Katika mechi hiyo ya kundi C iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Taifa Stars ilipata mabao hayo matatu kipindi cha pili.
Mshambuliaji Thomas Ulimwengu, aliyeingia kipindi cha pili badala ya Mrisho Ngassa, alianza kuzitikisa nyavu za Morocco dakika ya 46 baada ya kupokea pasi kutoka kwa beki Erasto Nyoni.
Mbwana Samatta aliiongezea Taifa Stars bao la pili dakika ya 66 baada ya kuambaa na mpira kutoka wingi ya kushoto na kufumua shuti lililompita kipa Lamyagir Dadir.
Samatta, ambaye pamoja na Ulimwengu wanacheza soka ya kulipwa katika klabu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, aliongeza bao la tatu dakika ya 79 baada ya gonga safi kati yao.
Morocco ilipata bao la kujifariji dakika ya 89 lililofungwa na Elarabi Yousser baada ya kipa Juma Kaseja wa Taifa Stars kutema shuti la mchezaji mwingine wa timu hiyo.
Morocco ililazimika kumaliza mchezo huo ikiwa na wachezaji 10 baada ya Abdelaziz kutolewa nje kwa kadi nyekundu na mwamuzi, Neermal Bodhoo wa Afrika Kusini kwa kosa la kutoa lugha chafu.
Kutokana na ushindi huo, Taifa Stars inaendelea kushika nafasi ya pili katika kundi hilo, ikiwa na pointi sita baada ya kucheza mechi tatu.
Ivory Coast, ambayo mwishoni mwa wiki iliyopita iliibamiza Gambia mabao 3-0, bado inaongoza kundi hilo kwa kuwa na pointi saba wakati Morocco imeambulia pointi mbili.
No comments:
Post a Comment