KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, March 14, 2013

BURIANI KILAMBO ATHUMANI



Marehemu Kilambo Athumani alipokuwa akiumwa kansa ya koo

Marehemu Kilambo Athumani (katikati) akiwa na wachezaji wa zamani wa Pan African, Saad Matheo (kushoto) na Kitwana Manara. Kulia ni mmoja wa wanachama maarufu wa Pan African
Kilambo Athumani  (wa pili kushoto waliosimama) akiwa na kikosi cha Yanga kilichokwenda Brazil miaka ya 1960. Hapa ni kwenye uwanja wa Macarana.

MWANASOKA mkongwe wa klabu ya Yanga ya Dar es Salaam, Kilambo Athumani amefariki dunia.

Kilambo (75) alifariki dunia usiku wa Jumapili iliyopita nyumbani kwake Mwananyamala mjini Dar es Salaam na kuzikwa katika makaburi ya Kisutu.

Kocha huyo wa zamani wa Pan African, alifariki dunia baada ya kuugua kwa muda mrefu ugonjwa wa kansa ya koo.

Mazishi ya mwanasoka huyo mkongwe yalihudhuriwa na wanamichezo mbalimbali, wakiongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jakaya Kikwete.

Kabla ya kifo chake, Kilambo aliwahi kujitokeza hadharani kupitia kwenye vyombo vya habari, akiomba apatiwe msaada wa fedha ili aweze kutibiwa ugonjwa huo.

Wapo waliosikiliza kilio chake na kumsaidia, lakini wengine kutokana na kutokuwa na uwezo, walishindwa kufanya hivyo.

Kilambo atakumbukwa na mashabiki wengi wa soka nchini waliowahi kumshuhudia akiichezea Yanga na timu ya Taifa, Taifa Stars miaka ya 1960 na 1970.

Alikuwa beki kisiki wa Yanga, aliyekuwa akicheza nafasi ya ulinzi wa pembeni kulia. Baadhi ya wachezaji aliocheza nao Yanga ni pamoja na Maulid Dilunga, Leonard Chitete, Omar Kapera, Hassan Gobosi, Muhidin Fadhili, Sunday Manara, Kitwana Manara, Abdulrahman Juma, Adamu Juma na Gibson Sembuli.

Marehemu Kilambo alizaliwa 1938 wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani na kupate elimu ya msingi katika shule ya Mwamba. Hata hivyo, hakuweza kuendelea na masomo hayo na kujikuta akiishia darasa la pili kutokana na wazazi wake kukosa fedha za kumlipia karo.

Baada ya kukatishwa masomo, Kilambo aliamua kujishughulisha na uvuvi wa samaki. Kila asubuhi na jioni alijumuika na watoto wenzake kucheza kabumbu hadi 1956 alipojiunga na timu ya TANU Boys, iliyokuwa ikimilikiwa na vijana wa TANU wakati huo.

Akiwa katika timu hiyo, alichaguliwa katika kombaini ya wilaya ya Bagamoyo kati ya 1960 na 1962, ambayo ilishiriki katika michuano maalumu ya kuwania Kombe la Dosa, iliyokuwa ikifanyika mjini Morogoro kwa kuzishirikisha timu za wilaya za Mahenge, Kisarawe, Kilosa, Mafia na Bagamoyo.

Mwishoni mwa 1962, Kilambo aliyefariki dunia akiwa na umri wa miaka 75, aliamua kujiunga na kikosi cha pili cha Yanga, ambacho wakati huo kilikuwa kikijulikana kwa jina la African Boys, ambayo aliichezea kwa mwaka mmoja kabla ya kupandishwa kikosi cha kwanza.

Kutokana na uhodari wake wa kutandaza kabumbu, Kilambo aliweza kupata namba ya kudumu kwenye kikosi cha kwanza cha Yanga. Wakati huo alikuwa akicheza nafasi ya beki wa kati kabla ya kuhamia nafasi ya beki wa pembeni kulia.

Namba hiyo ndiyo aliyokuwa akiicheza wakati alipoitwa kwa mara ya kwanza kwenye kikosi cha Taifa Stars kabla ya kustaafu kuichezea timu hiyo 1973 kutokana na umri kuwa mkubwa.

Pamoja na kucheza mechi nyingi akiwa na Yanga, Kilambo alikuwa akiukumbuka zaidi mchezo kati yao na Asante Kotoko ya Ghana uliopigwa 1969, ambapo mshindi ilibidi apatikane kwa njia ya kura ya shilingi baada ya timu hizo kutoka sare mechi zote mbili.

Katika mechi ya kwanza kati ya timu hizo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, zilitoka sare ya bao 1-1. Ziliporudiana mjini Accra, timu hizo zilitoka tena sare hiyo ya mabao. Asante Kotoko iliibuka na ushindi huo wa kura ya shilingi.

Baada ya kustaafu kucheza soka, Kilambo alianza kazi ya kuzifundisha timu mbalimbali kama vile Yanga B na Nyota Afrika ya Morogoro, iliyoanzishwa baada ya kumeguka kwa Yanga. Baadaye, Nyota Afrika ilibadilishwa jina na kuitwa Pan African. Aliifundisha timu hiyo hadi 1983.

Kilambo ndiye aliyeiwezesha Pan African kupata mafanikio makubwa katika michuano ya ligi na kimataifa miaka ya 1980.

Ilipofika 1984, kocha huyo aliombwa kuifundisha Asante Tololo iliyokuwa na maskani yake mitaa ya Kariakoo, Dar es Salaam hadi 1988 alipoingia mkataba wa kuifundisha Nyota Nyekundu hadi iliposhuka daraja 1990.

Mwaka uliofuata, Kilambo aliifundisha Cargo iliyokuwa ikishiriki ligi daraja la tatu na kuipandisha hadi daraja la pili.

Marehemu Kilambo aliwahi kuhudhuria kozi mbili za ukocha. Alihudhuria kozi ya kwanza 1977 iliyoendeshwa na Hans Marischna kutoka Hungary kabla ya kuhudhuria kozi nyingine 1986 iliyoendeshwa na Trutman kutoka Ujerumani.

Akihojiwa na Burudani 1997, Kilambo alisema soka ya kulipwa nchini haitawezekana hadi hapo klabu ama taasisi zinazomiliki klabu za ligi kuu, zitakapokuwa na vitega uchumi vya kutosha.

Kilambo alisema ni vigumu jambo hilo kufanikiwa kutokana na klabu zenyewe kutokuwa tayari kufanikisha azma hiyo kwa kuwa nyingi zimetawaliwa na kasumba ya kutegemea misaada kutoka kwa mtu mmoja ama kikundi cha watu wachache.

Alikitaja kikwazo kingine katika kufanikisha azma hiyo kuwa ni klabu nyingi kutawaliwa na migogoro ya mara kwa mara kati ya uongozi na wanachama na hivyo kuchangia kudumaza maendeleo ya mchezo huo.

Marehemu Kilambo alisema mara nyingi migogoro hiyo ilikuwa ikichangiwa na viongozi na baadhi ya wanachama kujali zaidi maslahi yao binafsi badala ya kuendeleza klabu zao.

Akizungumzia kiwango cha soka nchini wakati huo, Kilambo alisema enzi zao walikuwa wakicheza soka ka moyo na kwa lengo la kujipatia umaarufu na kuziletea timu zao ushindi, tofauti na sasa, ambapo wachezaji wengi wameweka mbele zaidi maslahi yao binafsi.

Alisema hali hiyo ndiyo iliyosababisha wachezaji kuhama kila mwaka kutoka timu moja hadi nyingine na kusababisha kiwango chao cha soka kushuka haraka na pia timu kutokuwa na mfumo unaoeleweka.

Kilambo alisema enzi zao ilikuwa vigumu kwa wachezaji kuhama holela kutokana na mapenzi waliyokuwa nayo kwa klabu zao na pia kuhofia kuonekana wasaliti.

"Tulichojali ni upenzi katika timu zetu, tofauti na ilivyo sasa, ambapo wachezaji wamekuwa wakiweka mbele maslahi yao binafsi kuliko mapenzi kwa timu wanazozichezea,"alisema.

Marehemu Kilambo pia alilalamikia tabia iliyokuwa imekithiri kwa viongozi na wachezaji kupanga matokeo ili waweze kujipatia chochote kwa lengo la kukabiliana na makali ya maisha.

Alisema kupanda na kushuka kwa kiwango cha soka nchini kutaonekana kwa wachezaji kuwa na maisha mazuri itakayowawezesha kucheza soka bila matatizo yoyote na pia kutokuwepo kwa migogoro katika klabu.

Mwanasoka huyo mkongwe pia alilalamikia uchezeshaji mbovu wa waamuzi katika ligi za nyumbani, ambao alisema husababisha timu za Tanzania kutolewa mapema katika michuano ya kimataifa.

Marehemu Kilambo ameacha watoto kadhaa. Watoto wake wawili, Ramadhani Kilambo na Athumani Kilambo waliwahi kuzichezea timu za Reli ya Morogoro, Yanga na Coastal Union ya Tanga.

Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pepa.

No comments:

Post a Comment