'
Wednesday, February 20, 2013
SUNZU AKWAMA READING, MATAPELI WALIMPIGA CHANGA LA MACHO
LUSAKA, Zambia
BEKI wa kimataifa wa Zambia, Stoppila Sunzu ameshindwa kupata mkataba katika klabu ya Reading ya England.
Sunzu amekwama kujiunga na Reading baada ya klabu yake ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo kusema kuwa, bado ana mkataba wa kuichezea timu hiyo.
Beki huyo wa kimataifa wa Zambia alimaliza majaribio yake Reading na kufuzu, lakini TP Mazembe ilimzuia kuhama hadi atakapomaliza mkataba wake.
Awali, wakala wa mchezaji huyo alidai kuwa, Sunzu alishamaliza mkataba wake na TP Mazembe na kwamba alikuwa mchezaji huru.
Hata hivyo, klabu hiyo yenye makao makuu yake Lubumbashi imesema, mkataba wa Sunzu unatarajiwa kumalizika 2015.
Reading iliamua kuachana na Sunzu baada ya kuzuka kwa mgogoro wa mkataba kati yake na TP Mazembe.
Uongozi wa TP Mazembe mwishoni mwa wiki iliyopita ulikutana na Sunzu na kujadili suala la mkataba wake.
"Tatizo hilo limeshapatiwa ufumbuzi baada ya kila upande kupitia mkataba wake na mchezaji amekiri kuwa, bado ana mkataba na TP Mazembe hadi 2015," Rais wa TP Mazembe, Moise Katumbi aliieleza BBC juzi.
"Tatizo ni kwamba, washauri wake wamekuwa wakimdanganya ndio sababu alikuwa akituona sisi kama kikwazo kwake. Tunahisi walitaka kuchukua pesa zake zote za ada ya uhamisho kwa kudai kwamba ni mchezaji huru,"aliongeza.
Katumbi alisema TP Mazembe ni klabu ya kulipwa na kamwe haiwezi kuwazuia wachezaji wake kwenda kucheza soka ya kulipwa Ulaya. Alisema jambo la msingi ni kwa wachezaji hao kufuata taratibu.
Rais huyo wa TP Mazembe alisema, siku zote wamekuwa wakitaka Sunzu akacheze Ulaya kutokana na ukweli kwamba, hawakumsajili kwa michuano ya klabu bingwa Afrika mwaka huu.
"Kama kuna klabu yoyote inayomuhitaji, hatuwezi kumzuia kuondoka, lakini klabu hiyo inapaswa kuzungumza na sisi,"alisisitiza Katumbi.
Kwa upande wake, Sunzu aliieleza BBC kuwa, anafurahi kuona suala hilo limepatiwa ufumbuzi.
Sunzu alisema ataendelea kuheshimu mkataba wake na TP Mazembe wakati akiwa anasubiri kupata ofa kutoka klabu za Ulaya.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment