KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, October 13, 2011

UCHE: Mimi si msagaji



LAGOS, Nigeria
MCHEZA filamu nyota wa Nigeria, Uche Uwuji amekanusha madai kuwa, anajihusisha na vitendo vya usagaji na kuongeza kuwa, taarifa hizo ni za uzushi mtupu.
Uche amesema wiki hii kuwa, picha zilizopigwa na kuchapishwa kwenye magazeti zikimwonyesha anabusiana na msichana mwenzake, hazikuwa na maana ya kujihusisha kwake na vitendo hivyo.
“Ego alikuwa mwanafunzi mwenzangu katika Chuo Kikuu cha Lagos na ni kama dada kwangu. Alikuja kwenye sherehe yangu ya kuzaliwa ili kufurahi nami. Ni kweli nilimpiga busu na kilichofuatia ni kuiona picha hiyo kwenye magazeti ikiambatana na habari za uzushi,”alisema.
“Mimi ni mtu wa Mungu. Sijihusishi kabisa na haya mambo yanayoenezwa na magazeti kuhusu mimi. Nilijihisi vibaya nilipoona taarifa hizi. Nilichoweza kufanya ni kucheka na kumuomba Mungu awasamehe waandishi wa habari kwa sababu hawaelewi madhara ya wanachokifanya,”aliongeza.
Uche amesema si jambo zuri kwa wanahabari kuandika habari za uzushi kwa lengo la kuvinufaisha vyombo vyao kibiashara. Alisema habari za aina hiyo zinachafua na kutia doa maisha ya watu.
Mwigizaji huyo amesema, anapenda kuolewa na mtu, atakayekuwa mcha Mungu na ambaye hawezi kuamini maneno ya uzushi kuhusu mkewe
“Ndoa nyingi za sasa hazidumu kwa sababu wanandoa hawamweki Mungu mbele. Kwangu mimi, nataka kuwa na mwanaume anayemweka mbele Mungu, mwanaume, anayeelewa kwamba, kwa Mungu lolote linawezekana,”alisema.
Uche amesema pia kuwa, licha ya kuishi singo, hana papara ya kutafuta mwanaume kwa ajili ya kuolewa.
“Sijawahi kuolewa, bado naishi singo, lakini sitafuti mwanaume,”alisema mwanadada huyo mwenye sura na umbo lenye mvuto.
Uche amesema baadhi ya vyombo vya habari vimekuwa vikiripoti taarifa nyingi kuhusu yeye, lakini nyingi ni za kutunga kwa sababu hazina ukweli.
Alisema baadhi ya taarifa hizo zimedai kwamba ana uja uzito na nyingine zimedai ana uhusiano wa kimapenzi na mwanasiasa mmoja wa nchi hiyo wakati si kweli.
“Kamwe sijawahi kupata uja uzito na hakuna aliyewahi kuniona nikiwa mja mzito. Sielewi kwa nini watu wanatunga habari hizi kuhusu mimi,”alisema.
“Pia sijawahi kuwa na uhusiano wowote wa kimapenzi na mwanasiasa. Sijihusishi na mambo hayo. Sielewi kwa nini watu wanapatwa na hisia hizi kuhusu mimi. Kuna mambo mengi, ambayo napaswa kutilia mkazo kwa sasa,”aliongeza.
Uche amesema haina maana kwamba hapendi kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mwanaume yeyote, bali muda huo kwake bado haujafika.
Mwanadada huyo amesema pia kuwa, suala la kufunga ndoa kwa sasa halipo kichwani mwake, lakini wakati utakapowadia, lazima afanye hivyo.
Alikiri kuwa, kwa mila na desturi za kabila lao la Igbo, alipaswa kuolewa tangu akiwa na umri mdogo, lakini kutokana na kuwa na mambo mengi yaliyomzunguka, anapaswa kuweka sawa kwanza maisha yake ya baadaye.
“Wakati ukiwadia, nitaolewa, lakini kama haujawadia, nitasubiri majaliwa ya Mungu kwa sababu ndiye mpangaji wa yote,”alisema.
Uche amesema ndoa ni kitu, ambacho kila mwanamke angependa kuwa nacho na kusisiti kuwa, iwapo ataolewa, hatojihusisha na uigizaji filamu kwa miaka mitano ili kuimarisha ndoa yake.
Mwanadada huyo amekiri kuwa, kazi yake imechangia kwa kiasi kikubwa kumfanya asiolewe kwa wakati huu kwa vile hutumia muda mwingi kutengeneza filamu.
Uche amezaliwa katika familia ya watoto sita. Baba yake ni mwanasheria, alioa wake wawili. Mama yake Uche ni mke wa pili. Ni mtoto wa pili kwa mama yake. Alizaliwa Lagos na kukulia katika mji huo.

No comments:

Post a Comment