KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, October 13, 2011

Tamasha la maridhiano lafana Ngome Kongwe


VIWANJA vya Ngome Kongwe mwishoni mwa wiki iliyopita vilirindima burudani mwanana ya muziki wa taarab iliyoporomoshwa maalumu kwa ajili ya uzinduzi wa tamasha la maridhiano.
Tamasha hilo lililofanyika kwenye ukumbi wa klabu ya Mambo na kuhudhuriwa na mashabiki lukuki, lilipambwa kwa burudani ya muziki huo kutoka katika vikundi vya Culture na Nadi Ikhwani Safaa.
Vikundi hivyo viwili, vilipanda jukwaani kukata utepe wa tamasha hilo litakalodumu kwa miezi miwili, ambalo pia litapambwa kwa ngoma asilia na maigizo.
Tamasha hilo limeandaliwa na Kituo cha Kukuza Sanaa za Utamaduni na Maonyesho Zanzibar, chini ya ufadhili wa ubalozi wa Norway nchini Tanzania na Kampuni ya Simu ya Zantel.
Kikundi cha Culture kiliporomosha vibao vyake kadhaa vipya na vya zamani, vikiwemo 'Mpunga', kilichoimbwa na Fatma Dawa, 'Kama yalivyonipata' (Sabrina Hassan), 'Bahati' (Amina Juma), 'Nisubiri hadi lini' (Mtumwa Mbarouk), 'Tunapendana' (Mgeni Khamis) na ‘Vya kale dhahabu’ cha mkongwe Makame Faki.
Baadaee ilifuatia zamu ya Nadi Ikhwan Safaa, ambacho kiliwainua vitini mashabiki kwa vibao vyake vya 'Hata haikuwa' (Baadie Omar), 'Ua' (Raifa Mosi), 'Kwangu amepoa' (Samir Basalama), 'Nampenda mpenzi wangu' (Fauzia Abdullah) na 'Leo tena' ulioghaniwa na Saada Mohammed.
Baada ya kila kikundi kuonyesha umahiri wake, ukafika wakati kwa wakongwe hao kujumuika pamoja na kuimba nyimbo tatu maalumu kwa ajili ya kusherehekea miaka miwili ya maridhiano na mwaka mmoja wa serikali ya umoja wa kitaifa Zanzibar.
Nyimbo hizo ni 'Nchi yetu' ulioghaniwa na Fauzia Abdallah na Mgeni Khamis, 'Sabahal-Kheir Mpenzi' (Keis Juma na Mtumwa Mbarouk) huku bibiye, Fauzia Abdallah Mattar akiwainua mashabiki kwa wimbo wa siku nyingi 'Cheo chako'.
Akifungua tamasha hilo, Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Abdilahi Hassan Jihadi alipongeza uamuzi wa kituo hicho kubuni tamasha hilo na kuzishauri taasisi nyingine kuiga mfano huo kwa lengo la kuimarisha maelewano kati ya wananchi wa visiwa hivyo.
Tamasha lingine la aina hiyo limepangwa kufanyika Oktoba 15 mwaka huu kwenye uwanja wa Umoja ni Nguvu kisiwani Pemba.

No comments:

Post a Comment