KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Friday, July 27, 2012

JOSE CHAMELEONE AVAMIA UBALOZI WA TANZANIA NCHINI UGANDA, ASHINIKIZA AREJESHEWE PASIPOTI YAKE

Chameleone akiteta jambo na mmoja kati ya wafuasi wake nje ya ofisi za ubalozi wa Tanzania nchini Uganda.

Chameleone akipiga gita huku wafuasi wake wakiwa wamebeba mabango nje ya ofisi za ubalozi wa Tanzania nchini Uganda.

Polisi wa Uganda wakimtuliza Chameleone na wafuasi wake wakati walipofanya maandamano ya amani nje ya ofisi za ubalozi wa Tanzania nchini Uganda.

Ofisa mmoja wa polisi akizungumza na wafuasi wa Chameleone nje ya ofisi za ubalozi wa Tanzania nchini Uganda.


Mwanamuziki Jose Chameleone na wafuasi wake jana asubuhi walivamia kwenye ofisi za ubalozi wa Tanzania nchini Uganda na kushinikiza arejeshewe pasi yake ya kusafiria.


Jose, mmoja wa wanamuziki tajiri katika nchi za ukanda wa Afrika, aliendesha gari lake aina ya Range Rover Sport na kuliegesha karibu na ubalozi huo.


Mwanamuziki huyo pamoja na wafuasi wake walikuwa na mabango yaliyokuwa na maandishi yanayomtaka mfanyabiashara Eric Shigongo arejeshe hati yake ya kusafiria.


Jose aliweka kambi kwa muda nje ya ubalozi huo na kupiga gita lake huku akiimba nyimbo mbali mbali. Wafuasi wake walikuwa wamebeba mabango ya kupinga kitendo cha Shigongo kumnyang'anya hati yake ya kusafiria.


Baadhi ya mabango yalisomeka: 'Shigongo upo juu ya sheria?' , 'Tafadhali Tanzania nisaidieni', 'Nahitaji nirejeshewe hati yangu ya kusafiria'.


Shigongo ndiye aliyemwalika Jose kufanya onyesho wakati wa tamasha la matumaini lililofanyika hivi karibuni kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.


Jose alifanya onyesho wakati wa tamasha hilo, lakini inasemekana kuwa Shigongo alikataa kumlipa pesa zake kwa madai kuwa, tayari alishamlipa meneja wa mwanamuziki huyo, aliyejulikana kwa jina la George.


Imeelezwa kuwa, Shigongo alimlipa George dola 3,500 za Marekani kwa ajili ya Jose kufanya onyesho hilo, lakini mwanamuziki huyo alikana kumtambua meneja huyo.


Jose alifanikiwa kuondoka nchini baada ya kupewa hati ya muda ya kusafiria katika ofisi za ubalozi wa Uganda hapa nchini.


Uamuzi wa Jose kuvamia ubalozi wa Tanzania nchini Uganda, ulifanyika saa chache baada ya kutoka kufanya onyesho kwenye Uwanja wa Amahoro mjini Kigali, Rwanda.


Maofisa kadhaa wa polisi wa Uganda walifika kwenye ofisi za ubalozi huo wakiwa na gari yenye namba UP-2627 kwa ajili ya kulinda usalama.


Hata hivyo, Jose aliwaeleza polisi hao kuwa, yeye na wenzake waliamua kufanya maandamano ya amani kwa lengo la kushinikiza arejeshewe hati yake ya kusafiria.


Baadaye, nyota huyo wa muziki alikutana na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Uganda, ambaye alimuahidi kwamba atalifanyia kazi suala lake kwa kuwasiliana na Mkuu wa Jeshi la Polisi la Tanzania, Inspekta Saidi Mwema.

No comments:

Post a Comment