KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, March 14, 2013

MAMILIONI YA OKWI YATAFUNWA


UONGOZI wa klabu ya Simba umepanga kutuma viongozi wake watatu kwenda Tunisia kufuatilia malipo ya ada ya uhamisho wa mshambuliaji, Emmanuel Okwi aliyeuzwa kwa klabu ya Etoile du Sahel.

Habari kutoka ndani ya Simba zimeeleza kuwa, viongozi hao wanatarajiwa kuondoka nchini mwishoni mwa wiki hii baada ya taratibu zote muhimu kukamilika.

Chanzo cha habari kimeeleza kuwa, uongozi wa Simba umefikia uamuzi huo baada ya kuzuka kwa utata kuhusu dola 300,000 (sh. milioni 450) zilizolipwa na Etoile du Sahel kwa Simba kwa ajili ya ada ya uhamisho.

Kwa mujibu wa chanzo hicho cha habari, inasemekana kuwa Etoile du Sahel ilishalipa nusu ya fedha hizo kwa Simba, lakini baadhi ya viongozi wameamua kuzitafuna.

Okwi aliuzwa kwa klabu hiyo mwishoni mwa mwaka jana, ikiwa ni siku chache baada ya kuongeza mkataba mpya na Simba na kulipwa mamilioni ya fedha.

"Unajua kumekuwepo na taarifa tofauti kuhusu malipo hayo, ndio sababu tumeamua kufuatilia kwa karibu ili tujue ukweli. Tumewatuma viongozi watatu kwenda Tunisia kufuatilia malipo hayo,"alisema mjumbe mmoja wa kamati ya utendaji ya Simba, ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini.

Aliongeza kuwa, taarifa walizozipata zinaeleza kuwa, Etoile du Sahel ilishalipa nusu ya fedha hizo kwa kiongozi mmoja wa Simba na kuahidi kumalizia fedha zilizobaki mwezi uliopita.

"Ajabu ni kwamba viongozi wote wanadai kuwa, hakuna fedha zilizolipwa. Haiwezekani, tunahisi hapa kuna ujanja umefanyika, tutachunguza hadi tupate ukweli,"alisema mjumbe huyo.

Kwa mujibu wa mjumbe huyo, iwapo ni kweli fedha hizo zimelipwa na baadhi ya viongozi wamezitafuta, watachukuliwa hatua kali ikiwa ni pamoja na kufukuzwa uanachama.

Mapema wiki hii, Katibu Mkuu wa Simba, Evodius Mtawala alikaririwa akisema kuwa, klabu yake inadai fedha nyingi kutoka kwa watu mbalimbali, ikiwemo klabu ya Etoile Du Sahel, ambayo alisema wanaidai zaidi ya sh. milioni 450 za mauzo ya Okwi.

No comments:

Post a Comment