KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, March 7, 2013

JULIO AWATWISHA ZIGO VIONGOZI SIMBA




KOCHA Msaidizi wa timu ya soka ya Simba, Jamhuri Kihwelo 'Julio' amesema kutolewa kwao mapema katika michuano ya klabu bingwa Afrika kulitokana na maandalizi mabovu.

Julio alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, uongozi wa Simba haukufanya maandalizi mazuri kwa ajili ya mechi hiyo kama walivyofanya wapinzani wao.

Simba ilirejea nchini juzi usiku, ikitokea Angola, ambako ilikwenda kurudiana na Recreativo Libolo na kupigwa mweleka wa mabao 4-0.

Kipigo hicho kiliifanya Simba itolewe kwa jumla ya mabao 5-0 baada ya kupigwa mweleka wa bao 1-0 na Libolo katika mechi ya awali iliyochezwa wiki mbili zilizopita kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Julio alisema wachezaji wa Libolo wanauchukulia mchezo wa soka kuwa ajira, tofauti na wanasoka wa Tanzania, ambao amedai kuwa, hawajui umuhimu wa mchezo huo kwao.

Alisema wachezaji wa Simba hawapaswi kulaumiwa kutokana na timu hiyo kuondolewa mapema. Alisema lawama hizo zinapaswa kuelekezwa kwa uongozi wa klabu hiyo.

"Mechi zetu na Libolo zilikuwa ngumu, lakini wachezaji walicheza vizuri na hakuna wa kumlaumu kwa vile walitimiza wajibu wao. Tungepeta maandalizi mazuri, nadhani tungefanya vizuri,"alisema kocha huyo, ambaye ni mchezaji wa zamani wa Simba.

Amewataka mashabiki wa Simba kuwa na subira kwa vile timu hiyo inajipanga vizuri ili iweze kumaliza michuano ya ligi kuu ya Tanzania Bara ikiwa nafasi ya pili.

Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Baraza la Wazee la Simba, Hamisi Kilomoni amewataka wanachama wa klabu hiyo kutulia wakati uongozi ukipanga tarehe ya kufanyika kwa mkutano mkuu.

Kilomoni alisema mjini Dar es Salaam juzi kuwa, kwa vile uongozi umeshatamka kwamba utaitisha mkutano huo wakati wowote, wanachama wanapaswa kuwa na subira.

Alisema kwa sasa, uongozi wa Simba unasubiri ripoti ya Kocha Patrick Liewig kuhusu kutolewa mapema kwa timu hiyo katika michuano ya klabu bingwa Afrika kabla ya kupanga tarehe ya mkutano huo.

Simba ilirejea nchini juzi ikitokea Angola, ambako ilipigwa mweleka wa mabao 4-0 na Libolo na kutolewa katika michuano hiyo kwa kipigo cha jumla cha mabao 5-0.

"Nawaomba wanachama wenzangu wa Simba watulie, kama wanazo hoja zao wasubiri tarehe ya mkutano, siku hiyo watapata nafasi ya kutoa madukuduku yao, wasifanye fujo kwa vile Simba ni klabu ya kistarabu,"alisema.

No comments:

Post a Comment