KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, October 13, 2011

BELLA: Nakwenda kurekodi nyimbo zangu Ufaransa


MWIMBAJI na kiongozi wa bendi ya muziki wa dansi ya Akudo Impact, Christian Bella amesema moja ya malengo yake katika siku zijazo ni kuwa mwanamuziki wa kimataifa.
Bella alisema mjini Dar es Salaam wiki hii kuwa, katika kutimiza malengo yake hayo, amepanga kwenda kurekodi albamu yake binafsi nchini Ufaransa mwezi ujao.
Mwimbaji huyo mwenye sauti tamu na murua amesema, amepanga kufanya ziara ya maonyesho ya kimuziki barani Ulaya kwa vile anaamini anao uwezo wa kuwapagawisha mashabiki kwa tungo zake mwanana.
“Ipo siku nataka nifanye ziara ya kimuziki duniani. Kwa kuanzia, nimepanga kwenda kurekodi nyimbo zangu binafsi nchini Ufaransa,”alisema mwimbaji huyo anayependa kuimba kwa kutumia mtindo wa ‘acapela’.
Bella, ambaye ni mmoja wa waimbaji kutoka Congo wanaounda Akudo Impact amesema, tungo zake nyingi zinagusa hisia, ndio sababu zimepata umaarufu mkubwa kwa mashabiki wa hapa nchini.
Mwimbaji huyo alijiunga na Akudo mwaka 2007 na kujizolea umaarufu mkubwa kwa kibao chake cha ‘Yako wapi mapenzi’ kabla ya kuibuka na kibao cha ‘Safari sio kifo’.
Mbali ya vibao hivyo viwili vilivyomo kwenye albamu ya Impact ya bendi hiyo, Bella pia alirekodi albamu yake binafsi mwaka 2009 inayokwenda kwa jina la ‘Don’t panic’.
Bella amesema wakati alipowasili nchini mwaka 2007, hakuwa akifahamu kuzungumza na kuandika Kiswahili, lakini baada ya kujifunza kwa bidii, hivi sasa anaifahamu vyema lugha hiyo.
“Nimekuwa nikiandika nyimbo zangu mimi mwenyewe, siandikiwi na mtu. Mwanzoni nilikuwa naandika Kicongo na kuwauliza watu maana ya maneno ya Kiswahili,”alisema.
Amesema si kweli kwamba anatunga na kuimba zaidi nyimbo za mapenzi, isipokuwa mapenzi yanagusa sehemu kubwa ya maisha ya binadamu.
Bella amesema huwa anasikia raha ya aina yake na ya pekee anapokuwa akiimba, pengine kuzidi hata ile raha anayoipata mtu anayesikiliza nyimbo zake.
Mwimbaji huyo alisema, hapendi tabia ya kutunga nyimbo zenye mwelekeo wa kuwapiga vijembe wenzake wka sababu hiyo sio tabia yake.
“Napenda kuumiza kichwa changu kutunga nyimbo za kuwafurahisha mashabiki wangu. Sipendi nyimbo za madongo,”alisema.
Kwa mujibu wa Bella, hajasomea muziki bali ni kipaji alichozaliwa nacho kwa wazazi wake, ambao wote wawili walikuwa waimbaji kanisani.
Alisema bendi ya Akudo imekuwa ikitunga zaidi nyimbo zake kwa lugha ya kilingala kwa sababu imeshazoeleka na kupendwa na mashabiki wengi hapa nchini.
Pamoja na mafanikio makubwa ya bendi yake, Bella alisema wanamuziki wanaofaidika zaidi kimaisha ni wale wanaopiga muziki wa kizazi kipya.
Amesema kufanikiwa kwa wanamuziki hao kumechangiwa zaidi na muziki wao kutangazwa sana na vyombo vya habari kuliko aina nyingine za muziki.
Akizungumzia uvaaji wa mavazi ya nusu uchi kwa wacheza shoo, Bella alisema hilo halikwepeki kwa sababu ni sehemu ya burudani kwa mashabiki.
“Muziki si kanisa, ni kitu tofauti, ni staili, japokuwa si vizuri kuvaa vichupi kwenye steji, lakini hilo haliwezi kukwepeka,”alisema.
“Wao sio waliobuni uvaaji huo, wameukuta, lakini wakati mwingine huwa tukiwapangia kuvaa nguo za heshima tunapokwenda kufanya maonyesho kwenye maeneo maalumu,”aliongeza.
Bella amesema ukimya wa bendi yake umetokana na ziara ndefu ya kimuziki waliyoifanya kwa kipindi cha miezi mitatu na nusu katika mikoa ya Mwanza, Mara na Shinyanga. Alisema si kweli kwamba bendi yao imesambaratika.
Amesema kwa sasa wapo katika maandalizi ya kurekodi albamu yao ya pili, itakayojulikana kwa jina la History no change'. Alivitaja baadhi ya vibao vitakavyokuwemo kwenye albamu hiyo kuwa ni Umejificha wapi, Pongezi kwa wanandoa, Ubinafsi, umefulia, usikate tamaa, ubinadamu kazi na Usifuate wambeya.
Mwimbaji huyo amesema hawakuwa na haraka ya kurekodi albamu mpua kwa sababu albamu yao ya kwanza bado ilikuwa ikifanya vizuri sokoni na mashabiki wanavipenda vibao vyake.

No comments:

Post a Comment