KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, February 28, 2013

TOURE: MAN CITY HAIWEZI KUFANANA NA BARCELONA



LONDON, England
KIUNGO Yaya Toure wa klabu ya Manchester City ameonya kuwa, itakuwa vigumu kwa timu hiyo kupata mafanikio katika ligi kuu ya England kwa kuiga staili ya Barcelona.

Toure (29) amesema hayo kufuatia mpango ulioandaliwa na Manchester City wa kuanzisha timu za vijana na pia kuiga staili ya uchezaji ya miamba hiyo ya soka duniani.

Katika kutimiza azma hiyo, tayari Manchester City imeshawaajiri Mtendaji Mkuu, Ferran Soriano na Mkurugenzi wa Soka, Txiki Begiristain kutoka Barcelona.

Toure, ambaye kwa sasa ndiye mchezaji ghali kuliko wote katika klabu ya Manchester City, aliichezea Barcelona kwa miaka mitatu akiwa na kina Xavi, Andres Iniesta na Lionel Messi na kuiwezesha kutwaa taji la ligi ya mabingwa wa Ulaya 2009 kabla ya kuhamia England mwaka juzi.

Manchester City imepanga kusajili wachezaji nyota wenye umri mdogo kutoka sehemu mbalimbali duniani na kuwapeleka katika kituo chake maalumu cha kukuza soka.

Hata hivyo, Toure ameukosoa mpango huo kwa kusema, itakuwa vigumu kwa Manchester City kumudu kucheza soka ya pasi nyingi inayochezwa na Barcelona katika ligi kuu ya England.

"Sifikirii iwapo itakuwa sahihi kucheza kama Barcelona kwa sababu ligi kuu ya England ni tofauti na soka ya Hispania,"alisema Toure alipohojiwa na gazeti la Daily Mail la Uingereza wiki hii.

"Kiwango cha soka cha Hispania kipo juu na soka yake inachezwa kwa ufundi mkubwa. Ukiwa England, unahitajika kuwa na kila kitu, nguvu, stamina na mbio,"aliongeza.

Toure alisema pia kuwa, katika ligi ya England, wachezaji wanatumia ngumu zaidi kuliko Hispania na kwamba si rahisi kwa mchezaji kumiliki mpira na wakati huo huo kumtazama mwenzake yupo wapi.

"Unapaswa kuwa mwepesi katika maamuzi, vinginevyo mchezaji kama Kyle Walker (wa Tottenham) atakuangusha. Hapa England, wachezaji wanacheza kwa kutumua nguvu zaidi. Unapaswa kupigania kila mpira na kuwa wa kwanza katika kila tukio, tofauti na Hispania na Italia,"alisema kiungo huyo wa kimataifa wa Ivory Coast.

Toure ameibuka kuwa shujaa wa Manchester City tangu alipojiunga na klabu hiyo 2010 kwa malipo ya pauni 240,000 kwa wiki na kuifungia bao la ushindi katika mechi ya fainali ya Kombe la FA dhidi ya Stoke City mwaka uliofuata, lililofuta ukame wa mataji uliodumu kwenye klabu hiyo kwa miaka 35.

Kocha Mkuu wa Manchester City, Roberto Mancini amemwelezea kiungo huyo kuwa ni mchezaji muhimu na wa aina yake na aliyesababisha kiwango cha timu hiyo kubadilika Januari mwaka huu alipokwenda kushiriki katika michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika.

Makocha kadhaa wanaofundisha klabu za ligi ya Hispania wamekuwa wakihusishwa na mipango ya kurithi kibarua cha Mancini, akiwemo Manuel Pellegrini wa Malaga.

Manchester City mwishoni mwa wiki iliyopita ilifufua matumaini ya kutwaa ubingwa wa England baada ya kuichapa Chelsea mabao 2-0.

Kabla ya ushindi huo, matumaini ya Manchester City kutwaa taji hilo yaliingia doa baada ya kupigwa mweleka wa mabao 3-1 na Southampton.

Akizungumzia mchezo huo, Toure alisema kucheza na timu ngumu kama Chelsea ilikuwa rahisi kwa Manchester City, inayoundwa na nyota wengi kuliko kucheza na timu kama Southampton.

"Napenda kucheza mechi ngumu. Baadhi ya wakati ni kwa sababu ya mashabiki na wakati mwingine kwa sababu ya kiwango cha soka,"alisema nyota huyo.

"Mechi ngumu ni zile dhidi ya klabu kama Chelsea, Manchester United, Tottenham, Liverpool. Tunapaswa kuonyesha uwezo wetu katika mechi za aina hii. Lakini Chelsea sio timu nyepesi kuifunga,"aliongeza.

Toure alisema siku zote wapinzani wao wamekuwa wakicheza kwa kukamia kutokana na timu yake kuwa mabingwa wa ligi hiyo. Alisema unapokuwa mwanamichezo, unapaswa kushinda mechi zote.

Mwanasoka huyo amecheza soka katika nchi tano tofauti. Alianzia Ubelgiji, Ukraine, Ugiriki, Hispania na sasa England. Aliondoka Afrika tangu akiwa mdogo.

Toure alisema anapenda kuendelea kubaki Manchester City baada ya mkataba wake wa sasa kumalizika mwaka 2015, licha ya kaka yake, Kolo Toure kusema kuwa, ataondoka mwishoni mwa msimu huu.

Alisema hajawahi kuichezea klabu yoyote kwa zaidi ya miaka mitatu, lakini hali ni tofauti England kwa vile anataka kubaki Manchester City kwa miaka mingi zaidi.

"Unaweza kubadilika pale unapokosa furaha na kitu fulani. Manchester City inaundwa na wachezaji wenye mvuto kama David Silva na Sergio Aguero na mashabiki wanafanya vitu vya kuvutia.

"Kila wiki wanaimba nyimbo na kutaja jina lako na wapo karibu na klabu. Siku zote mashabiki wamekuwa wakijaribu kutusaidia na hiki ni kitu cha aina yake,"alisisitiza.

No comments:

Post a Comment