'
Friday, March 8, 2013
BINGWA KOMBE LA NSSF KUZOA MIL NNE, VUMBI KUANZA KUTIMKA KESHO
BINGWA wa mwaka huu wa michuano ya soka ya Kombe la NSSF katika mchezo wa soka atazawadiwa kitita cha sh. milioni nne.
Akitangaza zawadi hizo kwa waandishi wa habari mjini Dar es Salaam leo, Meneja Kiongozi, Idara ya UHusiano na Huduma kwa Wateja wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Eunice Chiume alisema mshindi wa pili atazawadiwa sh. milioni tatu wakati mshindi wa tatu atapata sh. milioni 1.5.
Eunice alisema kwa upande wa netiboli, bingwa atazawadiwa sh. milioni tatu, mshindi wa pili atapata sh.milioni mbili na wa tatu sh. milioni moja.
Alisema NSSF imeamua kutumia sh. milioni 13.6 kwa ajili ya zawadi za timu na wafungaji bora kwa lengo la kuongeza ushindani kwa timu shiriki.
Kwa mujibu wa Eunice, wafungaji bora wa michezo yote miwili watapata zawadi ya sh. 300,000 kila mmoja.
Eunice alisema michuano hiyo inatarajiwa kuanza kesho asubuhi kwa mechi kati ya mabingwa watetezi Habari Zanzibar na Changamoto katika soka wakati NSSF itamenyana na Mlimani TV katika netiboli.
Aliongeza kuwa, mgeni rasmi katika sherehe za ufunguzi wa michuano hiyo anatarajiwa kuwa Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudencia Kabaka.
Michuano ya mwaka huu ni ya 10 kuandaliwa na kudhaminiwa na NSSF na ni maalumu kwa ajili ya vyombo vya habari. Michuano ya mwaka huu inatarajiwa kugharimu sh. milioni 120 na itazishirikisha timu 17 za soka na 15 za netiboli.
Timu zitakazoshiriki katika michuano ya mwaka huu ni wenyeji NSSF, IPP, TBC, Mwananchi, Uhuru Media, Business Times, Sahara Communications, Global Publishers, Free Media, Changamoto.
Timu zingine ni Mlimani TV, Tumaini Media, Redio Kheri, New Habari, TSN, Jambo Leo na Habari Zanzibar.
Mashindano haya yalianzishwa 2004 kwa lengo la kujenga uhusiano kati ya NSSF na vyombo vya habari, ikiwa ni wiki ya NSSF, inayosherehekewa Machi ya kila mwaka.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment