KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, July 12, 2012

Kalala Junior kutegua kitendawili mwezi ujao

MWIMBAJI nyota wa nyimbo za muziki wa dansi nchini, Kalala Junior amesema atategua kitendawili cha bendi ipi atajiunga nayo katikati ya mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan.
Kalala alisema mjini Dar es Salaam wiki hii kuwa, kwa sasa ameamua kujipumzisha na masuala ya muziki kutokana na kuchoshwa na kazi hiyo.
Mwanamuziki huyo alielezea msimamo wake huo alipotakiwa kujibu swali kuhusu bendi ipi anayotarajia kujiunga nayo baada ya kujiengua Mapacha Watatu.
Kalala alitangaza kujitoa Mapacha Watatu wiki kadhaa zilizopita bila kuweka wazi kuhusu mipango yake ya baadaye, lakini kulikuwa na uvumi kwamba anataka kujiunga na bendi ya Mashujaa.
Akizungumzia tetesi hizo, Kalala ambaye ni mtoto wa mwanamuziki mkongwe nchini, Hamza Kalala alisema, hadi sasa bado hajaamua kujiunga na bendi yoyote.
“Nimeamua kupumzika kwa miezi miwili. Lakini ifikapo katikati ya mwezi wa Ramadhan nitaweka wazi kuhusu bendi ipi nitakayojiunga nayo,”alisema.
Alisema kama binadamu, amefanyakazi ya kuimba kwa muda mrefu na kukesha kwenye kumbi za burudani kwa saa nyingi, hivyo anahitaji kupumzika.
Hata hivyo, Kalala alikiri kuwa amekuwa akifuatwa na bendi nyingi zikimtaka ajiunge nazo, lakini bado anatafakari kuhusu ipi itakayomfaa zaidi.
“Ni kweli hadi sasa wamekuja wanaume wanne kunifuata, hivyo napaswa kumchagua mmoja,”alisema.
Alipobanwa kuhusu tetezi kwamba amepanga kujiunga na Mashujaa, Kalala hakuwa tayari kukubali au kukataa. Alisema wakati utakapofika, atalazimika kuweka wazi kila kitu.

No comments:

Post a Comment