KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Tuesday, March 12, 2013

TBL KUDHAMINI TENA BONANZA LA TASWA APRILI 6



KAMPUNI ya Bia Tanzania (TBL) itadhamini bonanza la vyombo mbalimbali vya habari litakalofanyika Aprili 6 mwaka huu viwanja vya Leaders Klabu, Dar es Salaam likiandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA).

Akizungumza katika mkutano na wanahabari kutambulisha bonanza hilo Dar es Salaam jana, Ofisa Uhusiano wa TBL, Doris Malulu alisema huu ni mwaka wa tano mfululizo kwa kampuni yake kudhamini bonanza linaloandaliwa na TASWA na kwamba wamekuwa na matumaini makubwa na chama hicho ndiyo sababu wanakubali kushirikiana nacho kila mwaka.

Malulu alisema zaidi ya Sh. Milioni 50 zitatumika kwa ajili ya bonanza hilo na kusisitiza kuwa lengo la kampuni yake ni kuona linakuwa na mafanikio makubwa kuliko mengine yaliyopita.

“Wanahabari ni wadau wetu wakubwa, hivyo kupitia TASWA tunaona ni njia nzuri ya kutuunganisha na kukaa pamoja kutafakari masuala mbalimbali,” alisema Malulu.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa TASWA, Amir Mhando aliishukuru TBL kwa udhamini huo na kusema kuwa zaidi wa washiriki 1,500 wanatarajiwa kuhudhuria tamasha hilo linaloandaliwa na TASWA kila mwaka likijulikana kama Media Day Bonanza.

“Lengo la bonanza letu ni kuwaweka pamoja waandishi wote wa habari bila kujali ni wa siasa, michezo, uchumi, afya na mambo mengine pamoja na wafanyakazi wa vyombo mbalimbali vya habari, ili kubadilishana mawazo na kufurahi pamoja,” alisema.

Alieleza kuwa bonanza hilo litaambatana na michezo mbalimbali itakayohusisha vyombo vyote vitakavyoshiriki na pia kutakuwa na burudani ya muziki kutoka katika moja ya bendi kubwa za muziki wa dansi hapa nchini, ambayo itatangazwa siku zijazo.

Bonanza la mwaka jana lilifanyika ukumbi wa Msasani Beach Klabu, ambapo mgeni rasmi alikuwa Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, ambaye pia ni Mbunge wa Urambo Mashariki na aliyekuwa Spika wa Bunge la Tisa, Samuel Sitta.

Pamoja na mambo mengine, Sitta alikabidhi zawadi za vikombe na medali kwa washindi mbalimbali walioibuka siku hiyo, pia alipata fursa ya kuzungumza na washiriki zaidi ya 1,500 wa bonanza hilo.

No comments:

Post a Comment