KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Sunday, March 31, 2013

WADAU WA FILAMU WAMPONGEZA WEMA KWA KUMWOKOA KAJALA



WADAU mbalimbali wa fani ya filamu wamempongeza msanii nyota wa tasnia hiyo nchini, Wema Sepetu kwa kumwokoa msanii mwenzake, Kajala Masanja kwenda jela kutumikia kifungo cha miaka 12.

Wakizungumza na Burudani kwa nyakati tofauti mjini Dar es Salaam jana, wadau hao walisema kitendo kilichofanywa na Wema kumlipia Kajala faini ya sh. milioni 13 ni cha ujasiri na mfano wa kuigwa.

Kajala, ambaye alisota rumande kwa mwaka mmoja, alinusurika kwenda jela Jumatatu iliyopita baada ya kupatikana na hatia ya makosa mawili kati ya matatu ya kutakatisha fedha.

Mume wa msanii huyo, Faraja Chambo alihukumiwa kwenda jela kutumikia kifungo cha miaka 12 baada ya kupatikana na hatia ya makosa yote matatu na kushindwa kulipa faini ya sh. milioni 213.

Kajala na Chambo, walifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Marchi 15, mwaka jana, wakikabiliwa na mashitaka matatu ya kula njama ya kubadilisha umiliki wa nyumba iliyopo Kunduchi, Salasala, Dar es Salaam kinyume cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa.

"Kwa kweli kitendo kilichofanywa na dada huyu ni ujasiri wa aina yake. Wapo wasanii wengine maarufu wa filamu, lakini wameshindwa kumsaidia mwenzao kama alivyofanya Wema,"alisema Robert Justine, mkazi wa Kiwalani, Dar es Salaam.

Mwanadada Lucy Tesha, mkazi wa Mnazi Mmoja, Dar es Salaam alisema, alichokifanya Wema, hakuna mwingine wa kumlipa fadhila zake, isipokuwa Mwenyezi Mungu.

"Wema asisubiri kulipwa wema wake hapa duniani. Atalipwa na Mungu,"alisema dada huyo.

Mkazi mwingine wa Buguruni, aliyejitambulisha kwa jina la Chambo Waziri alisema, Wema amefanya kile, ambacho si watanzania wengi wanaweza kukifanya.

"Fikiria, Kajala amehukumiwa kwenda jela miaka 13, wazazi wake ni masikini, yeye na Wema ni marafiki wa kawaida tu, lakini amemsaidia utadhani ndugu yake wa kuzaliwa tumbo moja,"alisema.

Shamsa Majid, mkazi wa Ilala Boma alisema, msanii mwingine anayestahili kupongezwa ni Mahsen Awadh, maarufu kwa jina la Dk. Cheki kutokana na kuwa mstari wa mbele kusaidia wenzake.

"Kwa kweli nampa big up Cheni. Alikuwa mstari wa mbele kumsaidia Lulu (Elizabeth Michael) na juzi tumemuona akiwa mstari wa mbele kumsadia Kajala. Hawa wengine wamebaki maneno maneno tu,"alisema.

No comments:

Post a Comment