KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Tuesday, October 18, 2011

MAKONGORO: Viongozi waache tamaa ya utajiri

Makongoro Nyerere (kushoto) akizungumza na mmiliki wa blogu hii, Rashid Zahor ofisini kwake Musoma mkoani Mara



UNAPOTAJA majina ya watoto wa Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, jina linaloweza kutambulika kirahisi zaidi kutokana na umaarufu wake ni la Makongoro Nyerere.
Umaarufu wa Makongoro unatokana na mambo mengi, lakini yaliyo makubwa ni kujihusisha kwake na masuala ya siasa na pia kupenda kujichanganya na watu mbalimbali kwa ajili ya kubadilishana mawazo na kupata kinywaji kidogo.
Makongoro, ambaye ni mtoto wa tano wa Baba wa Taifa, aliwahi kuwa mbunge wa Arusha Mjini kwa tiketi ya NCCR-Mageuzi mwaka 1995 na aliwahi kumtembelea baba yake Butiama akiwa na viongozi wenzake wa chama hicho.
Hata hivyo, Makongoro hakuweza kudumu kwenye ubunge kwa muda mrefu. Aliondolewa kwenye nafasi hiyo kwa uamuzi wa mahakama, kufuatia kesi iliyofunguliwa ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa jimbo hilo.
Miaka michache baadaye, Makongoro alirejea CCM na miaka ya hivi karibuni, alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa chama mkoa wa Mara, wadhifa anaoendelea kuushikilia hadi sasa.
Makongoro ni mwanasiasa mzuri. Licha ya kuijua vyema historia ya TANU, CCM, mapambano ya kugombea uhuru wa Tanganyika na siasa za vyama vingi, ni mtu mwenye ushawishi na uelewa mkubwa juu ya mambo mbalimbali.
Hayo yalijidhihirisha wakati nilipobahatika kuzungumza na mwanasiasa huyu kwenye ofisi za CCM mkoa wa Mara baada ya kumkosa nyumbani kwake kijiji cha Butiama kilichopo wilaya ya Musoma Mjini.
Katika mazungumzo hayo, ambayo yalilenga maadhimisho ya miaka 12 tangu kufariki kwa Baba wa Taifa na miaka 50 ya uhuru wa Tanganyika, Makongoro alisema njia pekee nzuri ya kumuenzi Mwalimu Nyerere ni kudumisha umoja na mshikamano miongoni mwa watanzania.
Makongoro alisema Mwalimu Nyerere na wazee wenzake, akiwemo hayati Abeid Amaan Karume, kwa makusudi walifanya juhudi za kisayansi kuwaunganisha watanzania kuwa wamoja baada ya kugundua kwamba, wakoloni waliokuwa wakiwatawala, hawakuwa wengi na walitumia mbinu kuwagawa.
“Walichofanya ni kuchukua hatua mbalimbali kuleta umoja kabla ya uhuru na miaka 10 baada ya uhuru. Umoja huu bado upo, lakini unaweza kuyumba kutokana na maongozi ya kisiasa ya vyama vingi, halafu tukawaambukiza wananchi,”alisema.
Mwanasiasa huyo machachari alisema, watanzania bado wana umoja, lakini vyama vya siasa vinaweza vikaanzisha makundi ndani ya vyama vyenyewe na kisha makundi hayo kuhamia kwa wananchi.
“Hivyo kwangu mimi, njia pekee nzuri kwa wananchi kumuenzi Baba wa Taifa na viongozi wenzake wa wakati huo ni kudumisha amani na umoja, vilivyodumu wakati wao hadi walipotuachia uongozi,”alisema.
Akizungumzia uwepo wa vyama vingi vya siasa nchini, Makongoro alisema bado unakwenda kama ulivyoachwa na Mwalimu Nyerere, isipokuwa zipo dosari chache, lakini haziwezi kutishia amani iliyopo nchini.
Alisema uhuru ni jambo jema, lakini uhuru usio na nidhamu ni haramu. Alisema iwapo inatokea watu wanakwenda kufanya vurugu mahali kwa mtu, ambaye ni mwanasiasa ama si mwanasiasa, huo ni uhuni na inatakiwa waadhibiwe.
Alisema matukio ya aina hiyo yanaweza kutokea nchi yoyote,wakati wowote na kufanywa na mtu yeyote, lakini hayamaanishi kwamba amani inatoweka. Alisisitiza kuwa, amani bado ipo nchini.
Alitoa mfano wa uchaguzi mdogo wa jimbo la Tarime, kufuatia kifo cha mbunge wake, Chacha Wangwe, ambapo baadhi ya wananchi walikatwa mapanga na mbunge mmoja kupiga risasi hewani ili kujitetea.
Mfano mwingine uliotolewa na Makongoro ni ule wa wafuasi wa CHADEMA kumvisha mbwa fulana yenye nembo ya CCM na watu kumkatakata mapanga.
“Huyu ni mnyama masikini, hajui lolote na kwa mazingira ya Tarime yalivyo, pengine aliona wamemsitiri kwa baridi, kumbe kuna watu wengine wamekerwa na kitendo kile,”alisema.
“Vyama vina matatizo. Palipo na haki pana wajibu. Huwezi kutaka haki ya kuwa huru, lakini hutaki kuwajibika na kuwa na nidhamu. Uhuru wako utakuwa mchezo wa kuigiza,”aliongeza.
Makongoro alisema, kutokana na tukio hilo, CCM ingeweza kulalamika kwa tume ya taifa nay eye alikuwa mwenyekiti, lakini hakupelekewa malalamiko hayo zaidi ya kupewa taarifa ya tukio na kuelezwa kwamba mbwa huyo ameshashughulikiwa.
“Unaweza kuita ni uvunjifu wa amani, lakini hapana, huu ni ushabiki uliovuka mpaka. Wangeweza kuniita na kunieleza. Tume ya uchaguzi inapaswa kukemea. Haiwezekani kila tunapoingia kwenye uchaguzi mdogo, watu wakatane mapanga,”alisema Makongoro.
Aliongeza kuwa, watu wanaofanya vurugu wakati wa uchaguzi mdogo wanajulikana vyema, hivyo wakati umefika kwa bunge kutunga sheria ya kuwadhibiti ili kukomesha vitendo hivyo.
Makongoro alisema vyama vingi vya siasa vilivyopo sasa, Baba wa Taifa aliviacha na kama ni kuongezeka, huenda ni kimoja ama viwili. Alisema Mwalimu Nyerere ni mmoja wa waasisi wa siasa ya vyama vingi nchini baada ya kura ya maoni.
Alisema katika upigaji huo wa kura ya maoni, asimilia 80 ya watanzania hawakutaka vyama vingi wakati asilimia 20 ndio waliotaka na kwamba kwa kuzingatia idadi hiyo, kulikuwa hakuna haja ya kuwaunga mkono watu wachache.
“Lakini mwalimu siku zote alikuwa anaona mbali. Alisema kama unataka kudumisha amani, kungali mapema tusifanye kosa hilo. Hao wachache nao tuwaingize kwenye taratibu za nchi. Alitoa ushauri, anaheshimika, CCM na serikali ikakubali ushauri wake, katiba ya nchi ikabadilishwa,”alisema.
Makongoro alisema kwa sasa, hakuna juhudi za kutosha za kutoa raslimali kwa wasiokuwa nacho na kuongeza kuwa, wakati wa Mwalimu Nyerere, raslimali zilikuwepo, lakini ziligawiwa sawa na kasi ya waliotajirika haikuwa kubwa kama hivi sasa.
Alisema kasi hiyo kwa sasa imeongezeka, wasiokuwa nacho wamebaki hivyo na waliofaidika nazo, wameendelea kutajirika zaidi na kufanya tofauti kati yao iwe kubwa.
Makongoro pia alilalamikia kukiukwa kwa miiko ya uongozi, ambapo alisema jambo hilo limekuwa likisababisha matatizo makubwa katika jamii. Alisema serikali ilifanya kosa kubwa kutenganisha miiko ya uongozi na maadili ya uongozi.
“Viongozi wakati wa historia yetu, walipunguza masharti ya Azimio la Arusha yaliyokuwa yakiwabana, pengine kwa nia nzuri. Kuna viongozi hawakuruhusiwa kufanyakazi zingine, hali zao ni mbaya.
“Tunayo mifano hai ya viongozi, ambao wameruhusiwa kufanya shughuli zingine, wamestaafu, lakini hali zao ni ahueni kidogo. Lakini haina maana kwamba mwanya huu hautumiki na wengine, ambao wapo madarakani na wengine wamestaafu, kujitajirisha kupita kiwango,”alisema.
“Wakikurupuka na Azimio la Zanzibar ghafla, unaweza kufumba macho yako kuona mambo, ambayo ni kweli yapo sasa hivi. Tunao viongozi pengine aliwahi kuwa katibu mkuu wa CCM akastaafu, ukienda kumuona hali yake, bado yupo hai, hali yake ni mbaya kwa sababu alikuwa mwadilifu. Pengine azimio hilo lilimlenga mtu kama huyu,”aliongeza.
“Wapo wengine, ambao walijiangalia tu vizuri kwa nafasi zao, iwe waziri au yeyote, walitumia vizuri fursa hizo, waliishi vizuri na watoto wao kuwafikisha mahali wanajitegemea. Wengine walitumia mwanya huo kufanya balaa,” alisema.
“Mwalimu alikuwa anaishi kwa kufundisha kwa vitendo maisha yake yote. Usichanganye bahati aliyopata yeye ya kupendwa na kuhesimiwa na wananchi baada ya kifo chake kutokana na matendo yake na alivyojiweka.
“Waswahili wanasema imani huzaa imani, chuki huzaa chuki na upendo huzaa upendo. Yeye alipata bahati hiyo, wenzake aliowaachia walipanga utaratibu wa kumuenzi, si kila nchi inapanga hivyo, ilikuja kutokana na tabia zake.
“Mwalimu amepata bahati, nchi hii imeendelea kumpenda hadi sasa na nchi hii inamtunza mjane wake, haitunzi wanawe, ni bahati kwamba heshima yake ni nzuri na mazingira yanaonyesha hiyo ni kamali mbaya, angeweza kuondoka hana nyumba.
“Ameacha nyumba mbili, moja kajengewa na chama kwa lazima, nyingine alijengewa na jeshi, angebaki na nyumba yake binafsi ya Butiama, hali ingekuwa mbaya.
“Tusimsifu mwalimu kwa kuwa ameondoka, alikuwa mwadilifu. Huyo mwingine umemtayarishia utaratibu gani? Mwalimu alifanya hivyo kwa sababu aliishi kwa imani na watanzania wanamrudishia imani hiyo,”alisema Makongoro.
Makongoro alisema kwa mazingira ya Tanzania, historia imebadilika na kwamba, serikali iliyotawaliwa na ufisadi, haiwezi kuwa na usalama popote. Alisema nchi inapaswa kupata mwongozo kwa watu wenye kipato cha chini kutazamwa upya.
Amewaonya watu wanaojiona matajiri kwamba wanajidanganya kwa kudhani watanunua chama na heshima. Alisisitiza kuwa, kamwe hilo haliwezekani, isipokuwa linatokea kutokana na mazingira ya nchi kuwa maskini.

No comments:

Post a Comment