KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, March 7, 2013

TFF YAUFYATA KWA SERIKALI



HATIMAYE Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limekutana na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk.Fenella Mkangara na kujadiliana naye kuhusu mgogoro uliojitokeza katika uchaguzi mkuu wa chama hicho.

Kikao hicho kati ya uongozi wa juu wa TFF, ukiongozwa na Rais wake, Leodegar Tenga na Dk. Fenella kilifanyika kwenye ofisi za wizara hiyo mjini Dar es Salaam.

Mbali na Dk. Fenella, kikao hicho pia kilihudhuriwa na naibu wake, Amos Makalla, ambaye TFF ilikuwa haitaki ishiriki.

Akizungumza na Burudani mjini Dar es Salaam jana, Makalla alisema waliamua kikao hicho kifanyike jana badala ya leo kama TFF ilivyoomba kwa sababu Dk. Fenella alikuwa akijiandaa kwa safari.

Makalla alisema Dk. Fenella alitarajiwa kuondoka nchini jana kwenda nje ya nchi kikazi.

"Tuliamua kikao kifanyike leo (jana) kwa sababu ilikuwa muhimu waziri ahudhurie kabla ya safari yake,"alisema Makalla.

Naibu Waziri alisema katika kikao hicho, hoja mbalimbali zilijadiliwa na serikali imetoa mapendekezo kuhusu nini kifanyike ili kutatua mgogoro huo.

Hata hivyo, Makalla hakuwa tayari kutaja mapendekezo hayo na kumtaka mwandishi wa gazeti hili kuwasiliana na viongozi wa TFF ili wazungumzia jambo hilo.

Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah hakuweza kupatikana jana kuzungumzia mapendekezo hayo kwa vile hakuwa akipokea simu yake ya mkononi.

Ofisa Habari wa shirikisho hilo, Boniface Wambura alisema asingeweza kuzungumza lolote kwa vile alikuwa nje ya ofisi. Tenga hakupatikana kwa simu yake ya mkononi.

TFF iliomba kukutana na Dk. Fenella baada ya waziri huyo kuamuru mchakato wa uchaguzi mkuu wa shirikisho hilo uanze upya na kwa kutumia katiba ya 2006.

Dk. Fenella alitoa agizo hilo baada ya kubaini kuwa, mabadiliko ya katiba ya TFF ya 2012 yalifanywa kinyume na sheria ya Baraza la Michezo la Taifa (BMT) na hayakupata baraka za wajumbe wa mkutano mkuu wa shirikisho hilo.

Mgogoro huo uliibuka baada ya Kamati ya Rufani ya TFF kumwengua Jamal Malinzi kuwania nafasi ya urais kwa madai kuwa, hana uzoefu wa uongozi wa miaka mitano kama katiba inavyotaka.

Kufuatia uamuzi huo wa kamati ya rufani, Malinzi aliwasilisha malalamiko kwa Shirikisho la Soka la Dunia (FIFA) kupinga kuenguliwa kwake.

Tayari FIFA imeshaingilia kati mgogoro huo kwa kuahidi kuleta wajumbe wake kufanya uchunguzi kwa kukutana na pande zote zinazohusika kabla ya kutoa ushauri wa nini kifanyike. Ujumbe huo unatarajiwa kuwasili nchini katikati ya mwezi huu.

No comments:

Post a Comment