YANGA jana iliendelea kujiimarisha kileleni mwa ligi kuu ya soka ya Tanzania Bara baada ya kuichapa Azam bao 1-0 katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salam.
Ushindi huo uliiwezesha Yanga kuwa na pointi 39 baada ya kucheza mechi 16 huku ikiwa na mechi moja mkononi wakati Azam ni ya pili ikiwa na pointi 36 baada ya kucheza mechi 17. Simba ni ya tatu ikiwa na pointi 31.
Kiungo Haruna Niyonzima ndiye aliyepeleka majonzi kwa mashabiki wa Azam baada ya kuifungia Yanga bao pekee na la ushindi dakika ya 31. Alifunga bao hilo baada ya gonga safi kati yake na Hamisi Kiiza.
Pambano hilo lilikuwa na burudani ya aina yake kutokana na timu zote mbili kuonyesha soka ya ufundi, hasa katika safu ya kiungo na ulinzi. Katika safu ya ushambuliaji, ukosefu wa umakini ndio uliokuwa kikwazo kuzikosesha kupata mabao.
Mshambuliaji Jerry Tegete aliikosesha Yanga mabao mengi wakati alipobaki yeye na kipa Mwadini Ally wa Azam mara tatu. Kipa huyo ndiye aliyekuwa nyota ya mchezo kutokana na kuokoa mipira mingi ya hatari.
Mwamuzi Abdalla Hashim wa Dar es Salaam alijikuta akiingia kwenye matatizo na wachezaji wa Azam kutokana na maamuzi yake kuwa ya kutatanisha. Baada ya pambano hilo kumalizika, mwamuzi huyo alilazimika kuokolewa na askari wa kutuliza ghasia (FFU) baada ya wachezaji wa Azam kumvamia.
Katika mechi nyingine ya ligi hiyo iliyochezwa jana, Prisons ilishindwa kutambiana na Polisi Moro baada ya kutoka suluhu katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.
JKT Mgambo iliutumia vyema uwanja wake wa nyumbani baada ya kuichapa JKT Ruvu bao 1-0 katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga.
Bao pekee na la ushindi la Mgambo JKT lilifungwa na Fully Maganga dakika ya 25.
No comments:
Post a Comment