KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, March 14, 2013

STARA ALALAMIKIA UGUMU WA KUTENGENEZA FILAMU




MSANII nyota wa fani ya filamu nchini, Wastara Juma amesema utengenezaji wa filamu kwa sasa ni kazi ngumu kwa wasanii kuliko ilivyokuwa miaka ya nyuma.

Wastara, ambaye ni maarufu zaidi kwa jina la Stara alisema mjini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki iliyopita kuwa, baadhi ya wasanii wameshaanza kukata tamaa kutokana na ugumu wa kazi hiyo.

Alisema watayarishaji wa filamu wamekuwa wakikaa muda mrefu kusotea kazi zao kutokana na wauzaji na wasambazaji kuzichelewesha bila ya sababu za msingi.

Stars alisema hali hiyo imesababisha filamu nyingi zinapoingia sokoni, kuonekana zimepitwa na wakati kwa sababu ya kuchelewa kuuzwa.

"Soko la filamu kwa sasa ni gumu kuliko ambavyo jamii inaliona. Ukiona kazi imetoka sokoni, ujue watu wametabika kwa kiwango kikubwa,"alisema.

Kutokana na ugumu wa kazi hiyo na pia mihangaiko ya kumuuguza na kumpoteza mumewe, Stara alisema ameamua kupumzika kwa muda kujihusisha na fani hiyo.

Stara alisema amefikia uamuzi huo kwa lengo la kuipumzisha na kuijenga upya akili yake kabla ya kujipanga upya.

Stara alifiwa na mumewe, Juma Kilowoko mwaka jana kutokana na ugonjwa wa kansa ya utumbo. Kilowoko, ambaye ni maarufu zaidi kwa jina la Sajuki, alikuwa mmoja wa wasanii wa bongo movie.

"Ninasafiri wiki ijayo kwenda Arabuni kwa ajili ya kupumzika. Nitakapokuwa mapumziko, nitaangalia nitoke vipi, yaani nifanyekazi kwa staili ipi,"alisema mwanamama huyo, ambaye ni mama wa mtoto mmoja, aliyezaa na Sajuki.

Stara alisema familia yake ndiyo iliyoamua aende huko kwa lengo la kujifariji baada ya matatizo yaliyomkuta.

Mwanamama huyo alikiri kuwa, yapo baadhi ya mambo, ambayo hawezi kuyasahau katika maisha yake kutokana na kifo cha Sajuki.

“Siku aliyoaga dunia, jana yake aliniomba nisiondoke na kumuacha peke yake, lakini kwa sababu zilizokuwa nje ya uwezo wangu, niliondoka. Naumia kwa kuwa ningejua atakufa, nisingeondoka,” alisema Stara.

Alilitaja jambo lingine kuwa ni ombi la Sajuki kumtaka watengeneze filamu ya mapenzi, inayofanana na mikasa mbalimbali iliyowahi kuwakuta katika maisha yao.

Alisema waliitunga filamu hiyo miaka miwili iliyopita na Sajuki aliomba acheze anakufa na kurudi tena duniani. "Nikilikumbuka hili naumia sana, siwezi kusahau maishani mwangu,"alisema.

Stara alisema pia kuwa, hawezi kuisahau siku, ambayo Sajuki alimuomba mjomba wake amletee gunia la mkaa, siku atakaporejea kutoka katika safari yake nchini Uganda.

“Tuliokuwepo tulimshangaa na kumuuliza kwa nini? Akasema huo mkaa una kazi yake, amletee tu. Cha kushangaza, mjomba wake aliuleta siku ambayo ni ya msiba wake,” alisema Stara.

Alilitaja tukio lingine, ambalo hawezi kulisahau katika maisha yake kuwa ni ombi la mumewe kutaka arekodi wimbo alioutunga kwa ajili ya kuwashukuru watanzania.

“Wimbo huo alisema utaitwa Nisameheni. Cha kushangaza, alipoanza kunishushia mistari, akaanza kuchanganya na mambo yasiyoeleweka, nikahisi ameanza kuchanganyikiwa. Nilimuita daktari wake na hata lile zoezi la kurekodi halikufanyika tena,” alisema mwanamama huyo.

No comments:

Post a Comment