'
Thursday, March 14, 2013
UHURU MEDIA YATINGA ROBO FAINALI KOMBE LA NSSF
TIMU ya soka ya Uhuru Media juzi ilifuzu kucheza robo fainali ya michuano ya Kombe la NSSF baada ya kuichapa Mlimani TV mabao 2-1 katika mechi iliyopigwa kwenye uwanja wa klabu ya Sigara, Chang'ombe, Dar es Salaam.
Kutokana na ushindi huo, Uhuru Media sasa itakutana na mshindi wa mechi kati ya Jambo Leo na Global iliyochezwa jana kwenye uwanja huo.
Iliwachukua Uhuru dakika nne kuhesabu bao la kwanza lililofungwa kwa kichwa na Saidi Ambua kutokana na mpira wa adhabu uliopigwa na Moni Lyambiko.
Bao la pili la Uhuru lilifungwa na Moni dakika ya 25 kwa mpira wa adhabu uliomponyoka kipa Aikael wa Mlimani TV aliyekuwa akijiandaa kuuweka kwenye himaya yake.
Uhuru ilipata pigo dakika ya 65 baada ya kipa wake, Ricardo Bigenda kutolewa nje kwa kadi nyekundu kwa kosa la kudaka mpira nje ya eneo lake. Awali, Ricardo alionyeshwa kadi ya njano kwa kosa hilo.
Ilibidi Uhuru impuzishe kiungo wake, Nassoro Nassoro na kumwingiza kipa Emmanuel Koba, ambaye alishindwa kuzuia shuti la mpira wa adhabu lililopigwa na Singute wa Mlimani TV na kuwa bao la kwanza.
Bao hilo liliongeza kasi kwa Mlimani TV, ambayo iliwapumzisha wachezaji wake watano na kuingiza wengine kwa lengo la kuiongezea nguvu.
Hata hivyo, ukuta wa Uhuru uliokuwa chini ya Brendan, Moni, Haji Iddi na Abdalla Saidi ulikuwa imara kuokoa hatari zote zilizosababishwa na safu ya ushambuliaji ya Mlimani TV.
Katika mechi za netiboli, IPP ilitoa kipigo kikali cha mabao 33-4 dhidi ya Jambo Leo wakati Business Times iliikung'uta Changamoto bila huruma mabao 69-4.
Michuano hiyo inatarajiwa kuendelea tena leo kwa mechi kati ya Mwananchi na Sahara zitakazomenyana kwenye uwanja wa Sigara wakati TSN itamenyana na Tumaini kwenye uwanja wa DUCE.
Katika netiboli, mabingwa watetezi Habari Zanzibar watamenyana na wenyeji NSSF katika mechi za kwanza za robo fainali wakati TBC itamenyana na Free Media.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment