KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, July 25, 2012

YANGA, APR KIAMA LEO

Mshambuliaji Olivier Karekezi wa APR ya Rwanda

Kiungo Haruna Niyonzima wa Yanga. Zamani alikuwa mchezaji wa APR


MABINGWA watetezi wa michuano ya soka ya Kombe la Kagame, Yanga leo wanashuka dimbani kumenyana na APR ya Rwanda katika mechi ya nusu fainali itakayopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Pambano hilo litatanguliwa na mechi nyingine ya nusu fainali kati ya Azam na AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo litakalopigwa kuanzia saa nane mchana.
Mechi zote mbili zinatarajiwa kuwa na upinzani mkali kwa vile timu zitakazoshinda si tu kwamba zitafuzu kucheza fainali, bali pia zitajihakikishia zawadi ya dola 50,000 za Marekani zitazotolewa kwa mshindi wa kwanza na wa pili.
Bingwa wa michuano hiyo atazawadiwa dola 30,000, wa pili dola 20,000 na wa tatu dola 10,000. Fedha hizo zimetolewa na Rais Paul Kagame wa Rwanda.
Yanga imetinga nusu fainali baada ya kuitoa Mafunzo ya Zanzibar kwa penalti 5-3 baada ya timu hizo kumaliza dakika 90 zikiwa sare ya bao 1-1. Nayo APR ilitinga hatua hiyo baada ya kuitoa URA ya Uganda kwa mabao 2-1.
Akizungumzia mechi hiyo juzi, Kocha Mkuu wa Yanga, Tom Saintfiet alikiri kwamba itakuwa ngumu kwa vile wapinzani wao hawawezi kukubali kufungwa mara mbili.
Yanga iliichapa APR mabao 2-0 katika mechi ya mwisho ya hatua ya makundi, kipigo ambacho kilipokelewa kwa furaha kubwa na mashabiki wa klabu hiyo.
“Ni vigumu kwa timu kukubali kufungwa mara mbili na timu moja katika michuano ile ile. Binafsi nilikuwa naomba dua APR ifungwe na URA ili tusikutane nayo tena,”alisema.
Washambuliaji Hamizi Kiiza, Saidi Bahanuzi na beki Nadir Haroub ‘Cannavaro’ walionyesha wasiwasi wao kuhusu mechi hiyo, lakini waliapa kupambana kufa na kupona ili waweze kushinda na kufuzu kucheza fainali.
“Mechi itakuwa ngumu kwa sababu wapinzani wetu lazima watacheza kwa nguvu zao zote, lakini nasi tumejiandaa vizuri,”alisema Bahanuzi.
Kwa upande wake, Cannavaro alisema hawatakuwa tayari kupoteza mechi hiyo kwa vile wakifungwa, watakuwa wamewaangusha mashabiki wao, ambao wamekuwa wakiwaunga mkono kwa nguvu zote.
Katika kuhakikisha timu yao inaibuka na ushindi, kamati ya utendaji ya Yanga jana iliitisha kikao cha dharula kwa ajili ya kuweka mikakati ya kushinda mechi hiyo.
Moja ya maamuzi yaliyofikiwa katika kikao hicho ni kukutana na wachezaji leo asubuhi na kuahidi kuwapa zawadi kubwa iwapo watashinda mechi hiyo na kusonga mbele.
Kocha Mkuu wa APR, Ernest Brandy alikiri kwamba Yanga ni timu nzuri, lakini aliahidi kuwepo kwa mabadiliko makubwa katika mchezo wa leo.
Kocha huyo alisema hawakucheza kwa nguvu katika mechi ya awali kwa sababu walishakuwa na uhakika wa kusonga mbele, lakini safari hii hawatakuwa na mzaha.
Nahodha wa timu hiyo, Olivier Karekezi alisema kazi yake leo itakuwa ni moja tu, kumdhibiti kiungo wa Yanga, Haruna Niyonzima, ambaye alisema anamfahamu vyema.
Karekezi alisema amecheza pamoja na Niyonzima alipokuwa APR na waliwahi kwenda kufanya majaribio ya kucheza soka ya kulipwa pamoja katika nchi za Ufaransa na Sweden, hivyo anafahamu vyema jinsi ya kumdhibiti.
Wakati huo huo, Kocha Mkuu wa Azam, Stewart Hall amekiri kuwa pambano lao la leo dhidi ya AS Vita litakuwa gumu na lenye ushindani mkali.
Stewart alisema jana kuwa, ugumu wa pambano hilo unatokana na ukweli kwamba kikosi cha AS Vita kinaundwa na wachezaji wengi wazuri na wenye uzoefu wa michuano ya kimataifa.
Hata hivyo, kocha huyo kutoka Uingereza alisema, wamejipanga vyema kuhakikisha wanashinda mechi hiyo na kutinga hatua ya fainali.
Taarifa iliyotolewa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) jana ilieleza kuwa, viingilio katika mechi hiyo vitakuwa sh. 5,000, sh. 7,000, sh. 15,000 na sh. 20,000.

No comments:

Post a Comment