KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, October 27, 2011

Simba yapania kumiliki TV na redio


Mkakati ni kuwa na wanachama milioni moja

Yatamba falsafa yake ni kuwa kama Barcelona

Na Ezekiel Kamwaga

MPAKA wakati huu ninapoandika makala hii, Simba inaongoza ligi kuu ya Tanzania Bara ikiwa na pointi 27 baada ya kucheza mechi 11. Pia inaongoza kwa kufunga mabao 18 na ni timu pekee iliyofungwa mabao machache.
Simba pia ina wastani mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa. Tofauti ya mabao yake ya kufunga na kufungwa ni 14 na ina idadi nzuri ya wachezaji waliofunga mabao kwenye mechi za ligi.
Kwa kawaida, timu inayochukua ubingwa ni ile ambayo haitegemei mtu mmoja kufunga. Unahitaji kuwa na wachezaji takribani watatu wanaopachika mabao ili uwe na uhakika wa kutwaa ubingwa.
Simba inao wachezaji wanne katika orodha ya wafungaji kumi wanaoongoza katika ligi kuu. Kuna Emmanuel Okwi, Patrick Mafisango, Felix Sunzu na Gervais Kago.
Haina tofauti na Barcelona ya Hispania, ambayo baada ya mechi nane za La Liga, inao wachezaji wanne katika orodha ya wafungaji wanaoongoza nchini humo; Lionel Messi, Cesc Fabregas, David Villa na Xavi Alonso.
Simba pia kwa sasa ina kikosi bora zaidi cha vijana wa chini ya miaka 20 katika timu zote zinazoshiriki Ligi Kuu. Humo ndipo wachezaji kama Frank ‘Nteze John’ Sekule, Abdallah Seseme, Hassan Khatib, Ramadhan Salum na Ramadhani Singano (Messi) wanapopikwa.
Vijana hawa wanatengenezwa na gwiji wa zamani wa Simba, Selemani ‘Veron’ Matola, akishirikiana na Amri ‘Stam’ Said. Lakini pia kuna kikosi cha vijana wa chini ya miaka 17 na kile cha chini ya miaka 14 kinachofundishwa na Maka Malwisi.
Hakuna wasiwasi kuwa, Simba ndiyo timu pekee hapa nchini yenye timu zisizo za ubabaishaji za vijana. Hii ina maana kuwa, katika kipindi kifupi kijacho, ‘Lunyasi’ itakuwa ikitengeneza wachezaji wake wenyewe kama ilivyo kwa Barcelona.
Klabu zote kubwa duniani hujitambulisha kwa falsafa fulani. Simba inajulikana kuwa falsafa yake ni mpira wa chini, wenye pasi na ufundi mkubwa. Ndiyo maana wengi wa mashabiki wa Simba hupenda pia soka ya Barcelona. Ni kwa sababu ya falsafa tu.
Katika mazoezi ya timu zetu za vijana, akina Matola na Maka husimamisha mpira wakati mchezaji anapobutua mpira mbele. Hiyo si falsafa ya Simba. Inacheza mpira na si kubutua. Vijana hawa wakiwa wakubwa, watajua wanachezea timu gani. Wanajengwa wangali vijana kuchezea Simba ikiwa ni pamoja na kuijua falsafa yake.
Kubwa kuliko yote, nje ya uwanja kuna umoja na mshikamano mkubwa baina ya viongozi na wanachama. Hakuna tena masuala ya mapinduzi, migogoro na rabsha, ambazo zilizoeleka miaka ya nyuma.
Amani na utulivu uliopo umewezesha timu kuendeshwa kisasa zaidi na pengine ni miongoni mwa klabu chache katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, ambazo walau zinaendeshwa katika mfumo wa kisasa.
Mchakato wa ujenzi wa uwanja wa kisasa katika eneo la Bunju jijini Dar es Salaam umeanza. Simba itakuwa na uwanja wake yenyewe kwa ajili ya mechi na mazoezi.
Kama mipango yote itakwenda kama ilivyopangwa, Simba inaweza kuwa klabu ya kwanza katika ukanda wa Afrika Mashariki kuwa na uwanja wake wenye uwezo wa kubeba watu takribani 30,000.
Uwanja huo utakuwa miongoni mwa vyanzo vikubwa vya mapato kwa klabu. La kufahamu ni kuwa, mchakato wa kujenga uwanja ni suala lenye kuhitaji subira ya hali ya juu.
Simba pia imeingia katika mkakati kabambe wa kuongeza idadi ya wanachama wake. Katika kipindi cha miezi sita iliyopita, maelfu ya mashabiki wa klabu wamefikiwa katika juhudi za kutaka kuongeza wanachama.
Matawi mapya yamefunguliwa. Kupitia kauli mbiu ya mwaka huu ya Siku ya Simba (Simba Day) iliyosema; Simba ni Matawi, Simba ni Wanachama, idadi ya wanachama wapya imeongezeka na wengi wanazidi na kutaka kujiunga.
Klabu kuwa na wanachama wengi ni suala la siha. Klabu kama Real Madrid ya Hispania (nasikia ipo ya Mbezi kwa Musuguri) ina nguvu kubwa kwa sababu ya kuwa na wanachama wengi.
Ada ya mwaka kwa mwanachama mmoja wa Simba ni Sh. 12,000. Kama timu ikiwa na wanachama milioni moja tu ( Lunyasi ina wapenzi zaidi ya milioni 10), klabu ina uwezo wa kukusanya kiasi cha Sh. bilioni moja kwa mwezi. Hii maana yake ni Sh bilioni 12 kwa mwaka mmoja tu.
Fedha hizi ni mara kumi ya zile zinazotolewa na wadhamini wa Ligi Kuu ya Tanzania (Vodacom) kwa timu zote zinazoshiriki ligi hiyo kwa mwaka mzima.
Fedha hizo zinamaanisha kuwa, Simba itakuwa na uwezo wa kumaliza ujenzi wa uwanja wake kwa kasi, kusajili wachezaji wa kiwango cha juu, kuongeza thamani yake kwa wadhamini na kushindana katika hadhi ya kimataifa.
Ndiyo maana, ni jambo la kheri kuwa idadi ya wanachama inaongezeka kila kukicha. Chini ya uongozi wa Mwenyekiti, Ismail Aden Rage (Mb) na Makamu Mwenyekiti, Geofrey Nyange ‘Kaburu’, suala la kuongeza idadi ya wanachama ni kipaumbele.
Si kitu ambacho wengi wanakifahamu, lakini Simba iko mbioni kuanzisha kituo chake cha televisheni (Simba TV). Katika muda si mrefu ujao, Simba itakuwa na kituo chake chenyewe cha runinga, gazeti na jarida. Tayari tovuti ya klabu imeanza, ingawa bado inakabiliwa na changamoto mbalimbali.
Iwapo mipango yote hiyo ya vyombo vya habari itakamilika kama ilivyopangwa, klabu itazidi kupiga hatua kubwa. Wapenzi, wanachama, wadhamini na wadau wengine watapata fursa ya kupata habari zote za klabu na kubadilishana taarifa kila wakati. Hili ni jambo muhimu sana katika maendeleo ya klabu.
Zaidi ya kuwa na vyanzo vya habari, vyombo hivi pia vinaweza kuwa vyanzo vizuri vya mapato. Hivyo mipango hii inamaanisha kuwa, wakati wapenzi wakiwa wanapata taarifa, klabu pia itakuwa inaongeza mapato yake.
Klabu ya Simba pia inafanyakazi kwa karibu na Kampuni ya Push Mobile. Kupitia ushirikiano huu, wapenzi takribani 34,000 wa Simba wanapata taarifa za kila siku za klabu kupitia simu zao za mkononi.
Simba imekuwa klabu ya kwanza Afrika Mashariki kuwa na utaratibu huu. Ni utaratibu, ambao unahakikisha wapenzi wake wanapata taarifa kabla ya wananchi wengine kuhusu klabu yao, lakini umesaidia pia kuongeza mapato ya klabu.
Changamoto ziko nyingi na kadri tuendavyo mbele, kuna changamoto zaidi zitakuja. Lakini jambo moja la msingi ni kwamba, Simba inaanza kwenda mbele kwa kasi sana. Na mwendo huo unahusisha masuala ya nje na ndani ya uwanja.
Siku moja, miaka mingi ijayo, watu watazungumzia kipindi hiki kuwa ndipo haswa Simba ilipoanza harakati za kufika pale itakapokuwa wakati huo.


Mwandishi wa makala hii ni Ofisa Habari wa klabu ya Simba na pia mwandishi wa habari.

No comments:

Post a Comment