'
Thursday, March 14, 2013
BRANDTS: MECHI ZOTE ZILIZOSALIA KWETU NI FAINALI
KOCHA Mkuu wa Yanga, Ernie Brandts ametamba kuwa, mechi zote zilizosalia katika michuano ya ligi kuu ya Tanzania Bara kwao ni sawa na fainali hivyo hawawezi kuzipuuza.
Brandts alisema hayo baada ya mazoezi ya timu hiyo yaliyofanyika juzi kwenye uwanja wa Mabatini uliopo Kijitonyama, Dar es Salaam.
Kocha huyo alisema wanaipa uzito mkubwa mechi kati yao na Ruvu Shooting itakayochezwa keshokutwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kwa vile wapinzani wao si timu ya kubeza.
Katika mechi ya kwanza kati ya timu hizo iliyochezwa Oktoba 20 mwaka jana, Yanga iliichapa Ruvu Shooting mabao 3-2.
Yanga inaongoza ligi hiyo kwa kuwa na pointi 45 baada ya kucheza mechi 19 wakati Ruvu Shooting inashika nafasi ya sita ikiwa na pointi 29 baada ya kucheza mechi 18.
"Ninakiandaa kikosi changu kuhakikisha kinapata pointi tatu katika kila mchezo ili kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa,"alisema Brandts.
"Kila mchezo tunaocheza kwa sasa ni fainali kwetu, kila timu inahitaji kupata pointi ili kujiweka katika nafasi nzuri, na sisi pia tunahitaji kupata pointi tatu katika kila mchezo. Nadhani mechi itakuwa ngumu,"aliongeza kocha huyo.
Katika mechi yake iliyopita, Yanga iliwalaza ndugu zao wa Toto African bao 1-0. Mechi hiyo ilipigwa wiki iliyopita kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Wakati huo huo, daktari wa Yanga, Nassoro Matuzya amesema wachezaji Kevin Yondan na Saidi Bahanuzi wameanza mazoezi na wenzao baada ya kuwa majeruhi kwa siku kadhaa.
Nassoro alisema Yondan alikuwa akisumbuliwa na maumivu ya kidole gumba, aliyoyapata katika mechi dhidi ya Toto African wakati Bahanuzi alikuwa akisumbuliwa na maumivu ya msuli wa kisigino.
Daktari huyo alisema pia kuwa, beki Ladislaus Mbogo ameshafanyiwa upasuaji wa uvimbe shavuni na hali yake inaendelea vizuri.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment