'
Thursday, October 4, 2012
YANGA BADO SAAANA KWA SIMBA
MABINGWA wa soka wa Tanzania Bara, Simba jana waliendelea kudhihirisha moto wao kwa watani wao wa jadi Yanga, baada ya kutoka nao sare ya bao 1-1 katika mechi ya mzunguko wa kwanza iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Katika mechi hiyo, Simba ilionyesha kandanda safi na kushangiliwa kwa mayowe mengi na mashabiki wao huku chipukizi wake, Christopher Edward na Jonas Mkude wakionyesha kandanda maridadi.
Simba ilikuwa ya kwanza kuhesabu bao dakika ya nne lililofungwa kwa mkwaju mkali na kiungo Amri Kihemba baada ya gonga safi kati ya Mwinyi Kazimoto na Mrisho Ngasa.
Baada ya kufungwa bao hilo na kuzidiwa kwa muda mrefu, kocha Fred Felix Minziro alilazimika kufanya mabadiliko ya wachezaji, ambapo alimtoa Hamisi Kiiza na kumwingiza Frank Domayo.
Mabadiliko hayo yalileta uhai kidogo kwenye safu ya kiungo ya Yanga, ambayo pia ilikuwa ikiundwa na Athumani Chuji na Haruna Niyonzima.Timu hizo zilikwenda mapumziko Simba ikiwa mbele kwa bao 1-0.
Yanga ilijiimarisha zaidi kwa kumwingiza Didier Kavumbagu kuchukua nafasi ya Nizar Khalfan kabla ya kumwingiza Juma Abdul kuchukua nafasi ya
Kwa upande wa Simba, nayo ilimpumzisha Christopher, ambaye nafasi yake ilichukuliwa na Daniel Akuffour kabla ya kumtoa Kazimoto, aliyeumia na kuingia Haruna Moshi.
Yanga ilipata bao la kusawazisha katika kipindi hicho lililofungwa kwa njia ya penalti na Saidi Bahanuzi baada ya beki wa kushoto wa Simba, Paul Ngelema kuunawa mpira ndani ya eneo la hatari.
Baada ya Yanga kupata bao la kusawazisha, pambano hilo lilitawaliwa na ubabe, ambapo Simon Msuva wa Yanga alitolewa nje kwa kadi nyekundu na mwamuzi Mathew Akrama kwa kosa la kumchezea rafu mbaya Juma Nyoso wa Simba.
Mwamuzi huyo aliwashangaza mashabiki wengi baada ya kumwonyesha kadi ya njano badala ya nyekundu Haruna wa Simba kwa kosa la kumvunja mguu Kelvin Yondan wa Yanga.
Matokeo hayo yameiwezesha Simba kuendelea kujikita kileleni mwa ligi hiyo ikiwa na pointi 13 baada ya kucheza mechi tano, wakati Yanga inazo pointi nane baada ya kucheza idadi hiyo ya mechi.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment