KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Monday, July 9, 2012

Wanasoka wawili wafariki katika ajali ya trekta Tabora

Na El - hadji Yuusuf, Sikonge.
Wachezaji wawili wa timu ya soka ya vijana ya TUPA ya kijiji cha Ipole wilayani Sikonge, wamefariki dunia baada ya trekta walilokuwa wakisafiria kupata ajali na kupinduka.
Kwa mujibu wa mratibu wa timu hiyo Anna Bagozi, wachezaji hao waliofariki wametajwa kwa majina ya Edson Brighton na Issa Nassoro ambao walifariki dunia mmoja akiwa papo hapo na mwingine alipokuwa hospitalini akipatiwa matibabu.
Amesema kuwa watu wengine 30 waliokuwa pamoja na wanamichezo hao walinusurika katika ajali hiyo huku wengine kumi wakipata majeraha.
Alisema kuwa kutokana na tatizo la ukosefu wa usafiri katika vijiji vya wilaya ya Sikonge, wanamichezo hao walilazimika kukodi Trekta kwa ajili ya kwenda kijiji cha Mibono ambacho kipo umbali wa zaidi ya kilomita 80 kutoka kijiji hicho.
Bagozi, alisema walipokuwa njiani ghafra tela lilikatika na hivyo kusababisha ajali hiyo, kwani liliacha njia na kupinduka hivyo kusababisha kifo cha Edson Papo hapo na Nassoro alipokuwa hospitalini.
Alisema ajali hiyo ilitokea saa kumi jioni katika eneo ambalo ambalo hata hivyo hakuweza kulitambua na kwamba ajali hiyo imewafadhaisha sana na kuwasikitisha.
Mganga mfawidhi wa hospitali ya wilaya ya Sikonge, Issaya Magana, amesema kuwa wamepokea majeruhi kumi wa ajali hiyo ambapo majeruhi sita wametibiwa na kuondoka na wamejeruhi wanne bado wanaendelea kupatiwa matibabu baada ya kulazwa na hali zao ni mbaya.
Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Tabora, ACP Antony Rutta, amethibitisha kutoa kwa ajali hiyo na kueleza kuwa polisi wanaendelea na uchunguzi.

No comments:

Post a Comment