KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, July 25, 2012

MUSONYE: KOMBE LA KAGAME KUREJESHWA JANUARI

Katibu Mkuu wa CECAFA, Nicholas Musonye

Katibu Mkuu wa CECAFA, Nicholas Musonye (kulia) akiwa na rais wa baraza hilo, Leodegar Tenga katika moja ya vikao na waandishi wa habari.


WAKATI michuano ya soka ya Kombe la Kagame ikiwa inaelekea ukingoni, Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) limekiri kuwepo kwa dosari kadhaa katika michuano yake na kwamba tayari limeshaanza kuchukua hatua za kuzirekebisha. Katika makala hii ya ana kwa ana iliyoandikwa na Mwandishi Wetu ATHANAS KAZIGE, Katibu Mkuu wa CECAFA, Nicholas Musonye anaelezea hatua mbali mbali zilizoanza kuchukuliwa na baraza lake.


SWALI: Unaweza kueleza ni kwa nini baraza lako limeamua kuyarejesha tena mashindano ya Kombe la Kagame hapa Tanzania wakati ilikuwa yafanyike Sudan na yalishafanyika hapa mwaka jana ?
JIBU: CECAFA imekubali mashindano hayo yafanyike Tanzania kutokana na machafuko ya kisiasa yaliyotokea Sudan na kusababisha vita vya wenyewe kwa wenyewe na pia kugawanyika kwa nchi hiyo na kuwa nchi mbili.
Awali, viongozi wa Chama cha Soka cha Sudan walitueleza kwamba tayari walishapata wafadhili kwa ajili ya kudhamini mashindano hayo, lakini baada ya hali hiyo kutokea, hatukuwa na la kufanya zaidi ya kuyahamisha.
Tuliamua kuhamishia mashindano haya Tanzania katika kikao cha dharula cha kamati ya utendaji ya CECAFA kwa lengo la kuyanusuru yasifanyike.
Kusema kweli, Tanzania ndio nchi pekee iliyokuwa tayari kuyanusuru mashindano haya. Isingekuwa hivyo, leo hii msingeweza kuyashuhudia. Jambo hilo lilituchanganya sana na kutupa wakati mgumu.
Katika hili, napenda sana kuwapongeza viongozi wa TFF (Shirikisho la Soka Tanzania) kwa kukubali mashindano hayo yafanyike Tanzania na imejitahidi sana kutafuta wafadhili.
TFF ilizungumza na kampuni za Said Salim Bakhressa (Azam), ambayo ndiyo wamiliki wa timu ya Azam na kukubali kudhamini mashindano haya, ambayo yalikuwa hatarini kutofanyika.
Awali, TFF ilifanya mazungumzo na uongozi wa Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL) ili idhamini mashindano haya, lakini ilikataa kutokana na kutingwa na majukumu mengi.
SWALI: Huoni kwamba kuchelewa kuanza ama kufanyika kwa mashindano haya hakuna maana yoyote ?
JIBU: Unajua lengo la mashindano ya Kombe la Kagame ni kuhakikisha timu za ukanda wetu, zinapata mazoezi ya kutosha ili ziweze kushiriki vyema katika mashindano ya klabu za Afrika. Hivyo ni kweli kuchelewa huko kumeziathiri.
Kwa sasa tumeanza kujipanga upya ili kuhakikisha kuwa, mashindano haya yanafanyika mwezi Januari kila mwaka kama ilivyokuwa miaka ya nyuma ili malengo yake yaweze kutimia.
SWALI: Ni jambo gani lililowahi kukukera tangu uliposhika wadhifa wa katibu mkuu wa CECAFA ?
JIBU: Hakuna kitu kinachonikera kama viongozi wa vyama vya soka vya nchi wanachama kushindwa kusimamia na kutekeleza vyema majukumu yao waliyopewa.
Tatizo hili ni kubwa sana kwa nchi wanachama na ni sumu kwa maendeleo ya nchi za ukanda wetu. Lazima nikiri kwamba, baadhi ya viongozi wamekuwa kikwazo kwa maendeleo ya nchi zetu. Wamekuwa wakizitumia nyadhifa zao kujinufaisha badala ya kuendeleza soka.
Kibaya zaidi, wapo baadhi ya viongozi wanashindwa kuandaa timu zao kwa ajili ya michuano ya Kombe la Kagame na Kombe la Chalenji na kusababisha zifanye vibaya na kupunguza hamasa na ushindani.
Binafsi napenda kuona idadi ya timu zinazoshiriki kwenye mashindano yetu ikiongezeka kutoka 12 hadi 16.
SWALI : Ni nchi zipi zilizo wanachama wa CECAFA hadi sasa ?
JIBU : Zipo Tanzania Bara, Zanzibar, Kenya na Uganda, ambazo ndizo waanzilishi. Zingine ni Djibouti, Rwanda, Sudan Kusini, Sudan, Burundi, Ethiopia, Eritrea na Somalia.
SWALI: Unajivunia katika uongozi wako ndani ya CECAFA hadi sasa?
JIBU: Tangu nilipoingia madarakani, nimepata mafanikio mengi ya kujivunia kupitia michuano ya Kombe la Kagame, Kombe la Chalenji na pia baadhi ya wachezaji wetu kupata nafasi ya kwenda kucheza soka ya kulipwa nje ya bara la Afrika kupitia michuano hii.
Baadhi ya wachezaji walionufaika kupitia michuano hii ni pamoja na David Obua, anayecheza ligi ya Scotland katika klabu ya Heart of Midlothian na Dennis Oliech, anayechezea Auxerre ya Ufaransa.
Wengine ni Mbwana Samatta, anayechezea TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo na Emmanuel Okwi, ambaye amekwenda kufanya majaribio ya kucheza mpira wa kulipwa Austria.
Licha ya mafanikio hayo kupitia wachezaji, CECAFA imeweza kupata ufadhili wa Super Sports, ambapo wachezaji wa ukanda huu wanaweza kuonekana ulimwengu mzima.
Hata hivyo, bado tuna changamoto nyingi zinazotukabili katika kuhakikisha ukanda wetu unapata mafanikio makubwa zaidi kisoka.Lakini ili tuweze kufikia malengo hayo, tunahitajika kufanya kazi kwa bidii zaidi na kuwa wabunifu.
Haitakuwa rahisi kwa CECAFA ama nchi zilizo wanachama wake kupata mafanikio kupitia michuano hii pekee. Tunapaswa kuwa wabunifu zaidi katika nchi zetu. Kikubwa ni kuweka kipaumbele katika soka ya vijana.
SWALI : Unaonaje viwango vya waamuzi katika mashindano yanayoandaliwa na baraza lako ?
JIBU: Matatizo ya uamuzi yapo kwa nchi zote wanachama. Lakini binafsi nawapongeza viongozi wa TFF kwa kubuni utaratibu wa kutoa mafunzo ya uamuzi kwa vijana wadogo. Nilikuwepo nchini Burundi hivi karibuni kushuhudia mashindano ya Rolling Stone na nilifurahishwa kuona waamuzi watoto kutoka Tanzania ndio waliochezesha mashindano hayo.
Nadhani wakati umefika kwa viongozi wa nchi zetu kujitahidi kuboresha viwango vya waamuzi wao na ikiwezekana kuiga mfano wa TFF wa kuwaandaa waamuzi tangu wakiwa vijana kwa lengo la kukuza weledi wao.
Mikakati yetu ni kuendelea kuomba msaada kutoka Shirikisho la Soka Afrika (CAF) na Shirikisho la Soka la Dunia (FIFA) kwa ajili ya kupata fedha za kuendesha kozi fupi fupi za kuwafundisha waamuzi wetu.
SWALI: Miaka ya nyuma tulishuhudia matukio mengi ya vurugu wakati wa michuano ya Kombe la Kagame, lakini hivi sasa hali inaonekana kuwa shwari. Nini siri ya mafanikio katika kukomesha matukio hayo ?
JIBU : Namshukuru Mungu kwamba mwaka huu, hadi tulipoingia hatua ya robo fainali, ni mchezaji mmoja tu aliyepewa kadi nyekundu. Hili ni jambo la kujivunia sana. Naona wachezaji wengi wamebadilika na malengo yao ni kucheza soka na kufika mbali.
Kila mchezaji anajitahidi kucheza vizuri ili aweze kuonekana na kupata nafasi ya kwenda kucheza soka ya kulipwa nje. Lakini msimamo wetu ni ule ule kwamba, mchezaji atakayeonyesha utovu wa nidhamu, atachukuliwa hatua kali.
SWALI: Michuano ya mwaka huu ya Kombe la Chalenji itafanyika katika nchi gani?
JIBU: Upo uwezekano mkubwa michuano hiyo ikafanyika Novemba mwaka huu nchini Uganda. Lakini bado mazungumzo yanaendelea kwa ajili ya kupata wafadhili, ingawa tayari tumeshaanza mazungumzo na baadhi ya kampuni, ikiwemo East Africa Breweries.

No comments:

Post a Comment