KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Sunday, March 31, 2013

YANGA YAWAONYA WAFANYABIASHARA



KLABU ya Yanga imewaonya wafanyabiashara wanaotengeneza na kuuza bidhaa mbalimbali zenye nembo ya klabu hiyo bila idhini ya uongozi.

Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga, Lawrence Mwalusako alisema mjini Dar es Salaam wiki hii kuwa, kufanya hivyo ni makosa kisheria na kwamba wahusika watachukulia hatua.

"Kwa miaka mingi sasa, kumekuwepo na tabia kwa wafanya biashara mbalimbali hapa nchini na nje ya nchi kujihusisha na utengenezaji, uingizaji na uuzaji wa bidhaa zenye nembo ya Yanga.

"Yanga inapenda kutoa angalizo kuwa tabia hiyo iliyokithiri ni ukiukwaji wa sheria na unaikosesha klabu mapato halali, ambayo ingeyapata kutokana na matumizi ya nembo yake,"alisema Mwalusako.

Kaimu Katibu Mkuu huyo alisema, nembo ya Yanga iliyosajiliwa rasmi kwa msajili Juni 2, 2009, inamilikiwa na klabu hiyo hivyo hairuhusiwi kwa mtu mwingine kuitumia bila ridhaa ya uongozi.

"Kwa mantiki hiyo, Yanga inatangaza rasmi kuwa ni marufuku kwa kampuni, mtu binafsi au kikundi chochote kutengeneza ama kuuza bidhaa zenye nembo ya Yanga bila ridhaa ya klabu.

Iwapo itatokea mtu yeyote kukiuka amri hii, uongozi utachukua hatua kali za kisheria ili kuikomesha,"alionya Mwalusako.

Kiongozi huyo wa Yanga amewashauri wafanya biashara wanaotaka kutengeneza na kuuza bidhaa zenye nembo ya klabu hiyo, kuwasiliana na uongozi ili wapewe haki hiyo kisheria.

Alisema mfanya biashara atakayekubali kufikia makubaliano na uongozi, atakubaliwa kutengeneza ama kuingiza bidhaa hizo kwa malipo maalumu.

Hata hivyo, Mwalusako alionya kuwa, lazima bidhaa hizo ziwe zenye kiwango na ubora, ambao utakubaliwa na kupitishwa na uongozi wa Yanga.

Mwalusako ametoa mwito kwa wanachama na wapenzi wa Yanga kutonunua bidhaa zozote zenye nembo ya klabu hiyo iwapo muuzaji hajaruhusiwa na uongozi kufanya hivyo.

No comments:

Post a Comment