'
Thursday, March 7, 2013
ZFA YAMKUBALIA MAKUNGU KUJIUZULU
HATIMAYE Kamati ya Utendaji ya Chama cha Soka cha Zanzibar (ZFA), imekubali ombi la Rais wake, Aman Ibrahim Makungu kujiuzulu nafasi hiyo.
Katika barua iliyoandikwa na ZFA Machi 4, mwaka huu na kutiwa saini na Makamu wa Rais Kisiwani Unguja, ambaye pia ni Kaimu Rais wa ZFA kikatiba, Alhaj Haji Ameir, yenye kumbukumbu namba ZFA/PRESIDENT/VOL.11/05, ombi hilo limekubaliwa.
Barua hiyo imesema Kamati ya Utendaji ya ZFA Taifa, ilikutana na kujadili kwa kina ombi la kujiuzulu la Makungu na kutafakari kwa makini na hatimaye kufikia uamuzi wa kulikubali.
Katika barua hiyo, ZFA Taifa wajumbe wamemshukuru Makungu kwa msaada alioutoa kwa chama hicho na kumuomba aendelee kukisaidia wakati wowote atakapohitajika.
Nakala za barua hiyo zimetumwa kwa Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Michezo la Zanzibar pamoja na Msaidizi wa Katibu wa ZFA Kisiwani Pemba.
Kwa mujibu wa katiba ya ZFA, chama hicho kitalazimika kufanya uchaguzi mdogo wa kujaza nafasi hiyo ndani ya siku 90.
Miezi miwili iliyopita, Makungu aliandika barua ya kuomba kujiuzulu nafasi hiyo kwa kile alichodai kuwa ni kuchoshwa na baadhi ya viongozi wa chama hicho wasiotaka mabadiliko huku wakionekana kuwagawa baadhi ya wajumbe wa ZFA kwa kisingizio cha U-Unguja na U-Upemba.
Hata hivyo, Kamati ya Utendaji ya ZFA Taifa ililikataa ombi hilo kwa madai kuwa, litachangia kurejesha nyuma soka ya Zanzibar.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment