'
Monday, March 18, 2013
WANACHAMA SIMBA WAMNG'OA RAGE, AUFANANISHA MKUTANO WAO NA KIKAO CHA HARUSI
WANACHAMA wa klabu ya Simba jana walitekeleza azma yao kwa vitendo baada ya kutangaza kumng'oa madarakani mwenyekiti wao, Ismail Aden Rage.
Mkutano huo uliofanyika kwenye ukumbi wa Star Light, Dar es Salaam, ulihudhuriwa na wanachama wanaodaiwa kufika 600.
Wanachama hao walipiga kura ya kumkataa Rage kwa madai kuwa, uongozi wake umekuwa ukiendesha klabu hiyo kinyume cha katiba.
Katika mkutano huo, aliyekuwa mwenyekiti wa kamati ya usajili, Zacharia Hanspope na makamu mwenyekiti wa kamati ya fedha, Rahma Al-Kharoos waliteuliwa kuwa viongozi wa kamati ya muda ya Simba.
Jukumu la viongozi hao litakuwa kuisimamia timu hadi michuano ya ligi kuu ya Tanzania Bara itakapomalizika.
Hata hivyo, bado kuna utata kuhusu uhalali wa wanachama waliohudhuria mkutano huo kwa vile hakukuwa na leja ya wanachama kwa ajili ya kuwabaini iwapo ni halali au la.
Vilevile kuna wasiwasi iwapo wanachama hao ni hai kwa vile hakukuwa na mtu wa kuhakiki iwapo wamelipia kadi zao za uanachama kwa mujibu wa katiba.
Mkutano huo uliodumu kwa saa mbili, uliendeshwa na Dk. Mohamed Wandi, ambaye alitoa fursa kwa wanachama kujadili mustakabali wa Simba.
Idadi kubwa ya wanachama walimkataa Rage kwa madai kuwa, ameivuruga timu na amekuwa akisema uongo. Pia waliuelezea uamuzi wake wa kumuuza mshambuliaji Emmanuel Okwi kwa klabu ya Etoile du Sahel ya Tunisia kwamba uliidhoofisha timu.
Akizungumza kwa njia ya simu kutoka India ambako amelazwa kwa ajili ya kupatiwa matibabu, Rage aliufananisha mkutano huo kuwa ni sawa na kikao cha harusi.
Alisema wanachama hao hawana ubavu wa kumng'oa kwa sababu mkutano waliouitisha ulikuwa kinyume cha katiba na baadhi ya wanachama waliohudhuria ni mamluki kwa vile si wanachama wa Simba.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment