'
Sunday, March 31, 2013
YANGA YABANWA, SIMBA YACHECHEMEA, AZAM YAPASUA ANGA
VINARA wa ligi kuu ya Tanzania Bara, Yanga jana walipunguzwa kasi baada ya kulazimishwa kutoka suluhu na Polisi Moro katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro.
Sare hiyo imeifanya Yanga iwe na pointi 49 baada ya kucheza mechi 21, ikifuatiwa na Azam yenye pointi 43, baada ya kuichapa Ruvu Shooting bao 1-0.
Kukosekana kwa kiungo Haruna Niyonzima kulionekana dhahiri kuipunguza kasi Yanga, hasa katika safu yake ya ushambuliaji.
Beki Mbuyu Twite alilazimika kufanyakazi ya ziada dakika ya 24 kuokoa mchomo mkali wa mshambuliaji Mokili Rambo wa Polisi uliokuwa ukielekea kwenye nyavu.
Kipa wa Polisi, Kondo Salum naye alilazimika kufanya kazi ya ziada dakika ya 26 kupangua mpira wa kichwa wa beki Nadir Haroub ‘Cannavaro’ wa Yanga kufuatia kona maridadi ya David Luhende.
Said Bahanuzi ‘Spider Man’ aliikosesha Yanga bao la wazi, baada ya kuchelewa kuiwahi krosi nzuri ya Simon Msuva na mpira ukapitiliza hadi mikononi mwa kipa wa Polisi.
Nayo Azam ilijipatia bao la pekee katika mechi yake dhidi ya Ruvu Shooting dakika ya 44 lililofungwa na Kipre Tchetche.
Wakati huo huo, mabingwa watetezi Simba jana waliendelea kuchechemea baada ya kulazimishwa sare ya mabao 2-2 na Toto African katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa CM Kirumba mjini Mwanza.
Kwa matokeo hayo, Simba SC inabaki nafasi ya tatu kwa pointi zake 35 baada ya kucheza mechi 21, nyuma ya Azam yenye pointi 43 na Yanga 49 kileleni.
Toto African ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya 25 lililofungwa na Mussa Saidi kabla Rashid Ismail kuisawazishia Simba dakika ya 2.
Mrisho Ngasa aliyeingia kipindi cha pili, aliiongezea Simba bao la pili dakika ya 62 kwa shuti kali lililokwenda moja kwa moja wavuni.
Toto ilisawazisha dakika ya 72 kwa bao lililofungwa na Selemani Kibuta baada ya mabeki wa Simba kujichanganya.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment