'
Sunday, March 31, 2013
MOURINHO, ABRAMOVICH WAMALIZA TOFAUTI ZAO
LONDON, England
MMILIKI wa klabu ya Chelsea ya England, Roman Abramovich amemaliza tofauti kati yake na kocha mkuu wa zamani wa timu hiyo, Jose Mourinho na kukubaliana kumrejesha katika klabu hiyo.
Abramovich na Mourinho walifikia makubaliano hayo Jumatatu iliyopita baada ya kufanya mazungumzo kwa faragha.
Mourinho alikuwepo nchini England kwa ajili ya kushuhudia mechi ya kirafiki ya kimataifa kati ya Brazil na Russia iliyochezwa kwenye uwanja wa Stamford Bridge. Katika mechi hiyo, timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1.
Abramovich alitofautiana na Mourinho baada ya kocha huyo kushindwa kuiwezesha Chelsea kutwaa mataji aliyokuwa akiyataka baada ya kuiwezesha kutwaa ubingwa wa England, Kombe la FA na Kombe la Carling.
Gazeti la Daily Mail la Uingereza liliripoti jana kuwa, Abramovich amekuwa akimtaka Mourinho arejee England kwa mara ya pili kwa ajili ya kuinoa Chelsea.
Tayari Abramovich na Mourinho wameshafikia makubaliano hayo, lakini hakuna yeyote kati yao aliyekuwa tayari kuzungumzia suala hilo.
Akihojiwa na kituo cha televisheni cha Sky Sports, Mourinho alisema kwa sasa bado yeye ni kocha mkuu wa Real Madrid ya Hispania na kwamba lengo lake ni kuiwezesha timu hiyo kutwaa taji la ligi ya mabingwa wa Ulaya msimu huu.
Hata hivyo, Mourinho hakuona aibu kuelezea mapenzi yake kwa England na kuvifananisha vyombo vya habari vya nchi hiyo kuwa sawa na sukari na pilipili katika chakula chake cha kila siku.
Abramovich amekuwa na mapenzi makubwa kwa Mourinho baada ya kushindwa kumpata kocha wa zamani wa Barcelona, Pep Guardiola, ambaye amejiunga na Bayern Munich ya Ujerumani.
"Siwezi kupinga. Licha ya hali hii ya hewa, napenda kuwepo hapa,"alisema Mourinho, ambaye pia ni maarufu kwa jina la Special One.
"Nafikiri siku moja nitarejea katika ligi kuu ya England katika klabu ya Chelsea au nyingineyo. Chelsea ipo moyoni mwangu, hivyo siku moja nitarejea. Tunayo nyumba hapa, binti yetu anakuja kusoma London hivyo kuwepo kwangu London ni kitu cha kawaida kwetu," aliongeza kocha huyo.
"Lakini kila ninapokuja hapa na watu wakiniona nakatiza mitaani ama kufanya manunuzi, wanaanza kuunganisha mambo. Sijali kwa sababu kila siku ninapopata nafasi, naeleza wazi kwamba napenda kuwepo hapa. Nilikuwa na wakati mzuri hapa na kwamba nitarejea. Huwa sipendi kusema mengi kuhusu hisia hizi kwa sababu napenda kuwepo hapa,"aliongeza.
Mbali na Chelsea, Mourinho pia amekuwa akihusishwa na mipango ya kujiunga na Manchester United na Manchester City.
Kwa sasa, Chelsea inanolewa na kocha wa muda, Rafael Benitez, ambaye mashabiki wa klabu hiyo wamekuwa hawamuungi mkono kutokana na matokeo mabaya katika ligi.
"Nilikuwepo Manchester wiki tatu zilizopita na hali ya hewa ya huko ilikuwa nzuri zaidi. Nilifanya mazungumzo na Sir Alex Ferguson kwa kumtumia ujumbe japokuwa alikuwa akikabiliwa na mechi,"alisema Mourinho.
"Lakini Manchester ni utawala wa Sir Alex na ningependa kazi hiyo iwe ya kudumu kwake. Bila shaka haiwezi kuwa hivyo, lakini ningependa aendelee na kazi hiyo kwa miaka mingi zaidi," alisisitiza.
Mourinho pia aliizungumzia Manchester City na kocha wake, Roberto Mancini. Alisema kutokana na kocha huyo kuiwezesha Manchester City kutwaa ubingwa wa ligi msimu uliopita, hafikirii iwapo yanaweza kufanyika mabadiliko yoyote.
"Hata kwa Benitez, natumaini kila kitu kinakwenda vizuri kwake na watamaliza msimu vizuri,"alisema Mourinho, ambaye pia amewahi kuzinoa FC Porto ya Ureno na Inter Milan ya Italia.
"Mwisho wa siku, nipo Real Madrid, nakabiliwa na majukumu mazito hadi mwisho wa msimu huu. Tumefuzu kucheza robo fainali ya ligi ya mabingwa wa Ulaya, tumefuzu kucheza fainali ya Kombe la Mfalme, hivyo watu wanaelewa mimi ni kocha wa kulipwa na kwamba kwa sasa nafikiria kazi yangu Real Madrid," alisema kocha huyo.
Mourinho alisema anaona fahari kuwa kocha aliyeweza kutwaa mataji mawili ya ligi ya mabingwa wa Ulaya akiwa na timu tofauti na kwamba angependa kutwaa tena taji hilo msimu huu.
Kocha huyo alisema atavunjika moyo iwapo atashindwa kutwaa taji hilo msimu huu baada ya baadhi ya vigogo kama vile Manchester United na Chelsea kutolewa hatua ya awali.
Hata hivyo, alikiri kuwa timu zote nane zilizosalia katika michuano hiyo ni nzuri na yoyote inaweza kutwaa ubingwa.
Msimu huu umekuwa mbaya kwa Mourinho, kufuatia Real Madrid kuzidiwa kwa tofauti ya pointi 13 na mahasimu wao, Barcelona katika msimamo wa ligi kuu ya Hispania.
Matumaini pekee ya kocha huyo kwa sasa yamebaki katika michuano ya ligi ya mabingwa wa Ulaya na Kombe la Mfalme wa Hispania, ambapo Real Madrid itacheza fainali dhidi ya Atletico Madrid.
Real Madrid imepangwa kumenyana na Galatasaray ya Uturuki katika robo fainali ya ligi ya mabingwa wa Ulaya.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment