KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, March 7, 2013

MECHI TANO ZA YANGA KUIVUA UBINGWA SIMBA



YANGA inaweza kuivua ubingwa Simba iwapo itashinda mechi zake tano kati ya nane zilizosalia za michuano ya ligi kuu ya Tanzania Bara.

Msimamo wa ligi hiyo unaonyesha kuwa, iwapo Yanga itashinda mechi hizo, itafikisha pointi 57, ambazo Simba haitaweza kuzifikia.

Simba, ambayo kwa sasa inazo pointi 31 baada ya kucheza mechi 18, imesaliwa na mechi nane na iwapo itashinda zote, itakuwa na pointi 54.

Yanga, inayoongoza kwa kuwa na pointi 42 baada ya kucheza mechi 18, iwapo itashinda mechi zake zote nane zilizosalia, itafikisha pointi 66, ambazo hakuna timu inayoweza kuzifikia.

Ushindani wa kuwania ubingwa wa ligi hiyo kwa sasa upo kwa Yanga na Azam yenye pointi 36 baada ya Simba kupoteza matumaini hayo kutokana na kuvurunda.

Mechi tano za Yanga, ambazo ikishinda zote itaivua ubingwa Simba ni dhidi ya Toto African (keshokutwa), Ruvu Shooting (Machi 16), JKT Ruvu (Machi 21), Polisi Moro (Machi 30) na JKT Oljoro (Aprili 10).

Mechi zingine zilizosalia kwa Yanga ni dhidi ya Mgambo JKT (Aprili 13), Coastal Union (Mei Mosi) na Simba (Mei 18).

Kwa upande wa Simba, imesaliwa na mechi nane dhidi ya Coastal Union (Machi 10), Kagera Sugar (Machi 27), Toto African (Machi 30), Azam (Aprili 13), Ruvu Shooting (Aprili 25), Polisi Moro (Aprili 28), Mgambo JKT (Mei 8) na Yanga (Mei 18).

Wakati huo huo, Kocha Msaidizi wa Yanga, Fred Felix Minziro amesema timu yake imepata mafanikio makubwa msimu huu kutokana na kucheza mfumo wa kiulaya.

Akizungumza na Burudani mjini Dar es Salaam jana, Minziro alisema Kocha Ernie Brandts amekuwa akiwafundisha wachezaji wa timu hiyo mfumo wa kiulaya, ndiyo sababu kiwango chao kipo juu.

Minziro alisema Yanga ya sasa siyo ile iliyocheza mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo kutokana na wachezaji kushika vyema mafunzo ya kocha huyo na kucheza pasi za uhakika.

"Tatizo pekee linalotusumbua kwa sasa ni washambuliaji wetu kupoteza nafasi nyingi za kufunga mabao,"alisema kocha huyo.

Aliusifu uongozi wa Yanga kwa uamuzi wake wa kuipeleka timu kambini nchini Uturuki na kuongeza kuwa, kambi hiyo imesaidia kuwabadili baadhi ya wachezaji.

No comments:

Post a Comment