KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Tuesday, July 10, 2012

SIMBA, AZAM ZAGOMA KUCHEZA AMAAN, FAINALI YAHAMISHIWA DAR

MECHI ya fainali ya michuano ya soka ya Kombe la Urafiki kati ya Simba na Azam imehamishwa kutoka Uwanja wa Amaan, Zanzibar kwenda Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mechi hiyo, ambayo awali ilikuwa ichezwe kesho kwenye Uwanja wa Amaan, sasa itachezwa Alhamisi kwenye Uwanja wa Taifa.

Katibu wa kamati ya maandalizi ya michuano hiyo, Suleiman Jabir aliwaambia waandishi wa habari mjini Dar es Salaam leo kuwa, uamuzi huo umefikiwa kutokana na timu hizo mbili kugoma kucheza uwanja wa Amaan.

Jabir amewaomba radhi mashabiki wa soka wa Zanzibar kutokana na fainali hiyo kuhamishiwa Dar kwa madai kuwa, jambo hilo lipo nje ya uwezo wao.

Awali, Simba na Azam ziligoma kucheza fainali hiyo kwenye Uwanja wa Amaan kwa madai kuwa ni mbovu na umesababisha kuumia kwa baadhi ya wachezaji wao.

Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geofrey Nyange 'Kaburu' aliwaambia waandishi wa habari kuwa, eneo la kuchezea soka kwenye uwanja huo ni bovu.

Kaburu alisema wapo tayari kucheza fainali hiyo kwenye uwanja wowote, lakini si Uwanja wa Amaani.

Alisema waliwasilisha malalamiko hayo kwa waandaaji kwa muda mrefu, lakini hawakuweza kuyafanyia kazi.

Kaburu alisema kutokana na timu yake kushiriki kwenye michuano ya Kombe la Kagame, wana hofu wachezaji wao wanaweza kuumia zaidi kwenye mechi hiyo.

Aliwataja wachezaji wa Simba walioumia tangu kuanza kwa michuano hiyo kuwa ni Lino Masimbo, Salim Kinje na Mussa Mudde.

Meneja wa Azam, Patrick Setter alisema klabu yake inawapenda na kuwaheshimu mashabiki wa Zanzibar, lakini kutokana na hali ya uwanja wa Amaan, hawawezi kucheza mechi ya fainali visiwani humo.

“Tupo tayari hata kwenda kucheza Pemba ama kwingine kokote, lakini sio hapa Amaan. Hofu yetu ni wachezaji wetu wengi zaidi kuumia,"alisema.

Kwa mujibu wa Patrick, wachezaji wa Azam walioumia tangu kuanza kwa michuano hiyo ni Michael Kipre, Jabir Azizi na Kipre Tchetche.

Alisema hawagomi kucheza mechi hiyo Uwanja wa Amaan kwa sababu ya maslahi, bali wanajali zaidi afya za wachezaji wao.

Rais wa ZFA, Amani Makungu alisema wapo tayari kupokea lawama kutoka kwa wapenzi wa soka wa Zanzibar, lakini hawana la kufanya.

Alisema walikuwa wakifikiria kuihamishia mechi hiyo Uwanja wa Gombani, Pemba lakini wameshindwa kutokana na gharama kubwa kwa vile viongozi wa Simba na Azam wametaka kusafirishwa kwa ndege.

Simba na Azam zilifuzu kucheza fainali jana baada ya kuibuka na ushindi dhidi ya Falcon na All Stars.

No comments:

Post a Comment