'
Sunday, March 24, 2013
CHOKI; HATUWEZI KULINGANA NA WACONGO KIMUZIKI
KIONGOZI wa bendi ya muziki wa dansi ya Extra Bongo, Ally Choki amesema si rahisi kuyalinganisha mafanikio ya wanamuziki wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo na yale ya Watanzania.
Choki alisema mjini Dar es Salaam wiki hii kuwa, wanamuziki wa Congo wamepata mafanikio makubwa kimuziki kutokana na muziki wao kukubalika kimataifa.
Mbali na muziki wao kukubalika kimataifa, Choki alisema wanamuziki wa Congo kama vile Fally Ipupa na Koffi Olomide wanao udhamini wa uhakika ndio sababu wanaweza kukaa muda mrefu bila kurekodi albamu.
"Mauzo ya albamu moja ya mwanamuziki wa Congo kama vile Fally Ipupa na Koffi Olomide, yanaweza kuwafanya wapate pesa za kutumia kwa miaka minne hadi mitano, tofauti na wanamuziki wa Tanzania,"alisema Choki.
Alisema kutokana na ukweli huo, si rahisi kuyalinganisha mafanikio ya wanamuziki wa Congo na Tanzania kwa sababu yana tofauti kubwa.
Choki alitetea utaratibu wa bendi za Tanzania kufanya maonyesho matatu hadi manne kwa wiki kwa sababu ndiyo yanayowaingizia pesa nyingi kuliko mauzo ya albamu.
"Bendi za Tanzania zitaendelea kupata pesa kutokana na maonyesho ya kwenye kumbi za burudani na wenzetu wataendelea kutegemea mauzo ya albamu kwa sababu muziki wao ni wa uhakika,"alisisitiza Choki.
Kwa upande wake, mwimbaji nyota wa muziki wa dansi nchini, Ramadhani Masanja 'Banza Stone' amesema ni jambo lisilokwepeka kwa bendi za Tanzania kufanya maonyesho matatu au manne kwa wiki.
Banza alisema mjini Dar es Salaam wiki hii kuwa, mauzo ya albamu hayawezi kuzitosheleza bendi kimapato kutokana na usimamizi mbovu wa sheria ya hatimiliki.
"Kwa hapa Tanzania, bendi kufanya maonyesho matatu au manne kwa wiki ni sawa kwa sababu ndizo siku, ambazo mashabiki wanakwenda kustarehe, hakuna ujanja mwingine wa kutuwezesha kupata mapato,"alisema.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment