KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, July 18, 2012

SIMBA YAZINDUKA, YAIBAMIZA PORTS 3-0

SIMBA leo imefufua matumaini ya kufuzu kucheza robo fainali ya michuano ya soka ya Kombe la Kagame baada ya kuichapa Ports ya Djibouti mabao 3-0 katika mechi ya kundi A iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mshambuliaji Abdalla Juma ndiye aliyeibeba Simba baada ya kuifungia mabao mawili kati ya matatu, yote yakiwa yamepatikana katika dakika 30 za mwisho za pambano hilo.
Kwa matokeo hayo, Simba bado inashika nafasi ya tatu katika kundi hilo, ikiwa na pointi tatu baada ya kucheza mechi mbili, sawa na Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, lakini zinatofautiana kwa idadi ya mabao ya kufunga na kufungwa.
URA imekuwa ya kwanza kutinga robo fainali kutoka kundi hilo baada ya jana kuichapa Vita mabao 3-1 na kufikisha pointi sita katika mechi mbili ilizocheza.
Simba ilihesabu bao la kwanza dakika ya 60 lililofungwa na Abdalla, aliyeingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Haruna Shamte. Alifunga bao hilo baada ya kutengenezewa pasi safi na Mwinyi Kazimoto, aliyewatoka mabeki wawili wa Ports.
Felix Sunzu, ambaye alipoteza nafasi nyingi za kufunga mabao kipindi cha kwanza, aliifungia Simba bao la pili dakika ya 64 kwa njia ya penalti baada ya beki Jean Paul wa Ports kuunawa mpira ndani ya eneo la hatari wakati akijaribu kukwepa kuvikwa kanzu na Kazimoto.
Abdalla aliiongezea Simba bao la tatu dakika ya 74 baada ya kutanguliziwa krosi ndefu na Shomari Kapombe, akafumua shuti kali lililotinga moja kwa moja wavuni.
Ports ilikuwa ya kwanza kufanya shambulizi kwenye lango la Simba dakika ya pili wakati Roland Ayuk Agbor alipomtoka beki Amir Maftah na kupiga shuti kali, lakini lilitoka juu ya lango.
Dakika nane baadaye, Omar Mohamed Ahmed alikosa bao baada ya kupewa pasi na Loland, ambapo shuti lake lilipaa juu ya lango.
Katika dakika 15 za kwanza, timu zote mbili zilishambuliana kwa zamu na kucheza zaidi katikati ya uwanja, lakini tatizo kubwa lilikuwa umaliziaji mbovu.
Simba ilipata nafasi mbili nzuri za kufunga mabao dakika ya 20 na 25, lakini kikwazo kikubwa kilikuwa kipa Kalid Ali Moursal wa Ports aliyeokoa mashuti ya Sunzu na Mwinyi Kazimoto.
Kiungo Kanu Mbiyavanga alifanya kazi nzuri dakika ya 30 baada ya kuingia ndani ya 18 na kutoa pasi kwa Felix Sunzu, lakini shuti lake liliokolewa na kipa Kalid wa Ports.
Sunzu alipoteza nafasi nyingine nzuri dakika ya 36 baada ya kutanguliziwa mpira na Mussa Mudde, ambapo shuti lake lilipaa juu ya lango. Timu hizo zilikwenda mapumziko zikiwa suluhu.
Simba ilibadili staili ya mchezo katika kipindi cha pili na kupata nafasi kadhaa za kufunga mabao na iwapo Sunzu angekuwa makini, ingeweza kupata idadi kubwa ya mabao.
Nafasi nyingine nzuri ilipotezwa na Abdalla dakika ya 68 alipotanguliziwa mpira na kipa Juma Kaseja, akamtoka beki mmoja wa Ports na kubaki ana kwa ana na kipa Kalid aliyetoka golini, lakini shuti lake lilitoka nje.
SIMBA: Juma Kaseja, Shamte Ali, Amir Maftah, Shomari Kapombe, Lino Masimbo, Amri Kiemba/ Juma Nyoso, Haruna Moshi/ Uhuru Selemani, Mussa Mudde, Felix Sunzu, Mwinyi Kazimoto, Kanu Mbiyavanga.
PORTS: Kalid Ali Moursal, Kadar Abbas Abanel, Mohamed Omar Arab, Abdourama Isman, Jean Paul Niyobabariba, Mahdi Ahmed Moumin, Vincent Taboko Agbor, Omar Mohamed Ahmed, Daher Hassan Ali, Roland Ayuk Agbor na asama Jean Bosco.
Wakati huo huo, URA imekuwa timu ya kwanza kutoka kundi A kufuzu kucheza robo fainali baada ya kuichapa AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo mabao 3-1 katika mechi ya kwanza iliyochezwa kuanzia saa nane mchana.
Mabao ya URA yaliwekwa kimiani na Sula Bagala, aliyefunga mawili na Robert Ssentongo. Bao la kufutia machozi la Vita lilifungwa na Mutombo Kazadi.

No comments:

Post a Comment