KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Sunday, February 10, 2013

SIMBA YAVUTWA SHARUBU

KAMPENI za Simba kutetea ubingwa wa ligi kuu ya soka ya Tanzania Bara jana ziliendelea kuingia doa baada ya kulazimishwa kutoka sare ya bao 1-1 na JKT Oljoro katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha.

Hiyo ilikuwa sare ya pili mfululizo kwa Simba baada ya wiki iliyopita kulazimishwa sare ya idadi hiyo ya mabao na JKT Ruvu katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mara baada ya pambano hilo kumalizika, mashabiki wa Yanga waliokuwepo uwanjani walilipuka mayowe ya kushangilia huku wakiimba 'Okwi, Okwi, Okwi.'

Kutokana na sare hiyo, Simba imefikisha pointi 28 baada ya kucheza mechi 16, ikiwa nyuma ya Azam yenye pointi 30, ambayo leo inatarajiwa kukipiga na Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam. Yanga bado inaongoza kwa kuwa na pointi 33 huku ikiwa na mchezo mmoja mkononi.

Simba ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya saba lililofungwa na Mwinyi Kazimoto, kufuatia kazi nzuri iliyofanywa na Amri Kiemba na Nassoro Masoud Cholo.

JKT Oljoro ilisawazisha dakika ya 55 kwa bao lililofungwa na Paul Nonga baada ya kuwazidi ujanja mabeki wa Simba, Shomari Kapombe na Kimabil Keita.

Katika mechi nyingine ya ligi hiyo iliyochezwa jana, Prisons iliichapa African Lyon mabao 2-0.

No comments:

Post a Comment