagonjwa waliopo kwenye uangalizi maalum (ICU) kwa siku tano.

"Sasa nimerejea nikiwa mzima, kwa sasa natumia fimbo hii, ili kuwezesha uzito usielemee upande wa kulia nilikopanyiwa upasuaji, lakini sijambo kabisa," alisema Komba.

Komba alilaani baadhi ya vyombo vya habari, ambavyo viliripoti kwamba katika kuugua kwake alikuwa mahututi na kwamba alikuwa anaugua figo.

"Jamani ninyi waandishi wa habari, jizoesheni kuandika habari zilizokamilika siyo kurashia-rashia tu na kuzusha uongo. Mfano gazeti moja liliandika eti naugua figo, nipo mahututi wakati si kweli kabisa, ilikuwa jambo rahisi tu, kuja hapa nyumbani na kuniuliza au kuuliza mke wangu lingepata kwa uhakika ninachoumwa", alisema Komba.

NGASA AICHEFUA AZAM

Ngasa akiondoka kwenye jukwaa la mashabiki wa Yanga baada ya kuzawadiwa jezi

Ngasa akianza kuvaa jezi yenye rangi ya kijani na njano aliyopewa na mashabiki wa Yanga wakati Azam ilipokuwa ikimenyana na AS Vita ya DRC.

Ngasa akivaa jezi ya Yanga aliyopewa na mashabiki wa tawi la Yanga Bomba wakati Azam ilipomenyana na AS Vita ya DRC wakati wa mechi ya nusu fainali ya Kombe la Kagame Ngasa akielekea kwenye mlango wa kuingia uwanjani baada ya kuvaa jezi ya Yanga (Picha zote na Emmanuel Ndege wa blogu ya liwazozito)


Mshambuliaji Mrisho Ngasa juzi alifanya vitendo vya ajabu wakati timu yake ya Azam ilipokuwa ikimenyana na AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo katika mechi ya nusu fainali ya michuano ya Kombe la Kagame.

Katika mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Ngasa aliingia uwanjani kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Kipre Tchetche.

Kituko chake cha kwanza ni kwenda kushangilia bao la pili aliloifungua Azam katika mechi hiyo kwenye jukwaa wanalokaa mashabiki wa Yanga.

Muda wote wa pambano hilo, mashabiki hao walikuwa wakiizomea Azam, lakini baada ya mchezaji huyo kufunga bao na kuwafuata, walianza kumshangilia kwa mayowe mengi.

Kama hiyo haikutosha, mara baada ya pambano hilo kumalizika, Ngasa alikwenda kuungana na wachezaji wenzake kushangilia ushindi, badala yake alikwenda tena kwenye jukwaa la mashabiki wa Yanga, ambao walizidi kumshangilia.

Mbali na kumshangilia, mashabiki hao wa tawi la Yanga Bomba, walimzawadia Ngasa jezi yenye rangi ya kijani na njano, ambayo aliipokea na kuivaa mara moja na kisha kutokomea nayo nje ya uwanja, akipitia mlango maalumu wa dharula, mahali linapoegeshwa gari la wagonjwa.

Wakati Ngasa akitokomea nje ya uwanja, wachezaji wenzake pamoja na viongozi waliunda duara uwanjani wakiomba dua na kumshukuru Mungu kwa kuweza kushinda pambano hilo.

Mmoja wa maofisa wa Azam, ambaye hakupenda jina lake litajwe gazetini, alikiri kuwa, uongozi umekerwa na kitendo hicho cha Ngasa na huenda ukamchukulia hatua za kinidhamu.

Mechi hiyo ilikuwa ya kwanza kwa Ngasa tangu michuano ya Kombe la Kagame ilipoanza wiki mbili zilizopita.

Kocha Stewart Hall hakuwa anamchezesha kwa madai kwamba, alikuwa hajitumi mazoezini na kuonyesha dalili za kutaka kucheza.

Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya soka wamekielezea kitendo hicho cha Ngasa kuwa kilikuwa ishara ya kumwonyesha Stewart kwamba uwezo wake bado upo juu.

Wengine wamekitafsiri kuwa, kilikuwa ishara ya kuitaka Azam imruhusu arejee Yanga, timu aliyoichezea kwa miaka kadhaa kabla ya kununuliwa na wana rambaramba kwa kitita cha zaidi ya sh. milioni 50.

JOSE CHAMELEONE AVAMIA UBALOZI WA TANZANIA NCHINI UGANDA, ASHINIKIZA AREJESHEWE PASIPOTI YAKE

Chameleone akiteta jambo na mmoja kati ya wafuasi wake nje ya ofisi za ubalozi wa Tanzania nchini Uganda.

Chameleone akipiga gita huku wafuasi wake wakiwa wamebeba mabango nje ya ofisi za ubalozi wa Tanzania nchini Uganda.

Polisi wa Uganda wakimtuliza Chameleone na wafuasi wake wakati walipofanya maandamano ya amani nje ya ofisi za ubalozi wa Tanzania nchini Uganda.

Ofisa mmoja wa polisi akizungumza na wafuasi wa Chameleone nje ya ofisi za ubalozi wa Tanzania nchini Uganda.


Mwanamuziki Jose Chameleone na wafuasi wake jana asubuhi walivamia kwenye ofisi za ubalozi wa Tanzania nchini Uganda na kushinikiza arejeshewe pasi yake ya kusafiria.


Jose, mmoja wa wanamuziki tajiri katika nchi za ukanda wa Afrika, aliendesha gari lake aina ya Range Rover Sport na kuliegesha karibu na ubalozi huo.


Mwanamuziki huyo pamoja na wafuasi wake walikuwa na mabango yaliyokuwa na maandishi yanayomtaka mfanyabiashara Eric Shigongo arejeshe hati yake ya kusafiria.


Jose aliweka kambi kwa muda nje ya ubalozi huo na kupiga gita lake huku akiimba nyimbo mbali mbali. Wafuasi wake walikuwa wamebeba mabango ya kupinga kitendo cha Shigongo kumnyang'anya hati yake ya kusafiria.


Baadhi ya mabango yalisomeka: 'Shigongo upo juu ya sheria?' , 'Tafadhali Tanzania nisaidieni', 'Nahitaji nirejeshewe hati yangu ya kusafiria'.


Shigongo ndiye aliyemwalika Jose kufanya onyesho wakati wa tamasha la matumaini lililofanyika hivi karibuni kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.


Jose alifanya onyesho wakati wa tamasha hilo, lakini inasemekana kuwa Shigongo alikataa kumlipa pesa zake kwa madai kuwa, tayari alishamlipa meneja wa mwanamuziki huyo, aliyejulikana kwa jina la George.


Imeelezwa kuwa, Shigongo alimlipa George dola 3,500 za Marekani kwa ajili ya Jose kufanya onyesho hilo, lakini mwanamuziki huyo alikana kumtambua meneja huyo.


Jose alifanikiwa kuondoka nchini baada ya kupewa hati ya muda ya kusafiria katika ofisi za ubalozi wa Uganda hapa nchini.


Uamuzi wa Jose kuvamia ubalozi wa Tanzania nchini Uganda, ulifanyika saa chache baada ya kutoka kufanya onyesho kwenye Uwanja wa Amahoro mjini Kigali, Rwanda.


Maofisa kadhaa wa polisi wa Uganda walifika kwenye ofisi za ubalozi huo wakiwa na gari yenye namba UP-2627 kwa ajili ya kulinda usalama.


Hata hivyo, Jose aliwaeleza polisi hao kuwa, yeye na wenzake waliamua kufanya maandamano ya amani kwa lengo la kushinikiza arejeshewe hati yake ya kusafiria.


Baadaye, nyota huyo wa muziki alikutana na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Uganda, ambaye alimuahidi kwamba atalifanyia kazi suala lake kwa kuwasiliana na Mkuu wa Jeshi la Polisi la Tanzania, Inspekta Saidi Mwema.

Thursday, July 26, 2012

YANGA, AZAM USO KWA USO FAINALI YA KOMBE LA KAGAME

Mshambuliaji Hamisi Kiiza (kulia) wa Yanga akijiandaa kumtoka beki wa APR ya Rwanda wakati wa pambano lao la leo.


Mshambuliaji Kipre Tchetche (kulia) wa Azam akitafuta mbinu za kumtoka beki wa AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.


Yanga na Azam leo zimefuzu kucheza fainali ya michuano ya soka ya Kombe la Kagame baada ya kuibuka na ushindi dhidi ya APR ya Rwanda na AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.

Katika mechi hizo za nusu fainali zilizochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Yanga iliichapa APR bao 1-0 wakati Azam iliicharaza AS Vita mabao 2-1.

Mshambuliaji Mrisho Ngasa aliibuka shujaa wa Azam baada ya kuifungia bao la pili katika kipindi cha pili na kwenda kushangilia bao hilo kwenye jukwaa la mashabiki wa Yanga, ambao awali walikuwa wakiwazomea wachezaji wa Azam.

Katika kudhihirisha mapenzi yake kwa Yanga, mara baada ya mchezo huo kumalizika, Ngasa badala ya kupongezana na wachezaji wenzake wa Azam, alikwenda tena kwenye jukwaa la mashabiki wa klabu hiyo, ambao walimshangilia na kumkabidhi jezi ya njano, ambayo aliipokea na kutokomea nayo jukwaani.

Pambano kati ya Yanga na APR lilikuwa na upinzani mkali kutokana na timu zote mbili kucheza kwa kukamiana na hivyo kulifanya liwe gumu kutabirika.

Ilibidi Yanga isubiri hadi dakika 30 za nyongeza kupata bao hilo pekee na la ushindi baada ya timu hizo kumaliza dakika 90 zikiwa suluhu.

Uzembe wa mabeki wawili wa APR kuzozana na mchezaji mmoja wa Yanga, aliyeangushwa chini ndio uliosababisha kupatikana kwa bao hilo.

Rashid Gumbo, aliyeingia kipindi cha pili alitumia fursa hiyo kurusha mpira kwa haraka, ukamkuta Haruna Niyonzima, aliyemimina krosi golini, ikamkuta Hamisi Kiiza, aliyeunganisha wavuni kwa kifua.

Bao hilo lilipokewa kwa furaha kubwa na mashabiki wa Yanga, ambao muda mwingi wa mchezo huo walikuwa kimya kutokana na kutoamini iwapo timu yao ingeibuka na ushindi.

Kwa matokeo hayo, Yanga na Azam sasa zitakutana katika fainali ya michuano hiyo itakayopigwa Jumamosi kuanzia saa 10 jioni.

Mechi hiyo itatanguliwa na ile ya kutafuta mshindi wa tatu kati ya APR na AS Vita itakayopigwa kuanzia saa nane mchana.Bingwa wa michuano hiyo atazawadiwa kitita cha dola 30,000, wa pili dola 20,000 na wa tatu dola 10,000.

Wednesday, July 25, 2012

YANGA, APR KIAMA LEO

Mshambuliaji Olivier Karekezi wa APR ya Rwanda

Kiungo Haruna Niyonzima wa Yanga. Zamani alikuwa mchezaji wa APR


MABINGWA watetezi wa michuano ya soka ya Kombe la Kagame, Yanga leo wanashuka dimbani kumenyana na APR ya Rwanda katika mechi ya nusu fainali itakayopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Pambano hilo litatanguliwa na mechi nyingine ya nusu fainali kati ya Azam na AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo litakalopigwa kuanzia saa nane mchana.
Mechi zote mbili zinatarajiwa kuwa na upinzani mkali kwa vile timu zitakazoshinda si tu kwamba zitafuzu kucheza fainali, bali pia zitajihakikishia zawadi ya dola 50,000 za Marekani zitazotolewa kwa mshindi wa kwanza na wa pili.
Bingwa wa michuano hiyo atazawadiwa dola 30,000, wa pili dola 20,000 na wa tatu dola 10,000. Fedha hizo zimetolewa na Rais Paul Kagame wa Rwanda.
Yanga imetinga nusu fainali baada ya kuitoa Mafunzo ya Zanzibar kwa penalti 5-3 baada ya timu hizo kumaliza dakika 90 zikiwa sare ya bao 1-1. Nayo APR ilitinga hatua hiyo baada ya kuitoa URA ya Uganda kwa mabao 2-1.
Akizungumzia mechi hiyo juzi, Kocha Mkuu wa Yanga, Tom Saintfiet alikiri kwamba itakuwa ngumu kwa vile wapinzani wao hawawezi kukubali kufungwa mara mbili.
Yanga iliichapa APR mabao 2-0 katika mechi ya mwisho ya hatua ya makundi, kipigo ambacho kilipokelewa kwa furaha kubwa na mashabiki wa klabu hiyo.
“Ni vigumu kwa timu kukubali kufungwa mara mbili na timu moja katika michuano ile ile. Binafsi nilikuwa naomba dua APR ifungwe na URA ili tusikutane nayo tena,”alisema.
Washambuliaji Hamizi Kiiza, Saidi Bahanuzi na beki Nadir Haroub ‘Cannavaro’ walionyesha wasiwasi wao kuhusu mechi hiyo, lakini waliapa kupambana kufa na kupona ili waweze kushinda na kufuzu kucheza fainali.
“Mechi itakuwa ngumu kwa sababu wapinzani wetu lazima watacheza kwa nguvu zao zote, lakini nasi tumejiandaa vizuri,”alisema Bahanuzi.
Kwa upande wake, Cannavaro alisema hawatakuwa tayari kupoteza mechi hiyo kwa vile wakifungwa, watakuwa wamewaangusha mashabiki wao, ambao wamekuwa wakiwaunga mkono kwa nguvu zote.
Katika kuhakikisha timu yao inaibuka na ushindi, kamati ya utendaji ya Yanga jana iliitisha kikao cha dharula kwa ajili ya kuweka mikakati ya kushinda mechi hiyo.
Moja ya maamuzi yaliyofikiwa katika kikao hicho ni kukutana na wachezaji leo asubuhi na kuahidi kuwapa zawadi kubwa iwapo watashinda mechi hiyo na kusonga mbele.
Kocha Mkuu wa APR, Ernest Brandy alikiri kwamba Yanga ni timu nzuri, lakini aliahidi kuwepo kwa mabadiliko makubwa katika mchezo wa leo.
Kocha huyo alisema hawakucheza kwa nguvu katika mechi ya awali kwa sababu walishakuwa na uhakika wa kusonga mbele, lakini safari hii hawatakuwa na mzaha.
Nahodha wa timu hiyo, Olivier Karekezi alisema kazi yake leo itakuwa ni moja tu, kumdhibiti kiungo wa Yanga, Haruna Niyonzima, ambaye alisema anamfahamu vyema.
Karekezi alisema amecheza pamoja na Niyonzima alipokuwa APR na waliwahi kwenda kufanya majaribio ya kucheza soka ya kulipwa pamoja katika nchi za Ufaransa na Sweden, hivyo anafahamu vyema jinsi ya kumdhibiti.
Wakati huo huo, Kocha Mkuu wa Azam, Stewart Hall amekiri kuwa pambano lao la leo dhidi ya AS Vita litakuwa gumu na lenye ushindani mkali.
Stewart alisema jana kuwa, ugumu wa pambano hilo unatokana na ukweli kwamba kikosi cha AS Vita kinaundwa na wachezaji wengi wazuri na wenye uzoefu wa michuano ya kimataifa.
Hata hivyo, kocha huyo kutoka Uingereza alisema, wamejipanga vyema kuhakikisha wanashinda mechi hiyo na kutinga hatua ya fainali.
Taarifa iliyotolewa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) jana ilieleza kuwa, viingilio katika mechi hiyo vitakuwa sh. 5,000, sh. 7,000, sh. 15,000 na sh. 20,000.

MILOVAN ALALAMIKIA MAANDALIZI SIMBA

KOCHA Mkuu wa Simba, Milovan Cirkovic amesema kutolewa
mapema kwa timu yake katika michuano ya Kombe la Kagame
kumechangiwa na maandalizi hafifu.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya timu hiyo
kuchapwa mabao 3-1 na Azam juzi kwenye Uwanja wa Taifa, Dar
es Salaam, kocha huyo alisema Simba haikufanya maandalizi ya
kutosha kabla ya kushiriki michuano hiyo.
Milovan alikiri kuwa kikosi chake bado dhaifu kutokana na
kuundwa na wachezaji wengi wapya na pia wachezaji wake bado
hawajaweza kucheza kwa uelewano mkubwa.
Alisema alishalibaini tatizo hilo kabla hata ya kuanza kwa
michuano ya Kombe la Kagame na alishawaeleza mapema
viongozi wa klabu hiyo.
“Bado sina kikosi kizuri, ambacho unaweza kujivunia wakati
unashiriki katika michuano migumu kama hii," alisema.
Milovan alisema licha ya timu yake kutwaa ubingwa wa Kombe la
Urafiki kwa kuifunga Azam kwa njia ya penalti, bado hajaweza
kuunda kikosi imara na chenye ushindani.
“Lazima timu ipate maandalizi ya kutosha kabla ya kushiriki
mashindano makubwa kama haya. Kwa muda, ambao Simba
imejiandaa, tusingeweza kufika mbali,”alisema.
Aliimwagia sifa Azam kwa kusema ni timu nzuri na wachezaji
wake wanacheza kwa uelewano mkubwa kutokana na kukaa
pamoja kwa muda mrefu.
Hata hivyo, kocha huyo alisema ataendelea kukiimarisha kikosi
chake kabla ya kuanza kwa msimu ujao wa ligi na kuhakikisha
wanatetea taji lao. Ligi hiyo imepangwa kuanza Septemba mwaka
huu.

WAPINZANI WA NGORONGORO WATUA DAR

TIMU ya soka ya Taifa ya vijana wa chini ya umri wa miaka 20 ya
Nigeria (Flying Eagles) ilitarajiwa kuwasili nchini jana kwa ajili ya
pambano lake la michuano ya Afrika dhidi ya timu ya vijana wa
umri huo ya Tanzania, Ngorongoro Heroes.
Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface
Wambura alisema jana kuwa, timu hiyo ilitarajiwa kuwasili saa 10 jioni kwa ndege ya RwandAir ikiwa na msafara wa watu 30,
wakiwemo wachezaji 18.
Flying Eagles itapambana na Ngorongoro Heroes katika mechi ya
kwanza ya raundi ya pili itakayofanyika Jumapili kwenye Uwanja
wa Taifa, Dar es Salaam. Mechi hiyo imepangwa kuanza saa 10
jioni.
Mechi hiyo ya kuwania tiketi ya kucheza fainali za 18 za Afrika kwa
vijana wenye umri chini ya miaka 20 zitakazochezwa mwakani
nchini Algeria, itachezeshwa na waamuzi kutoka Kenya wakati
kamishna ni Charles Masembe kutoka Uganda.
Flying Eagles inayofundishwa na kocha John Obuh juzi ilicheza
mechi ya kirafiki na Rwanda (Young Amavubi) kwenye Uwanja wa
Amahoro jijini Kigali. Nigeria ililala bao 1-0.
Msafara wa timu hiyo unaongozwa na Mwenyekiti wa Kamati ya
Ufundi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Nigeria (NFF), Chris
Green.
Baadhi ya wachezaji waliomo katika kikosi cha Flying Eagles ni
Chidi Osuchukwu, Alhaji Gero, Shehu Abdullahi, Aminu Umar,
Aliyu Mohamed, Uche Agbo, Jonah Usman, Harrison Egbune,
Hassan Abubakar na Yahya Adamu.
Viingilio katika mechi hiyo vitakuwa sh. 3,000 kwa viti vya rangi ya
chungwa, bluu na kijani wakati VIP B na C itakuwa sh. 5,000.
Kiingilio kwa VIP A itakuwa sh. 10,000.

SIMBA YAITISHA MKUTANO MKUU AGOSTI 5

UONGOZI wa klabu ya Simba umeitisha mkutano mkuu wa
wanachama uliopangwa kufanyika Agosti 5 mwaka huu kwenye
ukumbi wa bwalo la maofisa wa Polisi, Oysterbay mjini Dar es
Salaam.
Simba imeitisha mkutano huo siku moja baada ya kutupwa nje ya
mashindano ya Kombe la Kagame katika hatua ya robo fainali
baada ya kuchapwa mabao 3-1 na Azam.
Ofisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga alisema mjini Dar es
Salaam jana kuwa, mkutano huo unatarajiwa kujadili masuala
mbali mbali yanayoihusu klabu hiyo.
Alizitaja baadhi ya ajenda zitakazojadiliwa katika mkutano huo
kuwa ni pamoja na ripoti ya mapato na matumizi na maandalizi
ya michuano ya ligi kuu ya Tanzania Bara na klabu bingwa Afrika.
Ili kufanikisha kufanyika kwa mkutano huo, Kamwaga alisema
klabu yake jana ilipokea msaada wa sh. milioni 20 kutoka kwa
Kampuni ya Bia Tanzania (TBL).
Hundi ya pesa hizo ilikabidhiwa kwa Makamu Mwenyekiti wa
Simba, Geofrey Nyange ‘Kaburu’ na Meneja wa Bia ya
Kilimanjaro, George Kavishe katika hafla iliyofanyika makao makuu
ya kampuni hiyo, Ilala, Dar es Salaam.
Kamwaga alisema wakati wa mkutano huo, watazindua Wiki ya
Simba na Jamii, ambayo itawahusu wachezaji, viongozi na
makocha kufanya ziara katika hospitali mbali mbali pamoja na
kutoa misaada kwa wagonjwa na watoto yatima.
Kwa mujibu wa Kamwaga, Simba pia imeandaa tamasha la kila
mwaka la klabu hiyo linalotarajiwa kufanyika Agosti 8 mwaka huu
kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
“Maandalizi ya tamasha hilo (Simba Day) yameshaanza na
yanaendelea vizuri na kwa sasa kocha wetu yupo kwenye harakati
za kuboresha timu,”alisema Kamwaga.
Kwa upande wake, Kavishe aliahidi kuwa, siku hiyo
watawakabidhi viongozi wa Simba basi jipya litakalokuwa
likitumiwa na wachezaji kwa ajili ya kusafiri mikoani.

MAKAMBA AMJIBU ZITTO KUHUSU ON MOBILE

NAIBU Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia jana alimuumbua mbunge wa Kigoma Kaskazini Zuberi Zitto kuwa serikali ilishaisimamisha kampuni ya Onmobile kuendelea kufanya kazi toka mwezi Juni mwka huu.
Alisema serikali iliamua kuisimamisha kampuni hiyo kuendelea kufanya kazi baada ya kampuni hiyo kuandika barua ya kuomba leseni.
Makamba alisema baada ya serikali kuipokea barua hiyo tarehe 29 february mwaka huu iliijibu barua hiyobaada ya kubaini mapungufu mbalimbali katika maombi hayo.
Naibu huyo alisema baadhi ya mapungufu hayo ni pamoja na kampuni hiyo kutosajiliwa BRELA na kutoa mchanganuo wa kibishara.
Hata hivyo, alisema baada ya serikali kugundua kuwa pamoja na kuomba leseni pia kampuni hiyo ilikuwa ikiendelea kufanya kazi kupitia kampuni za Vodacom na Airtel
Alisema hivyo hoja iliyotolewa na Zitto kuwa kampuni hiyo inafanya kazi bila leseni ilishagunduliwa na serikali na kuchukuliwa kwa hatua.
Akizungumzia kuhusiana na wizi wa kazi za wasanii, Makamba alisema serikali haitakubali kuona wasanii hao wanaibiwa kazi zao.
Alisema vita dhidi ya wizi wa kazi hizo ilianza toka mika ya 2009 ambako Rais Jakaya Kikwete alitoa jumla ya sh .milioni 16 kutoka kwenye mfuko wa Rais kwa ajili ya kumlipa mshauri mwelekezi kushauri TRA kuweka stika katika kazi za wasanii hao.
Naibu huyo alisema kabla ya kuondoka katika Ofisi ya Rais, yeye ndiye aliyetumwa na Rais kwenda kuonana na watalaamu mbalimbali ili kuangalia uwezekano wa kusaidia wasanii hao.
“Hivyo vita hii ilianza na Mheshimiwa Rais Mwenyewe na alinituma mimi nikaenda sehemu mbalimbali na tulifanya vikao na wasanii nikiwa mwenyekiti kujadiri maslahi yao’’
“Pia Rais Kikwete ndiye Rais wa kwanza ambaye aliwashirikisha wasanii wa Bongo Fleva na hata katika kampeni zake za uchaguzi Mkuu wa Rais mwka 2009’’
Makamba alisema ni haki ya msanii kulipwa mrahaba kwa kila wimbo wake unapotumiwa na kamapuni ya simu au hata redio.
Alisema serikali itaendelea kuwapigania wasanii hao pale makampuni ya simu yanapotumia nyimbo zao kwani ni haki yao.

ZITTO AZILIPUA KAMPUNI ZA SIMU

MBUNGE wa Kigoma Kaskazini Kabwe Zitto (CHADEMA), amezilipua kampuni za simu nchini kwa kuwanyonya watanzania hasa wasanii wa muziki kutokana na kuingiza mamilioni ya shilingi na kuwalipa kiduchu.
Amesema kampuni hizo ikiwemo Vodacom na Airtel zimekuwa zikiingiza kiasi cha sh. bilioni 43 kwa mwaka kwa kupitia Kampuni ya On Mobile kutokana na tozo za miito ya simu ambayo ni kazi za wasanii nchini. Pia amesema kuwa kampuni hiyo haijasajiliwa hivyo inaendesha shughuli zake kinyume cha taratibu na kutaka hatua zichukuliwe.
Zitto, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mashirika ya Umma, alilipua bomu hilo bungeni jana wakati akichangia hotuba ya makadirio ya Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, ambapo alisema huo ni wizi na unyonyaji kwa watanzania.
Alisema kampuni hizo hutoza sh. 400 kwa siku kwa kutumia nyimbo hizo za miito na sh.37 kila unapotumia miito hiyo, lakini msanii wa Tanzania amekuwa akiambulia asilimia saba ya mapato hayo huku kampuni hizo zikichukua asilimia 80 na asilimia 13 inakwenda kwa Kampuni ya On Mobile.
“Mheshimiwa Mwenyekiti, ukimpigia Waziri Mkuu utasikia muito ya simu wa nyimbo ya Rose Mhando, ukimpigia Malima utasikia wimbo wa Dar mpaka Moro na ukinipigia mimi aidha utasikia nyimbo ya Chadema au kidumu, lakini wasanii hawa hawalipwi ipasavyo,
“Inashangaza Mheshimiwa Mwenyekiti kampuni hii ya Oo Mobile haina leseni ya kufanya kazi hiyo, imejibana kati ya makampuni hayo tu na ina watumishi wawili tu, lakini inachukua fedha nyingi huku wasanii wetu wakibaki masikini, hii haiwezekani", alisema Zitto.
Alisema hakuna sababu ya kuendelea kuwepo kwa kampuni hiyo iliyojibanza kati ya VodaCom na Airtel inayojulikana kwa jina hilo la On Mobile, hivyo iondolewe kwani inafanya biashara bila leseni na kulikosesha taifa mapato.
Mbunge huyo alisema serikali inapaswa kusimama kuwatetea wasanii hao kwani kampuni hizo za simu ni kubwa hivyo ni rahisi kuwakandamiza.
Alisema wakati umefika sasa kwa kampuni hizo, ambazo zinatumia nyimbo za wasanii kama muito katika simu zao ni bora wakamlipa msanii mtunzi asilimia 50 ya mapato yanayotokana na kutumia nyimbo hizo.
Aidha Zitto alipendekeza kutumika kwa Shirika la Posta Tanzania katika kusambaza kazi za wasanii nchini badala ya wasambazaji wa kawaida wa sasa ambao wamekuwa wakiwaibia wasanii.
Mbunge huyo alisema shirika hilo lipo katika maeneo mengi na hasa maeneo ya vijijini na kwa sasa halina kazi nyingi hivyo serikali iliongeze na shirika hilo ili kuokoa kazi za wasanii.

FELLA AFYATUA ALBAMU YA TAARAB

KIONGOZI wa kundi la muziki wa kizazi kipya la TMK Wanaume Family, Saidi Fella amesema yupo katika hatua za mwisho za kukamilisha albamu yake ya muziki wa taarab.
Akizungumza mjini Dar es Salaam wiki hii, Fella alisema tayari amesharekodi nyimbo tano za muziki na yupo katika maandalizi ya kuzindua albamu hiyo.
Fella alisema hadi sasa bado hajaipa jina albamu hiyo na kwamba amerekodi nyimbo zake akiwa na bendi yake ya Mkubwa na Wanawe, aliyoianzisha hivi karibuni.
“Ninachokifanya kwa sasa ni kuandaa maonyesho, ambayo nitaimba nyimbo hizo nikiwa na bendi yangu,”alisema kiongozi huyo na mwasisi wa TMK Wanaume Family.
Fella alisema ameamua kushika kipaza sauti na kuimba kwa lengo la kuongeza ujuzi wake baada ya kufanya vizuri katika muziki wa kizazi kipya.
Mkongwe huyo alisema baada ya uzinduzi wa albamu yake, atakuwa tayari kupanda jukwaa moja na kikundi chochote cha muziki huo kwa lengo la kufanya maonyesho ya pamoja.
“Cha msingi ni kujadili tu mambo ya maslahi, nikiridhika nitaimba,”alisema.
Kwa mujibu wa Fella, katika albamu yake hiyo mpya, amewashirikisha baadhi ya waimbaji nyota wa muziki huo kama vile Hassan Kumbi, Maua Tego, Isha Ramadhani ‘Mashauzi’ na Khadija Omar Kopa.

MR. NICE SASA AGEUKIA TAARAB

BAADA ya ukimya wa muda mrefu, msanii machachari wa muziki wa kizazi kipya nchini, Lucas Nkenda amesema anajiandaa kupakua albamu yake mpya ya miondoko ya mduara.
Nkenda, ambaye ni maarufu zaidi kwa jina la Mr. Nice, alisema mjini Dar es Salaam wiki hii kuwa, albamu yake hiyo itajulikana kwa jina la Tabia gani.
Alisema ameamua kubadili mahadhi ya muziki anaopiga kutokana na maombi ya mashabiki wake wengi, hasa waliopo katika mikoa ya kanda ya Ziwa.
Msanii huyo aliyetamba vilivyo mwanzoni mwa miaka ya 2000 alisema, amefurahishwa na mapokezi makubwa aliyoyapata wakati wa ziara yake katika mikoa hiyo hivi karibuni.
“Sikutegemea kupata mapokezi makubwa kiasi kile. Kusema kweli nimefurahishwa kuona kwamba mashabiki wangu wa ndani na nje ya nchi bado wananikubali sana,”alisema.
Kwa mujibu wa Mr. Nice, anatarajia kuizindua albamu yake hiyo mara baada ya kumalizika kwa mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Katika hatua nyingine, msanii Fred Maliki ‘Mkoloni’ ameibuka na kibao kipya kinachokwenda kwa jina la Nilivyo na Walivyo.
Mkoloni alisema mjini Dar es Salaam wiki hii kuwa, kibao hicho kinaelezea matatizo mbali mbali yanayowakumba wananchi wa Tanzania.
Akifafanua, Mkoloni alisema kibao hicho kinaelezea hali duni za maisha, ambazo kwa kiasi kikubwa zinasababishwa na baadhi ya viongozi wa serikali kuweka mbele zaidi maslahi yao binafsi.

NYOTA WA DUNIA KUCHEZA ZENJI

TIMU ya wachezaji nyota wa zamani wa soka duniani, inajiandaa kufanya ziara visiwani Zanzibar kwa ajili ya mchezo maalumu dhidi ya timu ya Zanzibar, ' Zanzibar Heroes'. Mapato yatakayopatikana katika mchezo huo yatatumika kuendeleza mradi wa kuhifadhi mazingira katika eneo litakaloamuliwa na Serikali ya Zanzibar. Uamuzi wa kukileta kikosi hicho cha wachezaji nyota wa zamani wa dunia, wanaounda taasisi ya Global United, umefikiwa na Kocha Mkuu wa timu ya taifa ya Italia, Cesare Prandeli.
Kocha huyo alifikia uamuzi huo baada ya kufanya ziara katika kijiji cha Jambiani kama mtalii na kutoa zawadi ya seti moja ya jezi kwa timu ya kijiji hicho mapema mwaka huu.
Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Michezo la Zanzibar (BTMZ), Khamis Abdallah Said alisema wiki hii mjini hapa kuwa, nyota hao wa dunia watatua Zenji mapema mwakani.
Abdallah alisema tarehe ya ziara na mechi hiyo itatangazwa baada ya kukamilika kwa taratibu mbali mbali muhimu na kwa kutegemea utaratibu utakaoandaliwa na Prandelli.
Taasisi ya Global United, imepanga kujenga shule ya soka visiwani Zanzibar kwa lengo la kuibua vipaji vya vijana na kuwaendeleza.
Vijana watakaofanya vizuri katika masomo shuleni hapo, watapata nafasi ya kwenda kufanya majaribio ya kucheza soka ya kulipwa nje ya nchi.
Baadhi ya wanasoka nyota wa zamani wa dunia wanaotarajiwa kuwemo kwenye kikosi hicho ni pamoja na Zinedine Zidane, Luis Figo, Mustafa Hadji, Lucas Radebe, Philemon Masinga, Cafu na wengineo. Ziara ya Prandelli, iliratibiwa na Gerd Winkel, ambaye ni mmiliki wa hoteli ya Zanzibar Spice Island Resort iliyoko Jambiani.

CECAFA YAWAPONGEZA WAAMUZI WA TWALIPO

BARAZA la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) limewapongeza waamuzi wa kituo cha Jeshi cha Twalipo kwa umakini wao katika kuchezesha soka.
CECAFA ilitoa pongezi hizo wiki hii kupitia Katibu Mkuu wake, Nicholas Musonye wakati wa mahojiano maalumu na Burudani mjini Dar es Salaam.
Musonye alisema uamuzi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kutoa mafunzo ya uamuzi kwa vijana wa kituo hicho, ambao umri wao ni chini ya miaka 20, unapaswa kuwa mfano wa kuigwa.
Alisema aliwaona vijana hao wakati wa michuano ya Rollingstone iliyofanyika nchini Burundi hivi karibuni na kuvutiwa na uchezeshaji hao.
Waamuzi hao ndio pekee waliochezesha michuano hiyo, kufuatia ombi maalumu la Wizara ya Michezo ya Burundi.
Mbali na michuano hiyo, waamuzi wa kituo hicho pia wamekuwa wakitumika kuchezesha michuano ya Kombe la Uhai na Copa Coca Cola iliyomalizika hivi karibuni mjini Dar es Salaam.
“Nilikuwepo nchini Burundi hivi karibuni kushuhudia mashindano ya Rolling Stone na nilifurahishwa kuona waamuzi watoto kutoka Tanzania ndio waliochezesha mashindano hayo,”alisema.
“Binafsi nawapongeza sana viongozi wa TFF kwa kubuni utaratibu wa kutoa mafunzo ya uamuzi kwa vijana wadogo na ni mfano wa kuigwa wa nchi zingine wanachama wa CECAFA,”aliongeza.
“Nadhani wakati umefika kwa viongozi wa nchi zetu kujitahidi kuboresha viwango vya waamuzi wao na ikiwezekana kuiga mfano wa TFF wa kuwaandaa waamuzi tangu wakiwa vijana kwa lengo la kukuza weledi wao,” alisema Musonye.

MUSONYE: KOMBE LA KAGAME KUREJESHWA JANUARI

Katibu Mkuu wa CECAFA, Nicholas Musonye

Katibu Mkuu wa CECAFA, Nicholas Musonye (kulia) akiwa na rais wa baraza hilo, Leodegar Tenga katika moja ya vikao na waandishi wa habari.


WAKATI michuano ya soka ya Kombe la Kagame ikiwa inaelekea ukingoni, Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) limekiri kuwepo kwa dosari kadhaa katika michuano yake na kwamba tayari limeshaanza kuchukua hatua za kuzirekebisha. Katika makala hii ya ana kwa ana iliyoandikwa na Mwandishi Wetu ATHANAS KAZIGE, Katibu Mkuu wa CECAFA, Nicholas Musonye anaelezea hatua mbali mbali zilizoanza kuchukuliwa na baraza lake.


SWALI: Unaweza kueleza ni kwa nini baraza lako limeamua kuyarejesha tena mashindano ya Kombe la Kagame hapa Tanzania wakati ilikuwa yafanyike Sudan na yalishafanyika hapa mwaka jana ?
JIBU: CECAFA imekubali mashindano hayo yafanyike Tanzania kutokana na machafuko ya kisiasa yaliyotokea Sudan na kusababisha vita vya wenyewe kwa wenyewe na pia kugawanyika kwa nchi hiyo na kuwa nchi mbili.
Awali, viongozi wa Chama cha Soka cha Sudan walitueleza kwamba tayari walishapata wafadhili kwa ajili ya kudhamini mashindano hayo, lakini baada ya hali hiyo kutokea, hatukuwa na la kufanya zaidi ya kuyahamisha.
Tuliamua kuhamishia mashindano haya Tanzania katika kikao cha dharula cha kamati ya utendaji ya CECAFA kwa lengo la kuyanusuru yasifanyike.
Kusema kweli, Tanzania ndio nchi pekee iliyokuwa tayari kuyanusuru mashindano haya. Isingekuwa hivyo, leo hii msingeweza kuyashuhudia. Jambo hilo lilituchanganya sana na kutupa wakati mgumu.
Katika hili, napenda sana kuwapongeza viongozi wa TFF (Shirikisho la Soka Tanzania) kwa kukubali mashindano hayo yafanyike Tanzania na imejitahidi sana kutafuta wafadhili.
TFF ilizungumza na kampuni za Said Salim Bakhressa (Azam), ambayo ndiyo wamiliki wa timu ya Azam na kukubali kudhamini mashindano haya, ambayo yalikuwa hatarini kutofanyika.
Awali, TFF ilifanya mazungumzo na uongozi wa Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL) ili idhamini mashindano haya, lakini ilikataa kutokana na kutingwa na majukumu mengi.
SWALI: Huoni kwamba kuchelewa kuanza ama kufanyika kwa mashindano haya hakuna maana yoyote ?
JIBU: Unajua lengo la mashindano ya Kombe la Kagame ni kuhakikisha timu za ukanda wetu, zinapata mazoezi ya kutosha ili ziweze kushiriki vyema katika mashindano ya klabu za Afrika. Hivyo ni kweli kuchelewa huko kumeziathiri.
Kwa sasa tumeanza kujipanga upya ili kuhakikisha kuwa, mashindano haya yanafanyika mwezi Januari kila mwaka kama ilivyokuwa miaka ya nyuma ili malengo yake yaweze kutimia.
SWALI: Ni jambo gani lililowahi kukukera tangu uliposhika wadhifa wa katibu mkuu wa CECAFA ?
JIBU: Hakuna kitu kinachonikera kama viongozi wa vyama vya soka vya nchi wanachama kushindwa kusimamia na kutekeleza vyema majukumu yao waliyopewa.
Tatizo hili ni kubwa sana kwa nchi wanachama na ni sumu kwa maendeleo ya nchi za ukanda wetu. Lazima nikiri kwamba, baadhi ya viongozi wamekuwa kikwazo kwa maendeleo ya nchi zetu. Wamekuwa wakizitumia nyadhifa zao kujinufaisha badala ya kuendeleza soka.
Kibaya zaidi, wapo baadhi ya viongozi wanashindwa kuandaa timu zao kwa ajili ya michuano ya Kombe la Kagame na Kombe la Chalenji na kusababisha zifanye vibaya na kupunguza hamasa na ushindani.
Binafsi napenda kuona idadi ya timu zinazoshiriki kwenye mashindano yetu ikiongezeka kutoka 12 hadi 16.
SWALI : Ni nchi zipi zilizo wanachama wa CECAFA hadi sasa ?
JIBU : Zipo Tanzania Bara, Zanzibar, Kenya na Uganda, ambazo ndizo waanzilishi. Zingine ni Djibouti, Rwanda, Sudan Kusini, Sudan, Burundi, Ethiopia, Eritrea na Somalia.
SWALI: Unajivunia katika uongozi wako ndani ya CECAFA hadi sasa?
JIBU: Tangu nilipoingia madarakani, nimepata mafanikio mengi ya kujivunia kupitia michuano ya Kombe la Kagame, Kombe la Chalenji na pia baadhi ya wachezaji wetu kupata nafasi ya kwenda kucheza soka ya kulipwa nje ya bara la Afrika kupitia michuano hii.
Baadhi ya wachezaji walionufaika kupitia michuano hii ni pamoja na David Obua, anayecheza ligi ya Scotland katika klabu ya Heart of Midlothian na Dennis Oliech, anayechezea Auxerre ya Ufaransa.
Wengine ni Mbwana Samatta, anayechezea TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo na Emmanuel Okwi, ambaye amekwenda kufanya majaribio ya kucheza mpira wa kulipwa Austria.
Licha ya mafanikio hayo kupitia wachezaji, CECAFA imeweza kupata ufadhili wa Super Sports, ambapo wachezaji wa ukanda huu wanaweza kuonekana ulimwengu mzima.
Hata hivyo, bado tuna changamoto nyingi zinazotukabili katika kuhakikisha ukanda wetu unapata mafanikio makubwa zaidi kisoka.Lakini ili tuweze kufikia malengo hayo, tunahitajika kufanya kazi kwa bidii zaidi na kuwa wabunifu.
Haitakuwa rahisi kwa CECAFA ama nchi zilizo wanachama wake kupata mafanikio kupitia michuano hii pekee. Tunapaswa kuwa wabunifu zaidi katika nchi zetu. Kikubwa ni kuweka kipaumbele katika soka ya vijana.
SWALI : Unaonaje viwango vya waamuzi katika mashindano yanayoandaliwa na baraza lako ?
JIBU: Matatizo ya uamuzi yapo kwa nchi zote wanachama. Lakini binafsi nawapongeza viongozi wa TFF kwa kubuni utaratibu wa kutoa mafunzo ya uamuzi kwa vijana wadogo. Nilikuwepo nchini Burundi hivi karibuni kushuhudia mashindano ya Rolling Stone na nilifurahishwa kuona waamuzi watoto kutoka Tanzania ndio waliochezesha mashindano hayo.
Nadhani wakati umefika kwa viongozi wa nchi zetu kujitahidi kuboresha viwango vya waamuzi wao na ikiwezekana kuiga mfano wa TFF wa kuwaandaa waamuzi tangu wakiwa vijana kwa lengo la kukuza weledi wao.
Mikakati yetu ni kuendelea kuomba msaada kutoka Shirikisho la Soka Afrika (CAF) na Shirikisho la Soka la Dunia (FIFA) kwa ajili ya kupata fedha za kuendesha kozi fupi fupi za kuwafundisha waamuzi wetu.
SWALI: Miaka ya nyuma tulishuhudia matukio mengi ya vurugu wakati wa michuano ya Kombe la Kagame, lakini hivi sasa hali inaonekana kuwa shwari. Nini siri ya mafanikio katika kukomesha matukio hayo ?
JIBU : Namshukuru Mungu kwamba mwaka huu, hadi tulipoingia hatua ya robo fainali, ni mchezaji mmoja tu aliyepewa kadi nyekundu. Hili ni jambo la kujivunia sana. Naona wachezaji wengi wamebadilika na malengo yao ni kucheza soka na kufika mbali.
Kila mchezaji anajitahidi kucheza vizuri ili aweze kuonekana na kupata nafasi ya kwenda kucheza soka ya kulipwa nje. Lakini msimamo wetu ni ule ule kwamba, mchezaji atakayeonyesha utovu wa nidhamu, atachukuliwa hatua kali.
SWALI: Michuano ya mwaka huu ya Kombe la Chalenji itafanyika katika nchi gani?
JIBU: Upo uwezekano mkubwa michuano hiyo ikafanyika Novemba mwaka huu nchini Uganda. Lakini bado mazungumzo yanaendelea kwa ajili ya kupata wafadhili, ingawa tayari tumeshaanza mazungumzo na baadhi ya kampuni, ikiwemo East Africa Breweries.

Breaking News!!! Issa Kihange afariki dunia

KIUNGO wa zamani wa timu ya soka ya Simba, Issa Kihange amefariki dunia.
Kihange alifariki dunia juzi maeneo ya nyumbani kwake, Mbezi Jogoo, Dar es Salaam baada ya kuanguka uwanjani wakati akicheza mechi za maveterani.
Mtandao wa Bin Zubeiry umemkariri kiungo wa zamani wa Yanga, Waziri Mahadhi ‘Mandieta’ aliyekuwapo maeneo ya tukio akisema kuwa, Kihange alinguka wakati akishangilia bao alilofunga.
Kwa mujibu wa Mahadhi, mara baada ya kuanguka, mwanasoka huyo wa zamani alikimbizwa katika hospitali ya IMTU, ambako mauti yalimfika.
Kihange alikuwemo kwenye kikosi cha Simba kilichotwaa taji la pili la michuano ya klabu bingwa Afrika Mashariki na Kati mwaka 1991 mjini Dar es Salaam.

Kipigo ilichokipata Simba chazua tafrani Bungeni

KIPIGO ilichokipata Simba kutoka kwa Azam katika mechi ya michuano ya soka ya Kombe la Kagame, leo kilizua tafrani wakati wa kikao cha Bunge mjini hapa.
Tafrani hiyo ilizuka baada ya baadhi ya wabunge kumwandikia ujumbe mwenyekiti wa kikao cha asubuhi, Jenista Mhagama wakimtaka awafikishie ujumbe wenzao wa Simba watumie bidhaa za Azam ili wapate nguvu.
Jenista alisoma ujumbe huo wakati akitoa matangazo baada ya kumalizika kwa kipindi cha maswali na majibu.
Mara baada ya Jenista kumaliza kusoma ujumbe huo, mbunge wa Tabora Mjini (CCM), Ismail Aden Rage alisimama na kutaka kujibu, lakini hakupewa nafasi hiyo.
Hata hivyo, majibu ya kebehi hiyo yalitolewa na mbunge wa Urambo Magharibi (CCM), Profesa Juma Kapuya, ambaye aliwaelezea Yanga kuwa ni wazoefu wa kupigana uwanjani.
Profesa Kapuya alisema Simba haifanani na Yanga, ambao baada ya kufungwa mabao 3-1 na Azam katika mechi ya ligi, waliamua kufanya fujo uwanjani na kuonyesha ufundi wa kupigana kareti.
Simba ilitolewa na Azam katika michuano ya Kombe la Kagame baada ya kuchapwa mabao 3-1 na Azam. Mechi hiyo ilipigwa juzi kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

TBL yaimwagia Simba mil 20/-

Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geofrey Nyange 'Kaburu' akizungumza jambo wakati wa makabidhiano hayo. Kulia ni Meneja wa Bia ya Kilimanjaro, George Kavishe.

Mkurugenzi wa Sheria na Mahusiano wa TBL, Steven Killindo akimkabidhi mfano wa hundi ya sh. milioni 20, Makamu Mwenyekiti wa Simba SC, Geoffrey Nyange 'Kaburu' leo makao makuu ya TBL, Ilala mjini Dar es Salaam. Wengine ni George Kavishe, Meneja wa Kilimanjaro (kulia) na Katibu Mkuu wa Simba, Evodius Mtawala (kushoto).

Tuesday, July 24, 2012

Simba yatupwa nje Kombe la Kagame, yapigwa 3-1 na Azam

SIMBA leo imetolewa katika michuano ya Kombe la Kagame baada ya kuchapwa mabao 3-1 na Azam katika mechi ya robo fainali iliyopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mshambuliaji John Bocco ndiye aliyeibuka shujaa wa Azam baada ya kuifungia mabao yote matatu, moja kipindi cha kwanza na mengine kipindi cha pili. Bao pekee la Simba lilifungwa na Shomari Kapombe.

Ushindi huo umeiwezesha Azam kutinga nusu fainali, ambapo sasa itakutana na AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo. Vita imefuzu kucheza hatua hiyo baada ya kuitoa Atletico ya Burundi mabao 2-1 katika mechi iliyochezwa kuanzia saa nane mchana.

Mechi nyingine ya nusu fainali itazikutanisha Yanga na APR ya Rwanda. Yanga imetinga hatua hiyo baada ya kuitoa Mafunzo ya Zanzibar kwa penati 5-3 wakati APR iliitoa URA ya Uganda kwa mabao 2-1.

Kwa mujibu wa ratiba, mechi zote mbili za nusu fainali zitachezwa Alhamisi wiki hii. Mechi ya kwanza itazikutanisha Azam na APR wakati katika mechi ya pili, Yanga itavaana na AS Vita.

Fainali ya michuano hiyo inatarajiwa kupigwa Jumapili, ikitanguliwa na mechi ya kutafuta mshindi wa tatu.

Monday, July 23, 2012

WEMA SEPETU ATEMBELEA KITUO CHA YATIMA ARUSHA

WEMA SEPETU AKIWASILI KWENYE KITUO HICHO NA KUPOKEWA NA WENYEJI WAKE

WEMA KWA KUPENDA WATOTO. TAZAMA ALIVYOPENDEZA KWA KUMPAKATA MTOTO HUYU. NAYE AMETULIA TULII, UTADHANI YUPO NA MAMA YAKE. SIJUI KWA NINI HAKUMUASILI MTOTO HUYU


HUYU NDIYE ALIYEWATAMBULISHA WENZAKE KWAMBA WEMA ANAITWA WEMA DIAMOND.

WEMA AKITOA NENO LA SHUKURANI KUTOKANA NA MAPOKEZI MAZURI ALIYOYAPATA.

SNURA NAYE ALIKUWEPO KWENYE SHUGHULI HIYO


DADA PENDO, HUYU NDIYE ALIKUWA MC WA SHUGHULI HIYO


DADA GAUDENCIA, HUYU NDIYE ALIYEANDAA SHUGHULI HIYO NA KUMWALIKA WEMA. HONGERA SANA DADA.

HUYU NDIYE MMILIKI WA KITUO HICHO. HAPA AKITOA NENO LA SHUKURANI KWA WEMA NA WAGENI WENGINE.

WEMA AKIKABIDHI MSAADA WA PESA KWA MMILIKI WA KITUO HICHO.



WEMA AKIZUNGUMZA WAKATI WA SHUGHULI HIYO

NI TUKIO LA HUZUNI, SIELEWI ILIKUWAJE MAANA WEMA ALILIA NA MWENZAKE NAYE AKALIA

HAPA WEMA AKIFUNDISHWA KUCHEZA MUZIKI

HAPA WEMA AKAJIFANYA AMESHAANZA KUFAHAMU KUCHEZA MIONDOKO ALIYOFUNDISHWA

HAPA WEMA ALIVUTIWA SANA NA WATOTO HAWA AKAAMUA KUPIGA NAO PICHA. HABARI ZAO UTAZIPATA BAADA YA SIKU CHACHE ZIJAZO


BONGO MOVIE-WEMA SEPETU AKIWA KATIKA CHARITY EVENT-ARUSHA WIKI ILIYOPITA, ALIWAULIZA WATOTO YEYE NI NANI.. ALL OF THEM WALISEMA WEWE WEMA SEPETU TUNAKUONAGA KATIKA MAGAZETI NA TV. NAJIULIZA HAWA WATOTO WADOGO HIVI HAYO MAGAZETI WANAYAONAJE? NA WAPI... ILA HUYU PICHANI NDO ALIWAACHA WATU MIDOMO WAZI.. ALIWAAMBIA WENZAKE.. MMEKOSEA, HUYU ANAITWA WEMA "DIAMOND". WEMA ALITOA MACHO KAMA KAKABWA NA MFUPA.. ILIBIDI APIGE NAE PICHA. (PICHA, MAELEZO KWA HISANI YA ODAMA 1.BLOGSPOT)