KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, July 12, 2012

JAMBELE: LAZIMA YANGA IJITEGEMEE

WAKATI homa ya uchaguzi mdogo wa klabu ya Yanga ikiwa inazidi kupamba moto, mgombea wa nafasi ya mwenyekiti, John Jambeleamesema sera yake kubwa ni kutaka klabu hiyo ijitegemee.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi mjini Dar es Salaam jana, Jambele alisema Yanga haipaswi kuendeshwa kwa kutumia fedha za mifukoni mwa watu binafsi.

Jambele alisema iwapo Yanga itaendelea kuongozwa kwa utaratibu huo, watu hao wanapoondoka ni rahisi kwa klabu kuyumba kiuchumi.

Mgombea huyo alisema kwa hadhi ya Yanga, ni aibu mishahara ya wachezaji, benchi la ufundi na maofisa wengine wa klabu kulipwa na mtu binafsi, ambaye akijitoa, anawaacha kwenye wakati mgumu.

Ili kufikisha ujumbe wake kwa wanachama wengi zaidi wa Yanga, Jambele alisema ameitisha mkutano na waandishi wa habari utakaofanyika leo kwenye ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO), Dar es Salaam.

Alisema katika mkutano huo unaotarajiwa kuanza saa tano asubuhi, anatarajia kumwaga sera na mikakati ya kuikwamua klabu hiyo.

"Nilianza kampeni katika Manispaa ya Temeke, ikafuata Kinondoni na nitamaliza Ilala, lakini Yanga haipo Dar es Salaam peke yake ina wapenzi Tanzania nzima na nitafikisha ujumbe wangu kwao kupitia mkutano huo," alisema Jambele.

Wakati huo huo Justin Baruti anayegombea ujumbe wa kamati ya utendaji ya Yanga, amesema amejitosa kwenye kinyang'anyiro hicho kwa nia ya kuisaidia klabu hiyo ijitegemee kwa kuwa ina mtaji wa kutosha wa wanachama wanaoweza kuisaidia.

Baruti alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, iwapo atashinda nafasi hiyo, atawashawishi viongozi wenzake kuanzisha chuami (saccos) za wanachama katika manispaa tatu za Dar es Salaam na mpango huo ukipata mafanikio, utakuwa wa nchi nzima.

Justin, ambaye ni mtoto wa mweka hazina na katibu mkuu wa zamani wa Yanga, Steven Baruti, alisema kuwa matatizo mengine atakayoshughulikia kuyatatua ni kujenga uwanja wa kisasa wa Kaunda ili utumike kwa mechi za ligi kuu.

"Kupitia uwanja huu tutavuna fedha za viingilio na timu haitapata tabu sehemu ya kufanyia mazoezi," alisisitiza mgombea huyo, ambaye amedai kusikitishwa na matokeo mabaya iliyopata timu ya Yanga msimu uliopita.

Alisema kuwa uwanja huo unaweza kujengwa kwa fedha za mkopo benki na nguvu za wanachama, ambao atawashawishi wakate kadi ili wafike 200,000 kwa kuwa 12,000 waliopo sasa hawatoshi.

Justin alisema wakiongezeka hadi kufika idadi hiyo, hata wakichangishwa sh 10,000 kila mmoja pesa zitakazopatikana zinatosha kuboresha uwanja wa Kaunda.

Mgombea huyo, ambaye ni mwanachama wa Yanga kutoka tawi la Ubungo Terminal ambalo maarufu kwa jina la ukiona manyoya ujue kaliwa, amewasihi wanachama wenzake wachague wagombea makini wenye uwezo wa kuongoza na kuleta umoja.

Baruti ni meneja uendeshaji katika Kampuni ya CMACGM/DELMAS yenye ofisi zake kwenye Bandari ya Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment