KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, March 14, 2013

SIMBA WAMWANGUKIA HANSPOPE



Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha ya Simba, Rahma Al-Kharoos akisalimiana na wanachama wa tawi la Mpira Pesa alipotembelea tawi hilo mwishoni mwa wiki iliyopita Magomeni, Dar es Salaam. (Picha kwa hisani ya Simba).

KLABU ya Simba imepanga kumshawishi mwenyekiti wake wa kamati ya usajili, Zacharia Hanspope abadili uamuzi wake wa kujiuzulu wadhifa huo.

Kaimu Makamu Mwenyekiti wa Simba, Joseph Itang'are alisema mjini Dar es Salaam juzi kuwa, wameunda kamati ya watu watatu kwa ajili ya kwenda kumshawishi Hanspope.

Itang'are, maarufu kwa jina la Kitare alisema uamuzi wa kuunda kamati hiyo ulifikiwa katika kikao cha viongozi wa matawi ya Simba ya mjini Dar es Salaam kilichofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita.

Alisema kamati hiyo ilitarajiwa kukutana na Hanspope wakati wowote kuanzia jana.Hata hivyo, hakuwa tayari kutaja majina ya wajumbe wa kamati hiyo, lakini alisema ni watu maarufu na wanaoheshimika ndani ya Simba.

Kaimu Makamu Mwenyekiti huyo wa Simba alisema uongozi umeshaanza kuchukua hatua za kunusuru kuzuka kwa mgogoro ndani ya klabu hiyo, ikiwa ni pamoja na kumaliza tofauti zilizojitokeza kati yake na tawi la Mpira Pesa.

Alisema baadhi ya wajumbe wa kamati ya utendaji ya Simba, wakiongozwa na Rahma Al-Kharoos walitembelea tawi hilo mwishoni mwa wiki iliyopita na kuzungumza na wanachama.

"Napenda kutumia nafasi hii kuwaomba wanachama wote wa Simba kuendeleza utulivu na mshikamano ndani ya klabu ili tuwe kitu kimoja. Tukiwa kitu kimoja tutaweza kutatua matatizo yetu kwa ufanisi. Tukigawanyika tutazidi kuharibikiwa," alisema.

Wakati huo huo, Mwenyekiti wa tawi la Mpira Pesa, Ustaadh Masoud amesema hawana nia mbaya dhidi ya uongozi wa Simba, isipokuwa kuna mambo ambayo ni lazima yawekwe sawa kwa lengo la kuondoa tofauti zilizokuwapo siku za nyuma.

No comments:

Post a Comment